Monday, 20 February 2017

DADA`NGU MCHUMBA`NGU-Mtunzi: Elias Mwalongo



DADA`NGU
MCHUMBA`NGU
________________________________________________________________













Mtunzi: Elias K. Mwalongo(Kanton)
Ruaha Catholic UNiversity(RUCU)
+255769313224

Umri wangu si haba, ni miaka ya kutosha kuitwa mtu mzima. Hata nikimwambia mtu yeyote kuwa nataka kutafuta jiko hatanishangaa. Hata hivyo sasa nimechanganyikiwa akili, kichwani ni maluweluwe matupu. Najaribu kulala ili nipoteze mawazo lakini usingizi ukiisha mawazo yanarudia yaleyale. Ningekuwa mnywaji mzuri wa pombe, basi ningenunua pombe ya kutosha hata viroba vingi au mvinyo, ili ninywe nilewe hata nikizidiwa hadi kufa wacha nijifie tu.

Ninaikumbuka siku ile ya jumamosi nilipomwendea baba yangu aliyekuwa amekaa sebuleni akiangalia TV na nikamwambia kuwa nimepata mchumba na ninampango wa kumwoa endapo wazazi na ndugu wangeridhia.

Nilimweleza wazi baba yangu kuwa nilipata mchumba aitwaye Frida binti wa mzee Lukengelo. Baba alishituka akanikodolea macho, akanisogelea akaongea kwa kuninong`oneza akasema, “Mwanangu, umri wako unakuruhusu kuoa, umeshakuwa mtu mzima mwanangu, lakini chonde nakuomba usimuoe Frida maana, yule ni dada yako kabisa na baba yenu ni mimi ila naomba mwanangu usimwambie mama yako maana yeye hajui.” Nilimkodolea macho baba, Nilitaka kubishia lakini yeye akaendelea, “mwanangu chonde naomba utafute mwingine lakini usimwoe Frida maana ni dada yako na baba yenu ni mimi ila naomba usimwambie mama yako maana yeye bado haelewi hilo.”

Nilifedheheka na kuhuzunika moyoni kusikia kauli ya baba yangu. Kilichoniumiza zaidi ni ile kauli ya kwamba nitafute mwingine nisimwoe Frida, ukizingatia ni binti pekee ambaye nilimpenda kwa dhati, nilimweka moyoni mwangu. Alinipenda nami nilimpenda kwa dhati, mawazo yangu muda wote yalikuwa ni kwake. Nilimpenda sana Frida, yeye ndiye alikuwa ni shibe ya nafsi yangu na faraja ya moyo wangu. Kumkosa Frida maishani mwangu nilihisi ni sawa na kupoteza kiungo kikubwa mwilini mwangu.

Masaa yalienda kwa kasi, siku zikaja na kupita wiki ya kwanza ikapita. Wiki ya pili nayo ikabisha hodi na kunikuta ningali nafurukuta moyoni kwa hofu ya kumkosa Frida maishani mwangu. Msongo wa mawazo ukanikondesha na kunifanya mnyonge kila muda. Lakini ikafika wakati nikaona uvumilivu umenishinda, nisingeweza kuendelea kuficha siri ambayo baba aliniambia. Nilihisi kabisa mpango wangu wa kufunga ndoa na Frida ulikuwa umegonga mwamba. Basi niliamua liwalo na liwe, wacha niyatoe ya moyoni. Niliamua nimwambie Mama ukweli wote ambao baba alinieleza na kunisihi nisimwambie mama ili lisitokee timbwili lolote pale nyumbani. Kumbuka, msiri wa siri ya moyoni ni mwanasiri mwenyewe. Msiri huiweka siri sirini mwake na pango la siri ni moyo. Moyo wenyewe umeumbwa kisirisiri, hata ukiupasua, kamwe hauwezi kukwambia siri ya msiri. Na siri ni siri kwa upande mmoja tu wa mwanasiri, lakini ikishafahamika na wengine hiyo si siri tena. Na hii siri ya baba haikuwa siri tena maana aliniambia mimi, nami nikashindwa kuihifadhi moyoni nikaamua kumwambia mama yangu ili tu kutua mzigo mkubwa niliokuwa nimeubeba moyoni mwangu.

Ni juzi tu nilimfuata mama jikoni na kumkuta akijishughulisha na mapishi kama kawaida yake. Nikamsalimu kwa heshima aliyonifundisha yeye mwenyewe, kisha nikatulia. Yamkini mama aligundua kuwa nilikuwa na neno la kusema. Akanihamasisha niseme shida yangu, nami nikaanza kusema maana ilikuwa ni shida kweli niliyokuwa nayo. Nikamwambia, “Mama mimi nina neno la kusema” akadakia, “ehee sema mwanangu nakusikiliza” Nikaendelea “ Mama mimi nimepata mchumba…” Kabla sijaendelea mama aliweka bakuli lake chini alilokuwa amelishika, akakaa makini kunisikiliza mimi. Nami nikaamua kuanza upya nikasema, “Mama mimi nimepata mchumba, mchumba wangu anaitwa Frida, binti wa mzee Lukengelo, bila shaka unamfahamu! Mama akasema, “ndio, namfahamu vizuri mzee Lukengelo na familia yake yote na huyo binti uliyemtaja namfahamu. Mwanangu umri wako unakuruhusu, mimi naona umefanya uamuzi mzuri. Jipange mwangu, nitamwambia baba yako na sisi wazazi wako tutajipanga vema” Mimi nilikuwa namwangalia tu usoni anavonifagilia, kisha nikasema, “Lakini mama, nimemwambia baba juu ya suala hili amenikataza kabisa nisimwoe Frida, anasema kuwa Frida ni dada yangu na yeye ndiye baba yetu, ila alinionya nisithubutu kukwambia wewe, nami nimevumilia kwa muda mrefu, nimeshindwa kuendelea kuyaweka moyoni..” Niliongea maneno haya kwa hofu nikiogopa timbwili litakalotokea pale.

Hata hivyo nilimwona mama`ngu akitabasamu kwa furaha. Niliponyamaza kuongea akacheka mamangu kwa furaha, akacheza na kudua pale jikoni, akajaa furaha isiyokifani, akaniambia, “mwanangu, Kimfaacho mtu chake, mwoe Frida mie nipate mkamwana. Usijali maneno ya baba yako.” Maneno ya mama yalinifanya niduwae maana sikutegemea kama angenambia vile. Nikabaki nimemkodolea macho mama yangu ambaye alikuwa amejaa furaha tele. Mama akagundua kuwa nilikuwa sina amani moyoni akanambia “mwanangu, mwoe tu Frida mlete ndani, maana kama baba yako amesema yule nae ni mtoto wake basi kwa uhakika Frida sio dada yako maana hata huyo sio baba yako. Kwahiyo, wewe na Frida ni mama tofauti na baba tofauti, hivyo sio dada yako, wewe mwoe tu mlete ndani!” Nilipigwa na butwaa kusikia maneno haya ya mama ambayo wala sikuyategemea.

Huku mama akiendelea na shughuli zake pale jikoni, huku sasa akiwa amejaa furaha, nilisimama kwa muda kisha nikaondoka, kichwani nikiwa na mafuriko ya mawazo hata kuhisi nachanganyikiwa. Nikaondoka na kurudi moja kwa moja chumbani kwangu. Nikajaribu kulala ili kupoteza mawazo ijapo ni bado jioni na chakula cha jioni bado sijala lakini ikashindikana. Usingizi haukupatikani, muda wote mawazo yalinivamia na kujikuta namkumbaka mchumba`ngu Frida. Nakumbuka maneno ya baba yangu, nakumbuka na maneno ya mama yangu, kisha nayalinganisha. Nahisi ubongo umevurugana, sijui hatima ya maisha yangu na mchumbangu Frida. Nami naandika kwa mwandiko huu mbaya maana mikono inatetemeka nataka kuomba ushauri kwako msomaji. Je nifate maonyo ya baba kuto mwoa Frida japo naujeruhi moyo wangu uliopenda, au je mimwoe Frida nimfurahishe yeye na mama yangu?

Ndugu nami nimejikalisha chumbani hapa nimenyong`onyea nangoja ushauri wako ili nikamshirikishe mchumba`ngu Frida.



No comments:

Post a Comment

NITAKUPENDA DAIMA

Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU) Simu: 0769313224 ____________ Laazizi wangu wa moyo, nat...