Monday, 20 February 2017

POKEA BARUA YANGU BELINDA- MTUNZI: ELIAS MWALONGO



Pokea Barua Yangu
BELINDA
Na Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo(KANTON)
Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU)
Simu: 0769313224
TUMA NAMBA YAKO NIKUTUMIE AUDIO YA SIMULIZI HII USIKILIZE BURE KABISA IKISIMULIWA NA HILALI ALEXANDER TUHUNDWA
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
Si hali yangu ya kawaida, lakini imenipasa kuizoea !!
Belinda, nimeshazoea sasa. Ni mwaka mmoja sasa umepita. Nimenawa machozi kwa muda mrefu sana nikikulilia mpenzi wangu, maumivu yakaja kutulia. Asante Mungu!
Belinda, tukio la leo limenifanya niikumbuke siku ile nilipochota mchanga kwa kiganja changu na kuutupa ndani ya kaburi lako.
Nimekumbuka pia ulivyofungwa kama pipi kwenye sanda, ukawekwa kwenye jeneza la saizi yako, na jeneza likabebwa juu juu mpaka makaburini. Ukazikwa, na watu wakalishindilia kaburi lako kwa visigino mbele ya macho yangu ishara tosha kwamba hata ungefumbua macho ili uniage, usingeweza kuniona tena.
Nililia machozi siku ile kama mtoto mdogo aliyenyang`anywa mdoli wake wa kuchezea. Uso mzima nilinawa machozi. Kamasi nazo zilichungulia kwenye matundu mawili ya pua zangu, kana kwamba zilitaka pia kushuhudia mazishi yako mpenzi wangu. Miguu ilikufa ganzi nisiweze kusimama bila kushikiliwa. Uliniacha sina hali jamani mpenzi wangu.
Belinda, tangu umeniacha, leo limenikuta jambo jingine la kusikitisha na kunivunja mtima wangu, ndilo lililonifanya nichukue kalamu yangu, nikae kwenye kigoda nikuandikie barua, ujumbe ukufikie, huko uliko. Naomba pokea barua yangu Belinda.
Nilikupenda sana Belinda, lakini Mungu alikupenda zaidi. Mipango yote ya kimaisha ambayo tuliipanga kuifanya pamoja hatujatekeleza hata kiduchu. Tulimwomba Mungu atujalie watoto wanne waizunguke meza yetu na kuipamba nyumba yetu, Belinda, umeniacha bila hata mtoto mmoja. Tulipanga tuyajenge maisha yetu, lakini umeniacha natangatanga peke yangu kwenye dunia hii ya shuruba. Kila tulichokipanga kimevurugwa na mauti yako. Ukaniacha ninalia machozi, hata nikatamani na mimi nijifie. Ukizingatia ndo kwanza tulikuwa tunaanza maisha yetu na penzi letu lilikuwa ndo linachipua. Ugonjwa uliokuvamia ghafla ukaitoa roho yako.
Mama yangu ndiye aliyebaki kuwa mfariji wangu. Akanifariji nikapoa moyoni, akanifuta machozi mwanae nami nikatulia tuli. Nafsi ikakubaliana na yote yaliyokuwa yametokea.
Belinda, naandika barua hii kwa masikitiko kukutaarifu kuwa mama yangu kipenzi aliyekupenda, Mungu amemchukua leo alfajiri. Roho yake imemrudia mwenyezi aliyeiumba na mwili wake umerudishwa mavumbini ulikotoka. Jaribu kupata picha moyo wangu ulivyopondeka na kuishiwa pozi maskini mimi.
Ulikuwa kitulizo changu ukaenda zako ghafla bila hata kuniambia “kwaheri”. Mama aliyebaki kuwa mfariji wangu naye leo ameenda. Achilia mbali baba yangu aliyenitoka ningali bado mdogo kabisa kwa ajali ya basi asiniachie hata mdogo wangu.
Kwa hali hii nani atakuwa mhimili wangu katika kumalizia kipande cha maisha kilichobaki?. Niko wakati mgumu Belinda, hasa nikikumbuka upendo wako, na mikakati yetu tuliyoipanga ambayo sasa imepotelea hewani. Nikimkumbuka mama yangu kipenzi, masalale! Ninahisi kama vile sina la kulifanya tena hapa duniani, na kama litakuwepo basi halitakuwa la maana tena kwangu. Hata hivyo natamani ujumbe huu ukufikie huko uliko. Nami naendelea kuganga na maisha hata pale Mola atakapona inatosha. Naomba uniombee niweze kukabiliana na yote ya ulimwengu huu shupavu. Namwachia Mola aliye asili wa yote. Naweka kalamu yangu chini naomba pokea barua yangu Belinda. 
KARIBU 0769313224 NIKURUSHIE AUDIO YAKE BURE!

1 comment:

NITAKUPENDA DAIMA

Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU) Simu: 0769313224 ____________ Laazizi wangu wa moyo, nat...