DAMU YANGU
IMEMWAGWA NA MAMA`NGU
~~~~~~~~~~~~~~~~+++++++++~~~~~~~~~~~~~~~~~
Mtunzi:
Elias K.
Mwalongo (Kanton)
S. L. P 977
Njombe
Simu No: 0769313224
Facebook: Elias Mwalongo
Twitter: Elias
Mwalongo
Instagram: Elias
Mwalongo
______________________
Chapa Ya Pili, Oktoba 2016
Haki
zote zimehifadhiwa. Huruhusiwi kuiga, kupiga chapa, kutafsiri au kukitoa kitabu
hiki kwa jinsi yoyote ile pasipo idhini ya mwandishi wa kitabu hiki au mhariri
wake. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika.
~~~~~~~~~~~~~++++++++++~~~~~~~~~~~~~
Kitabu hiki nimekiandika kwa
heshima ya wale ndugu zangu ambao ninauhakika hawatakisoma. Wale ambao miili
yao ilisharudishwa mavumbini ilikotoka na roho zao zimemrudia Mwenyezi
aliyeziumba:
Marehemu: Elias Mwalongo (Babu)
Cassiana Mwabena (Bibi)
Kalistus Mwalongo (Baba)
Justine Mwalongo (Baba Mdogo)
Osmunda Mwalongo (Shangazi)
Expeditha Mgaya (Binamu)
~~~~~~~~~~~~~++++++++++~~~~~~~~~~~~~
Na Mtunzi:
Elias K. Mwalongo (Kanton)
Utangulizi
Katika kupambana na maisha ya hapa duniani, yametusibu
mengi na mengine yanaendelea kutusibu
kila uchwao. Mengine yanatutia machozi na kutufanya tuone hatustahili kuendelea
kuishi na mengine yanatufanya tutabasamu na kuona maisha yana maana kubwa
kwetu. Kila mmoja wetu anapatwa na yote, ya kumfurahisha na ya kumtia simanzi.
Ndugu jamaa na marafiki zetu tunaoishi nao wanaweza kuwa sababu ya furaha yetu
au huzuni. Inaumiza sana moyoni endapo ndugu yako wa karibu anayeonyesha
kukupenda na kukujali, nawe ukamtumaini, halafu siku ya siku yeye ndiye
anayefanya njama za kukutoa roho.
Ndani ya kijitabu hiki, DAMU YANGU IMEMWAGWA NA MAMA`NGU,
nimeandika simulizi ya kusisimua, ambapo Rebeka, binti mdogo wa darasa la tano,
anauawa kikatili na kukatwakatwa vipandevipande na mama yake wa kambo ambaye
alikuwa anaishi naye kwa furaha akionyesha kumpenda kwa dhati.
Hakika ukisoma simulizi hii utaiafiki kauli yangu
niliyoitaja katika kitabu changu kilichopita kinachoitwa MACHO YANGU
YANANIDANGANYA, kuwa nyumba nzuri si mlango fungua uone ndani, na usimwamini
yeyote, amini kivuli chako.
Hakika Kikulacho ki nguoni mwako na rafiki yako
unayemchekea ndiye adui yako! Wacha nisikucheleweshe, jisomee mwenyewe uone
mambo…!
Simanzi iliyotufika mtaani kwetu
Ilikuwa siku ya Jumatatu asubuhi na mapema nikiwa
chumbani kwangu, ghafla nilisikia kelele za yowe kutokea kwenye nyumba ya
jirani. Nilishitushwa na kelele hizo, nikasogea kwenye dirisha la chumba changu
ili nisikilize vizuri. Nilisikia, “uwiii, uwiii,uuuuwi mama yetu jamani
tutabaki na nani…jamani Mama Rebeka, umemwacha mwanao atatunzwa na
nani…uuuuwi….” Nilijawa hofu nikaogopa hata kutoka mlangoni. Nilibaki mle
chumbani nikifikiria kwa hofu. Lakini nilikuwa nimekwisha kujua ni Mama Rebeka
aliyefariki. Lakini nilikuwa kama siamini kuwa ni yeye kwani kuna kipindi
alikuwa anaumwa lakini alishapona kabisa na aliruhusiwa kurudi nyumbani. Pia
mume wake alisafiri kikazi akijua hali ya mke wake ni njema kabisa na
anaendelea vizuri.
Huku nikiendelea kusongwa na mawazo yaliyosukwa na hofu
kubwa nilisikia kelele za yowe zinazoashiria kuwepo na msiba ziliongezeka
ghafla, kumbe hata majirani sasa walikuwa wanaanza kumiminika pale nyumbani
pale kwa Marehemu Mama Rebeka. Nami nikapiga moyo konde, nikafungua mlango wa
chumba changu nikatoka taratibu nikipepesa macho huku nikiwa nimejawa na mshangao
kwa yale yaliyokuwa yanaendelea asubuhi ile pale mtaani kwetu. Nikaungana na
watu wengine waliokuwa wanaelekea kule nyumbani kwa Mzee Mlowe ambaye pia
alifahamika kama Baba Rebeka. Tulipofika tulikuta tayari watu wengi wamejaa
pale uwanjani, wote wakiwa na nyuso za huzuni. Pembeni hivi karibu na bustani
watu wengine wanaume walikuwa wametingwa wanachakarika kusogeza miti ya
kujengea jukwaa. Pale uwanjani ulikokwa moto na wengi walikuwa wameuzunguka
moto maana kulikuwa na baridi sana asubuhi ile.
Mimi nikiwa pale uwanjani jirani na moto nilikuwa
nasikiliza kwa makini minong`ono ya watu waliojaa pale nje huku mimi nikiwa
kimya sichangii hoja yoyote maana sina uhakika kama ni Mama Rebeka aliyefariki
na nini kimemsibu. Mama mmoja ambaye ni jirani yetu na ambaye mtoto wake Gloria
nilikuwa nasoma nae darasa moja, kwa sauti ya chini ya wasiwasi na majonzi
alisema, “…mama huyu ameteseka sana kwa homa yake. Walimwambia ana Maleria,
mara vidonda vya tumbo, mara kisukari, mara kifua kikuu,japo alitibiwa akapona
na aliruhusiwa kufaanya hata kazi ndogo ndogo za nyumbani. Hata hivyo jana
jioni nilipitia kumsalimu aliniambia hali yake inabadirika, anahisi kuishiwa
nguvu, na maumivu kwa mbali mwili mzima. Nilimsihi apumzike kwanza halafu kama
hali itazidi kuwa mbaya asubuhi nitamsindikiza hospitalini akapimwe. Ilipofika
saa kumi na moja alfajiri nikajaribu kumpigia simu nikakuta haipokelewi.
Nikajua huenda amezidiwa, nikakurupuka mbio hadi hapa nikabisha hodi mara
kadhaa bila kujibiwa nikaamua kuingia tu, masalale! nikamkuta amejilaza
kitandani kimya kama vile amelala fofofo nikajaribu kuita mara kadhaa tena kwa
sauti baadaye hata kwa kumtikisa lakini ilikuwa ni kazi bure. Hakufungua hata
jicho kunitaza kwa mara ya mwisho, hakutamka hata neno la kuniaga, wala
hakutikisa kiungo chake cha mwili hata kimoja hata kunipungia mkono wa
`kwaheri`. Nilipoendelea kuita kwa sauti kubwa ambayo sasa ilikuwa inageuka
kuwa kilio hakuamka wala kutikisika badala yake aliamka Binti yake wa pekee
Rebeka, ambaye alikuwa amelala fofofo kwenye kitanda kilichokuwa pembeni kidogo
mle chumbani. Kelele zangu ziliishia kumuamsha Rebeka na kushindwa kumuamsha
Mamake licha ya kumtikisa kwa nguvu, kumbe Roho yake ilikuwa imesharudi kwa
aliyeiumba na mwili wake ulikuwa ukingoja saa ya kurudishwa udongoni ulikotoka.
Ili kujiridhisha nikajaribu kusikiliza mapigo ya moyo wake, nikaishia kusikia
mapigo ya moyo wangu yaliyokuwa yanakwenda kasi kutokana na woga. Ghafla moyo
wangu ulikufa ganzi, nikalia kumpoteza rafiki yangu mpendwa, nikalalama moyoni
nikatamani hata kujipiga masumbwi na mimi nife, kwa woga nikapiga yowe mara
kadhaa ndipo majirani wakaanza kutiririka na sasa hapa pamejaa…” Mama Gloria
alimaliza kwa kusema, “Kabinti kake jamani, sijui katalelewaje” Mara nikaona
Mama Gloria akisumbuka kufutafuta mchozi yaliyokuwa yakitiririka mashavuni
mwake. Tuliposikia yaliyokuwa yamejiri, sote tulipigwa na butwaa kwani siku
zilizopita tulikuwa tukimwona Mama Rebeka akiwa mzima kabisa. Homa zake
zilizomsumbua kwa kipindi cha nyuma zilikuwa zimeshapona.
Wakati ule tukiwa tumejaa pale nje, ndugu wa marehemu
walikuwa ndani ya chumba fulani wakilia kwa uchungu wa kumpoteza ndugu yao.
Watu wengine walikuwa wametingwa na pilika pilika za kutuandalia chai sisi
tuliofika msibani pale asubuhi ile. Watu wengine niliwaona wakiwa wanachota
maji toka kisimani kuleta pale msibani.
Ilipofika saa nne asubuhi Baba Rebeka alifika pale
nyumbani ambapo sasa palikuwa pamefurika ndugu na majirani wakibubujika
machozi. Alikuwa amearifiwa jioni kuwa hali ya mke wake imebadilika, si nzuri
tena hivyo aliahirisha safari yake akaanza kurudi. Ilipofika alfajiri alitumiwa
ujumbe na majirani kwa njia ya simu kuwa alikuwa amempoteza mke wake, hivyo
alipofika hakushangaa umati ule wa watu kwani alikuwa anajua kinachoendelea.
Alishuka kwenye gari akiwa amevaa miwani myeusi na kofia. Mkononi alishika leso
nyeupe, bila shaka ilikuwa ya kufutia machozi. Alipokelewa na baadhi ya ndugu
zake wakampeleka moja kwa moja ndani ya chumba ambacho walikuwa wamehifadhi mwili wa marehemu Mama
Rebeka.
Baadaye mimi nikaungana na wale waliokuwa
wanajengajukwaa. Tukaendelea kujenga jukwaa mpaka saa sita hivi mchana ambapo
sasa watu wengine walitakiwa kukaa kwenye jukwaa hilo kwani watu walikuwa
wamejaa mno. Wakati tukitengeneza jukwaa watu wengine walikuwa wakichonga
jeneza na wengine walikuwa wanachimba kaburi. Pia wanawake wengine majirani
walikuwa wakiandaa chakula cha mchana
kwaajili ya watu wote waliofika pale msibani.
Ikafika saa nane na nusu hivi baada ya chakula cha
mchana, jeneza lenye mwili wa marehemu
likawekwa pale uwanjani, kisha baba mmoja akatangaza kuwa ulikuwa ni muda wa
kuaga mwili wa marehemu ikiwa ni maandalizi ya mazishi.
Basi alitangulia mume wa marehemu akiwa amemshikilia
mkono mtoto wake aliyekuwa akiangua kilio hali hajui nini kinaendelea kwani
alikuwa bado mdogo. Wakafuata wazazi wa marehemu yaani babu na bibi wa Rebeka,
wakafuata kaka, dada na wadogo zake marehemu. Baada ya ndugu wote wa marehemu kuisha
tukafuata sisi majirani.
Baada ya sisi sote kutoa salamu zetu za mwisho jeneza
likafungwa kisha wanaume fulani wakalibeba tayari kwa kuelekea makaburini.
Tukaanza kwenda makaburini huku tukipokezana jeneza lile mara kwa mara. Karibu
watu wote tukaongozana msururu mrefu kuelekea makaburini kwenye
mazishi.Wanawake wengine walianzisha nyimbo mbalimbali za mazishi.Tulipofika
tukaliweka jeneza nje ya kaburi pembemeni kidogo. Watu waliokuwa wanafuata
nyuma yetu wakafika wote wakazunguka pale kaburini huku wengine wakisimama juu
ya makaburi mengine yaliyokuwa jirani
Mazishi
yaliendelea huku watu wengine hasa ndugu wamarehemu na baadhi ya majrani wakiwa
wanalia kwa sauti. Wanawake wengine walikuwa wa kushikiliwa kwani walikuwa
wakilia kwa sauti, wakijipigapiga, wakijiangusha chini na kugaagaa,
wakijiviringisha na kujitupa chini, puu! Baada ya kuzika wanawake fulani
walianza kulia kwa nguvu, wakijidondosha juu ya kaburi la mama Rebeka.
Nilimgundua dada mmoja wa makamu ambaye alikuwa ni mdogo wake wa marehemu
ambaye alikuwa ametoka kuhitimu elimu yake ya chuo kikuu anasubiri ajira.
Nilifanikiwa kumuona Baba Rebeka akiwa amemshikilia binti yake, Rebeka kwa
mikono miwili huku akiwa amejiinamia kama mtu mwenye msongo wa mawazo na
majonzi. Nilipozidi kumuangalia vizuri nilimwona anajifuta machozi kwa leso
nyeupe aliyokuwa ameishika kwa mkono wake wa kushoto. Mimi niliendelea
kuyashuhudia haya nikiwa nimesimama juu ya kaburi fulani lililokuwa upande wa
juu.
Ukafika wakati wa kuweka mataji juu ya kaburi. Taji la
kwana liliwekwa na mwongozaji wa ibada ile ya mazishi. Akafuata mume wa
marehemu akiongozana na binti yake pekee. Wakafuata wazazi wa marehemu, kisha
wakafuata kaka dada na wadogozake marehemu. Kisha wakamalizia ndugu wengine wa
marehemu kama mjomba, binamu, shangazi, na wengineo. Baadaye mtu mmoja ambaye
bila shaka alikuwa ni ndugu wa marehemu alisoma historia fupi ya marehemu.
Nakumbuka alisema kuwa, marehemu alizaliwa mwaka 1986, amefariki akiwa na miaka
28. Alikuwa ni mkulima wa kawaida. Aliacha mume na mtoto mmoja. Mungu
aipimzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.
Kisha ukatangazwa utaratibu wa kuondoka kuelekea nyumbani
kwa wafiwa kunawa mikoni(kula chakula) basi
tukaanza kurudi taratibu huku wengine wakiendelea kulia na wengine wakiwa
wamenyong`onyea wanaomboleza kwa huzuni.Wanawake wengine wakiwa wamejifunika
kanga vichwani huku wakilia kimyakimya. Tulipofika pale nyumbani tulipokelewa
kwa maji ya kunawa, kisha tukagawiwa sahani za vyakula na kuonyeshwa sehemu za
kukaa. Wakati huu kulikuwa na ukimya pale nyumbani maana sote tulikuwa na
uchungu wa kuondokewa na mwenzetu ghafla vile.
Twiwalala
Jioni ile watu walikuwa bado wamefurika pale nyumbani
baada ya kula chakula cha jioniambacho tulikipata mida ya sa moja hivi jioni.
Watu tulikusanyika makundimakundi tukiota moto. Baadaye tulianza kuimba nyimbo
mbalimbali kama ilivyo kawaida ya misiba mingine. Nyimbo zilipozidikutunogea
baadae tulianza hata kucheza. Kila wimbo ulipoisha ulianzishwa mwingine, na
mimi nilikuwa nazifahamu kwani nilikuwa nimeshawahi kuzisikia mara nyingi tu.
Baadae ukaanzishwa wimbo ambao nilikuwa naupendelea zaidi, unaitwa “Twiwalala”, maana yake “tunapapasa au
tunatafuta”. Ulipoimbwa wimbo huu ni kama vile nilisahau kuwa nipo msibani
maana nilifurahi sana, tulicheza sana huku tukiwa kama vile tunatafuta kitu
kilicho potea. Nakumbuka tuliimba hivi: Twiwalala
u mama vesu(twiwalala) u mama vesu asivoneha(twiwalala) umama vesu ahele
whiya(twiwalala) Maana yake, Tunamtafuta mama yetu (tunatafuta) mama yetu haonekani (tunatafuta) mama yetu ameenda wapi(tunatafuta)…” Kama
ilivyo kawaida ya wimbo huu ukiimbwa,tulianza kwenda tunatafuta hadi makaburini
usiku ule huku tukiimba kwa sauti na vile tukienda tunakimbia viatu vilikuwa
vikisikika tukipiga na makofi kwa kufuata mapigo ya viatu, na sisi ndo
tuliendelea kuimba kwa hisia. Tulikimbia huku tunapapasa kuzunguka kaburi mara
kadhaa huku yowe zikisikika kati yetu, uuuuwii, uuuuuwii! Kwa mwendo uleule
tulioendea tukaanza kurudi nyumbani. Haya yote tuliyafanya saa tano kama sio
saa sita hivi usiku.
Tuliporudi wengine waliendelea kuimba nyimbo nyingine,
ila mimi na wengine tukaanza kusinzia tukatafuta sehemu ya kujilaza hadi jogoo
walipoanza kuwika. Asubuhi ile tulikunywa chai tuliyokuwa tumeandaliwa na baada
ya hapo watu wengine walianza kutawanyika kurudi kwao. Mimi nilikawia kidogo
kuondoka.
Baada ya Msiba kuisha
Siku tatu baada ya msiba wa mama Rebeka, ndugu wote
walikusanyika, ili kufanya tathimini ya tukio hilo lililowakumba na kuwatia
simanzi ndugu wote hata majirani pia. Wazo kuu katika kikao hicho ni juu ya
pengo lililoachwa na marehemu na hasa katika jukumu la kumlea Rebeka binti
pekee wa marehemu, pato la ujanani. Walisema kuwa baba Rebeka hataweza kumtunza
binti yake kwakuwa alikuwa bado ana umri mdogo. Hivyo walikubaliana kuwa Rebeka
akae na bibi yake. Tangu siku hiyo Rebeka aliaza kuishi na bibi yake. Kutokana
na akili yake ya kitoto Rebeka alisahau kabisa tukio la kifo cha mama yake hata
akamzoea bibi yake kwani kila wakati walikuwa pamoja. Rebeka aliendelea kuwa
mchangamfu mwenye busara na mwepesi kuchangamana na wenzake katika michezo yao
ya kitoto.
Baba Rebeka alionekana ni mwenye kukosa furaha kila siku
kutokana na kifo cha mke wake kipenzi, aliyempenda kwa dhati, akafunga naye
ndoa ya kikatoliki watu wakasherehekea. Walianza kuishi kwa furaha, na kupanga
maisha yajayo. Maisha yao yalianza kung`ara, na upendo ulitawala. Na Kwa neema
ya Mwenyezi Mungu walijaliwa kupata mtoto wao wa kwanza, pato bichi la ujanani.
Rebeka binti mnyenyekevu, mwenye sura ya upole, mwenye tabasamu la kujipatia marafiki
tele. Kumbe Mungu ndiye mpaji na mnyimaji, akawanyima nafasi ya kuendelea
kufurahia ndoa hiyo iliyokuwa ikinawili siku hadi siku. Astarehe kwa amani
mbinguni Mama Rebeka!.
Miezi minne baadaye
Miezi minne ilipita, ikawa bado haifahamiki kama baba
Rebeka ataoa mke mwingine au laa. Rafiki zake wengi walikuwa wakimshauri kuwa
aoe tena mke mwingine kwani umri wake ulikuwa bado unaruhusu, alikuwa ni kijana
mchapa kazi mwenye mvuto na heshima zake. Licha ya ushauri na maoni ya watu
mbalimbali Baba Rebeka hakuonyesha dalili zozote za kukubaliana na ushauri wao
au kukataa. Japo watu walikuwa wanasemasema kuwa lazima ataoa mwingine tu.
Kumbe lisemwalo lipo, kama halipo basi liko njiani linakuja na bila shaka litafika.
Baada ya miezi sita tangu kifo cha mama Rebeka, baba
Rebeka akajipatia mke mwingine na bila kukawia akaenda kumtambulisha kwa wazazi
wake kwamba ndiye atakayebadili nafasi ya Mama Rebeka. Wakati wako Sebuleni
yeye Baba Rebeka, Babu na bibi Rebeka, aliingia Rebeka akiwa hajui hili wala
lile alishtuka kuona sura ya baba yake baada ya kupoteana kwa muda mrefu kwani
baba yake alikuwa ni mfanyabiashara huko mjini, na ni mara chache tu aliweza
kufika kusalimu wazazi pale kijijini.
Kwa furaha na bashasha Rebeka alimrukia baba yake
akamsalimu na kung`ang`ania ampakate. Hapo Baba Rebeka alimkumbuka sana mke
wake kipenzi. Alionekana kuwa mnyongeghafla, lakini akapiga moyo konde,
akajikaza kisabuni, akaanza sasa kutabulisha. Akasema, “Wazazi wangu wapenzi,
baba na mama, baada ya kuondokewa na mke wangu, mama Rebeka, sasa Mungu
amenijalia, nimempata huyu ambaye natumaini ndiye atakayenifuta machozi na
kunisahaulisha msiba uliopita. Anaitwa Debora, binti pekee wa Mzee Linus na
mama Theodora wa mjini Makambako. Ninamatumaini makubwa naye. Amesoma japo si
sana. Natumaini atanilelea vizuri binti yangu Rebeka, na kunipatia wadogo zake
Rebeka. Naomba wazazi wangu, mmpokee kwa furaha aingie katika ukoo wetu” Wazazi
wake walitazamana kisha, baba yake akaanza kusema kwa busara, “Mwanetu
umechukua uamuzi ulio bora, hongera sana kwa kumpata Debora ambaye mtatunzana
mkiaminiana na kuheshimiana.Umefanya vema maana peke yako usingeweza kumlea
binti yako huyu, ukizingatia ni mtoto wa kike. Sisi wazazi wako maadamu sisi
ndio tuliotangulia kuliona jua, tutashirikiana pamoja nawe, usiwe na shaka”.
Akamgeukia Debora, mke mpya wa baba Rebeka akamwambia, “Karibu sana Debora
katika ukoo wetu. Sisi ni wazazi wako pia, tutakuwa nanyi bega kwa bega mtuzane
na kuthaminiana katika maisha yenu. Umlee vema Rebeka ili baadaye aje atusaidie
sote.” Debora huku akitabasamu, alitikisa kichwa juu-chini, kuonyesha
kukubaliana na maneno yale yaliyoongelewa.Mazungumzo yaliendelea kwa kitambo
kidogo kisha, baba Rebeka akaondoka na mke wake wakamwacha Rebeka na kwamba
watakuja tena kumchukua baada ya wiki moja.
Debora awa gumzo!
Wiki moja ilipotimia walienda kumchukua Rebeka kwa bibi
yake na kuanza kuishi naye. Maisha ya Rebeka na ma`mdogo wake yalikuwa murua
hata ndugu na majirani walitambua hilo.
Debora alimpenda Rebeka kama binti yake wa kumzaa. Rebeka naye aliishi na
ma`mdogo wake kwa furaha kwani alimzoea na kumchukulia kama mama yake kabisa.
Hali hii ilimpelekea Rebeka kusahau kuhusu marehemu mama yake mzazi.
Miaka miwili baadaye hali yao ya kimaisha ikiendelea kuwa
shwari kidogo, baba Rebeka alinunu gari la kutembelea pia alifungua duka mjini
Makambako. Rebeka nae alikuwa ameshaingia shule ya msingi yuko darasa la pili.
Ma`mdogo alikuwa akimnunulia Rebeka nguo, viatu, pipi, soda, sambusa, ubuyu na
zawadi nyingi kedekede. Licha ya mazuri yote waliyokuwa wakifurahia, familia
hii ilikuwa imepata pigo jingine ambapo iligundulika kuwa Debora, alikuwa tasa,
hivyo hakuweza kushika mimba. Kwa kujitambua hivyo Debora alijitahidi kuonyesha
upendo wake kwa Rebeka. Daima alipenda kuongozana naye katika matembezi yao
hata katika mapumziko. Alitamani na yeye siku moja apakatemtoto wa kumzaa yeye
mwenyewe lakini haikuwezekana kwa kuwa alikuwa tasa.
Hata hivyo hali hii ilimpelekea Debora ajiona ni mwenye
mapungufu makubwa na asiyestahili kati ya jamii yake. Alipokuwa akikutana na
wenzake waliokuwa wakikutana na wenzake waliomsalimu kwa furaha na mizaha naye
alijitahidi kutabasamu kwa uso wa furaha huku akijitahidi kuficha simanzi
iliyokuwa inautafuna moyo wake. Alipokuwa akitembea huku na kule alihisi macho
ya wapita njia wote yanamwangalia yeye kwa dharau, kumbe wala wengine walikuwa
hawajui tatizo lake la utasa. Aliumia sana moyoni maana alihisi kila mtu
anamnyoshea kidole yeye na kumbeza, na kumbinulia midomo, kumbe sivyo. Rafiki
zake waliomtembelea nyumbani aliwapokea kwa furaha lakini moyoni alijaa
simanzi, alikuwa dhaifu moyoni. Hata
hivyo alijitahidi kwa kila namna kuficha simanzi na uvuguvugu wa moyo
wake. Alicheka na marafiki zake, ndugu na majirani japo moyo wake ulisinyaa kwa
hofu ya maneno ya ndugu zake. Hata hivyo aliendelea kumlea Rebeka kwa furaha na
kwa upendo.
Siku zikazidi kusukumana na miezi ikienda kwa kasi ,
maneno ya watu yakaanza kumfikia bila chenga. Walikuwa wakiulizani, huyu wifi
yetu vipi, mbona hatuoni dalili kama siku moja atanyonyesha kama sisi? Huyu
wifi yetu vipi, bado anajipanga tu? Na maneno mengine mengi yalisikika
yaliyozidi kumuumiza sana moyoni. Ndugu wengine wakawa wanasema, “Baba Rebeka
ametuletea nuksi kwenye ukoo wetu. Hili ni balaa halijawahi kutokea kwenye ukoo
wetu. Kabla ya balaa hili halijaenea, amrudishe kwao”. Maneno haya na mengine
mengi ya kejeli yaliyoendelea kuvuma mitaani yaliendelea kumsononesha. Ndugu na
majirani walionekana kutompenda tena, walimjengea fitina na kumfanyia kila
jeuri pengine angeweza kujiondokea mwenyewe. Lakini hakuondoka aliendelea
kuishi pale akimlea Rebeka ambaye sasa
alikuwa darasa la tano.
Alianza kugundulika wazi sasa kuwa daima alikuwa na
msongo wa mawazo. Rebeka nae aligundua kuwa upendo wama`mdogo wake ulikuwa
umepungua kwa kiasi kikubwa. Aliona hamjali tena kama hapo awali.
Baba Rebeka alionekana kutojali sana tatizo la mke wake,
aliamua kukubaliana na hali halisi. Maneno ya wanandugu aliyapotezea na
kuendelea na shughuli zake maadamu Debora alikuwa anamlelea binti yake wa
pekee. Vile vile Baba Rebeka alimtumainia binti yake kuwa ndiye mrithi wa mali
zake. Alitoa matumaini kabisa ya kuoa mke mwingine na kujitafutia watoto kwani
aliona kama vile amepatwa na mkosi. Katika umiliki wa duka lake na gari
aliandika REBEKA, ambalo lilikuwa jina kamili la binti yake.
Debora alijitahidi kuvumilia, aliyahimili maneno na
machukizo ya ndugu na majirani na kuendelea kumpenda Rebeka kwa dhati kama vile
mtoto wake wa kumzaa, lakini yakamshinda, maskini!
Kikulacho ki nguoni mwako
Baada ya miezi michache Debora alionyesha wazi kuwa
aliishusha thamani ya Rebeka. Alionekana kutompenda sana kama hapo awali.
Rebeka naye aligundua kuwa upendo kati yake na mam`dogo wake ulikuwa
umeshuka,japo hakujua ni kwanini. Rebeka alijaribu kujisogeza na kuwa jirani na
mam`dogo wake hata hivyo mdogo wake alionyesha kutomjali kama vile mwanzo.
Baba Rebeka alikuwa akiendelea kuwapenda Debora na Rebeka
binti yake wa ujanani. Kasi ya maneno ya watu juu ya utasa wake yaliendelea
kumpa simanzi. Pia kitendo cha Baba Rebeka kuandika majina ya Rebeka katika kila
mali aliyomiliki ikiwe magari, duka, na vyombo mbali mbali kilimfanya Debora
kuumia zaidi kwani hakuwa na mtoto wa kumzaa ambaye jina lake lingeandikwa
kumiliki mali za baba yake, wala yeye mwenyewe hakuandikwa katika mali yoyote.
Alimwonea wivu sana Rebeka ambaye alikuwa bado binti
mdogo wa miaka 12 akisoma darasa la tano katika shule fulani ya bweni. Rebeka
hakujua kuwa anajengewa chuki na mam`dogo wake.
Wahenga husema, kikulacho ki nguoni mwako, rafiki yako
ndiye adui yako. Kauli hizi zilijidhihirisha katika familia hii ambayo sasa
ilikuwa imejaa wivu, fitina, chuki na sikitiko la moyo. Debora alijaribu
kujitahidi kuonyesha furaha na kumchangamkia Rebeka lakini moyo wake ulikuwa
umefura hasira , umekunja ngumi, tayari unajiandaa kupambana na familia yake.
Hata hivyo hakupenda ifahamike kuwa amejenga chuki moyoni mwake. Hivyo
aliendelea kujisogeza karibu na Rebeka kinafiki tu huku akiendelea kumnunulia
vitu vidogovidogo kama vile madaftari, kalamu, ubuyu, pipi hata nguo pia
alimnunulia.
Maneno ya watu yaliendelea japo sasa walisema,
“inaonekana Debora amelipokea tatizo lake la utasa, amerdhika ameamua kumchukua
Rebeka kama mtoto wake wa kumfariji. Kumbe maskini wa Mungu, Macho
yanadanganya, nyumba nzuri si mlango, fungua uone ndani! Debora alifanya vile
akiwa na lake jambo!
Ziara ya Debora shuleni kwa
Rebeka
Huku akiendelea kuficha chuki iliyokuwa moyoni mwake na
usoni akionesha kuendelea kumpenda Rebeka siku moja aliamua kwenda kumtembelea
shuleni kwake akiwa amembebea nguo, madaftari na fedha ambazo alimwachia za
matumizi, japo Rebeka mtoto mdogo vile hakuhitaji pesa nyingi za matumizi.
Alipofika shuleni pale alipokelewa vizuri akaonana na Rebeka, akaomba nafasi ya
kuongea nae kwa muda mfupi kama mzazi. Kisha akaonyeshwa mazingira ya shule
hiyo na chumba cha Rebeka hata kitanda
chake. Alikuwa analala bweni B chumba namba 3 kitanda cha juu jirani kidogo na
dirisha. Baada ya maongezi hayo ambayo hayakuchukua hata muda wa saa moja, huku
akijionyesha ni mwenye furaha, aliagana na walimu na kisha kuondoka kurudi
nyumbani huku Rebeka akirudi darasani kuendelea na vipindi. Rebeka alifurahi
sana kutembelewa na mama mdogo wake siku ile kwani hakutegemea, pia kwakuwa
alimletea fedha za matumizi. Ziara ya Debora shuleni kwa Rebeka ilimfariji sana
Rebeka, alijawa na furaha na kuhisi upendo wa Debora kwake ulikuwa unaongezeka.
Kumbe usilolijua ni kama usiku wa giza nene na kitanda usichokilalia hujui
kunguni wake. Ziara hiyo ilikuwa na lake jambo, si bure!
Ziara ya kwenda kumsalimu Rebeka, kumtembeza kwenye
mazingira ya shule kumwonyesha bweni analolala hadi kitanda chake lilichukuliwa
kama jambo la kawaida na hakuna aliye hamaki au kupata mashaka yoyote lakini
kumbe zilikuwa ni njama za kufanya mauaji. Kumteketeza binti Rebeka binti wa
watu jamani! Kwakuwa hakuna aliyeshitukia njama hizo, basi mikakati ya
maangamizi iliendelea kufanyika.
“Mama ananiniita!”
Siku iliyofuata Debora alitafuta vijana wa kiume watatu.
Akawaomba wakutane wazungumze juu ya suala hilo. Walipokutana akawapa maelekezo
yote. Aliahidi kuwapa kiasi cha shilingi laki nne kila mmoja endapo
watafanikisha zoezi hilo. Vijana hao bila kusita wala kuomba muda wa kufikiria
juu ya hilo wakasema wako tayari kuifanya kazi hiyo kwa umakini, kwa usahihi
bila kukosea kwani wanauzoefu mkubwa wa kazi hiyo.
Maandalizi yalifanyika, fedha walipewa, mbinu zilipangwa
na siku tatu baadaye, siku ya Jumatano usiku wa sa tano na nusu hivi walikutana
sehemu fulan hao vijana watatu pamoja na Debora. Siku hiyo baba Rebeka hakuwepo
nyumbani alikuwa amesafiri, kufuata bidhaa kwaajili ya biashara yake. Wote
walikuwa wamevaa nguo nyeusi na kujifunika hadi kichwani ili wasigundulike
kirahisi. Debora alikuwa mikono mitupu huku akiwaongoza vijana wake waliokuwa
wamebeba zana mbalimbali walizoona zitawafaa katika katika shughuli hiyo
waliyokuwa wanaiendea.Mmoja alikuwa amebeba panga lenye makali sana, mwingine
alibeba visu viwili kikubwa na kidogo wakati mwenzao alibeba shoka na kirungu
fulani si kikubwa sana.
Wakiongozwa
na Debora walienda mpaka pale shuleni. Walisogea taratibu mpaka pale alipokuwa
anakaa mlinzi wa shule hiyo. Walipofika walikuta amejiegesha pale kibandani
mwake akiwa amesinzia. Wakaamua kurudi nyuma kidogo kisha kupitia njia
nyingine, wakaenda moja kwa moja bwenini kwa Rebeka wakiongozwa na Debora
ambaye alikuwa tayari analifahamu bweni hilo. Wakasogea taratibu pale dirishani
ambapo kitanda cha Rebeka kilikuwa jirani.Kulikuwa kimya kuonyesha kuwa
wanafunzi wote walikuwa wamelala.Hata mlinzi naye alikuwa amesinzia pale
kibandani kwake. Debora akasogea pale dirishani kisha kwa sauti ya chini chini
akaita “Rebeka!Rebeka” Rebeka akashituka kwani alikuwa amekwishagundua kuwa ni
sauti ya mam`dogo wake anayempenda. Akaitika “Abee!” Debora akasema, “njoo hapa
dirishani mwanangu!” Rebeka alipotaka kuamka na kutaka kusogea dirishani,
aliitwa na mwenzake aliyekuwa kitanda
cha jirani, akamwuliza “Rebeka unaenda wapi?” Yeye akasema, “mama ananiita!” basi akasogea
dirishani na akafungua dirisha ili amsikuilize mama yake mdogo ambaye alimsikia
akimwita mara mbili.
Alipotaka tu kuchungulia nje, wale
vijana watatu wakamshika kwa nguvu, wakamvutia nje kupitia pale dirishani na
kabla hawajamtua chini, wakambonda na shoka kichwani mara mbili wakiwa bado
wamemshikilia juujuu, akakata roho palepale binti Rebeka maskini.
Kisha wakaubeba begani
mwili wa marehemu Rebeka kisha wakatokomea kwenye msitu fulani uliokuwa jirani
ambao ulikuwa umefunikwa na giza nene. Huku wale waliokuwa wamelala mle ndani
wasijue kilichokuwa kikiendelea nje ya bweni lao kwani walilala fofofo.
Huko porini
walimkatakata vipande Rebeka binti wa watu asiyekuwa na hatia yoyote. Kisha nao
wakatokomea, wakaenda zao, baada ya kufanya mauaji hayo ya kinyama. Debora nae
alirudi nyumbani ikiwa ni sa saba usiku. Alipofika nyumbani alienda kulala.
Asubuhi yake kama
kawaida yake akaendelea na shughuli zake akijitahidi kuficha uhalifu alioufanya
usigundulike kwa kumtazama tu usoni. Alikuwa akitafutiza furaha na tabasamu kwa
kuongeaongea na watu na kucheka nao. Yeye aliwambia wale vijana wake watatu
kuwa hilo liliofanyika iwe siri yake yeye na wao tu. Maskini Debora, alisahau
kuwa: Msiri wa siri ya moyo ni mwanasiri mwenyewe. Msiri huiweka siri sirini
mwake na pango la siri ni moyo. Moyo
wenyewe umeumbwa kisirisiri, hata
ukiupasua hauwezi kukwambia siri ya mwanasiri. Siri ni siri kwa upande mmoja tu
wa mwanasiri, ikisha sikika kwa wengine hiyo si siri tena. Pia siri ni siri
endapo inataka yenyewe kuwa siri vinginevyo ni kucheza madange tu.
Hakuna marefu yasiyo na
ncha na mbio za sakafuni huishia ukingoni.
Kindumbwendumbwe
shuleni
Kilizuka
kindumbwendumbwe baada ya kuona Rebeka hajaonekana pale asubuhi, iwe bwenini
kwake, wala sehemu nyingine yoyote. Na zaidi ilipofika mida ya saa mbili ambapo
wale wanafunzi walitakiwa kufanya usafi na hasa kufagia viwanja vyao, madarasa
na kudeki vyoo. Wachache walienda porini kuvunja matawi ya miti wayatumie kama
mifagio. Ghafla zilisikika yowe kutoka huko porini, wanafunzi wote waliokuwa
huko walirudi wanakimbia wakiwa wamejaa woga na hofu, wanahema wengine hadi
kulia kabisa kwa kile walichokishuhudia. Wengine walikimbia japo hawakujua
kulikoni. Basi mwalimu aliyekuwa zamu siku hiyo akashuhudia pilikapilika hizo
akawauliza nini kimetokea, binti mmoja aliyefahamika kwa jina la Jane alieleza
alichokiona huko porini, akasema, “Mwalimu, nipokuwa navunja mfagio kule porini
nikaona damu, nilipotaka nigeuke nimwite rafiki yangu Felista nimwambie nikakuta….”
Akashindwa kumalizia akaanza kulia, basi mwalimu huku na yeye akiwa na hofu
akasema twende ukaonyeshe. Wakaenda wakakuta ni mwili wa mtu aliyechinjwa kama
kuku na kukatwakatwa asigundulike alikuwa nani. Basi mwalimu aliamuru kengele
igongwe na wanafunzi wote wakusanyike. Wakati wanafunzi wanakusanyika
mwalimu alienda kuwambia baadhi ya
walimu wenzake kuhusu mkasa uliotokea.Walifanya hesabu ya wanafunzi ikaonekana
Rebeka hayupo pale shuleni. Hapo walikuwa wameshaita polisi kuja kuchunguza
tukio hilo. Pia Mwalimu mkuu alimpigia simu Baba Rebeka na kumtaka afike pale
shuleni pamoja na mke wake. Baba Rebeka kwakuwa alikuwa kwenye shughuli zake za
kibiashara alipopata taarifa hiyo iliyomshitua aliondoka na kwenda nyumbani
kumchukua Debora ili waende wote huko shuleni. Alipofika nyumbani alimkuta
Debora akiwa anafua nguo, alimpokea kwa furaha ya kulazimisha ili tu kuficha
uhalifu ambao alikuwa ameufanya usiku. Alipoambiwa kuwa wanahitajika shuleni
wote wawili, Debora alipigwa na butwaa, aliishiwa pumzi kabisa. Kichwani
alikuwa na maswali mengi, lakini wazo lake kuu lilikuwa, “yametimia, siri
imefichuka”. Huku akionyesha kuwa na mshaka makubwa na kushindwa kujificha.Basi
wakaondoka kuelekea shuleni kama walivyokuwa wameitwa na Mwalimu mkuu.
Walipofika shuleni wanafunzi wote walikuwa ukumbini, polisi pamoja na walimu
wote na baadhi ya wafanya kazi walikuwa wakifanya uchunguzi wa ile maiti
iliyopatikana porini. Ilikuwa imeshafahamika wazi kwamba ule ulikuwa ni mwili wa Rebeka maana
wanafunzi wote walikuwepo isipokuwa yeye. Hivyo
Debora na Baba Rebeka walipofika tu walipelekwa ofisini kwa mwalimu mkuu
ili wataarifiwe kwa utaratibu juu ya tukio hilo. Debora alizidi kupata mashaka
moyoni endapo atagundulika kuwa ndiye
mhusika mkuu katika tukio hilo la mauaji ya Rebeka. Basi wazazi wa
Rebeka walielezwa juu ya tukio hilo la mauaji ya binti yao. Baba Rebeka
akainamishwa kichwa chini baada ya kusikia yaliyomkuta binti yake mpendwa. Huku
Debora akionyesha kupigwa na butwaa na kubaki anawayawaya. Taratibu zilipokamilika Baba Rebeka alipiga
moyo konde kulipokea tukio hilo lakini ilimuwia vigumu. Hata hivyo ilimpasa
kujitahidi kuvumilia. Polisi waliahidi kufanyia utafiti na kubaini wahusika wa
tukio hilo.
Taratibu za
kuusafirisaha mwili wa marehemu kwenda nyumbani zilifanyika. Baadhi ya
wanafunzi na baadhi ya walimu waliongozana kusindikiza msiba ule. Huko nyumbani
nako maandalizi ya msiba yalikuwa yakiendelea . Masiba ulipokelewa nyumbani kwa
vilio visivyo pimika. Ndugu na jamaa walilia, waligaa gaa chini, kilio chenye
masikitiko kumlilia binti Rebeka, binti mpole mnyenyekevu, aliyekuwa kipenzi
cha watu nyumbani na shuleni kwake. Kila mmoja aliguswa na msiba ule na hasa
kwakuwa alikuwa ameuawa kikatili vile. Baba Rebeka, nae hakuwezakulivumilia
hili, alibubujika machozi kumlilia binti yake kipenzi pato lake la ujanani.
Alijaribu kuvuta kumbukumbu, akamkumbuka mke wake kipenzi aliyefariki kwa homa
kule kijijini, akakumbuka jinsi alivyojipanga ajipatie mke mwingine lakini
akampata Debora aliyekuwa tasa asimzalie hata mtoto mmoja. Alipuuza maneno na
kejeli za watu akiweka matumaini yote kwa Rebeka binti yake ambaye sasa alikuwa
amekutwa na balaa hilo. Alilia sana asikubali kufarijiwa na yeyote.
Debora nae alijiangusha
chini na kugaa gaa, akalilalia jeneza lililokuwa na mwili wa Rebeka, akalia kwa
nguvu kwa mfululizo huku machozi yakimtoka kama mtoto mdogo. Alilia kwa kwikwi,
akijipiga piga kama vile ana kifafa. Hakika, nyumba nzuri si mlango fungua uone
ndani. Debora alilia vile si kwasababu Rebeka alikuwa amefariki bali kwasababu
siri ilikuwa imefichuka. Alilia akijiuliza, itakuwaje endapo atagundulika kuwa
ndiye mhusika mkuu wa mauaji yake ya kinyama. Isitoshe jamii nzima ilijua kuwa
Rebeka alipendwa sana na Debora.
Msiba
ulipokelewa kijijinI
Basi siku iliyofuata
msiba ulisafirishwa kwenda kijijini kwao ambako mazishi yalifanyika.Huko
kijijini taarifa ya mauaji ya binti huyu ilimsikitisha kila aliyeisikia.Watu
wengi walikilaani kitendo hicho, waliombea wahusika wakamatwe mapema wawekwe
wazi hata kutangazwa kwenye vyombo vya habari.
Rebeka alisindikizwa
katika safari yake ya milele, alizikwa pembeni mwa kaburi la mama yake ambaye
alikuwa alishafariki miaka mingi tu iliyopita.Ilitimia kauli yake aliyoitamka
siku ile pale bwenini kuwa “MAMA
ANANIITA” Mazishi yalifanyika, maombolezo ya msiba ule yahudhuriwa na watu
wengi kuliko msiba wowote uliowahi kutokea pale kijijini. Walifika walimu wake
na baadhi ya wanafunzi wake. Ndugu na jamaa waliokuwa wanaishi mbali na karibu
wote walifika msibani. Rafiki zake aliokuwa akicheza nao michezo ya kitoto kama
sandakalawe, mdunguano, madange n.k. Wote wakiwa na nyuso za huzuni na
kutiririka machozi. Watu walitoa rambirambi kwa wingi kwani waliguswa sana na
tukio hilo la kinyama. Msiba ulipoisha, waombolezaji wakatawanyikana kurudi
makwao lakini wengi wakisema, “alaaniwe aliyemwua binti wa watu asiye na hatia”.
Ndugu nao walitawanyika kurudi kwao, huku moyoni wakiwa na hamu ya kujua tu ni
nani aliyemwua binti yao mpendwa.
Baada ya mambo kuisha
huko kijijini Baba Rebeka na Debora alirudi Makambako walikokuwa wanaishi. Hamu
ya Baba Rebeka ilikuwa ni kutaarifiwa tu ni watu gani walimwua binti yake. Japo
alifikiria kuwa lazima mhusika alikuwa na njama zake tu au alikuwa na fitina na
wazazi wake maana haikuwa rahisi kwa mtoto kama yule kuwa labda aligombana na
mtu kufikia hatua ya kumwua kikatili vile. Debora alijaribu kuficha hofu
iliyokuwa imemtanda moyoni mwake na kumfanya daima akose raha. Alikuwa
akijaribu kutoa maneno ya kumfariji Baba Rebeka ausahau msiba ule na kwamba ni
mapito tu hapa duniani na kila mtu anapitia. Lakini maneno ya Debora
yalionekana kutokuwa na mashiko mbele ya Baba Rebeka ambaye muda wote alikuwa
ni mtu mwenye mawazo akijisikia kama vile ni mkosi umempata. Pia kwakuwa Debora
hakuwa na uwezo wa kushika mimba na aliweka matumaini yake juu ya binti yake, sasa aliona kuwa hata Debora ni nuksi
tu pale nyumbani. Furaha, raha na mizaha ndani ya familia ile sasa viligeuka
kuwa karaha na kero tupu.
Siku zikazidi
kusukumana, miezi nayo ikasogea kwa kasi Baba Rebeka alijaribu kufuta
kumbukumbu juu ya binti yake lakini haikuwezekana hata kidogo, daima
alimkumbuka binti yake. Alikuwa akichukua picha za marehemu binti yake na
kuziangalia mara kwa mara. Kila alipoangalia alitiririka machozi kwa uchungu.
Na muda mwingine alikuwa anachukua picha ya marehemu Mama Rebeka na Rebeka
binti yake, aliziangalia na kukumbuka namna alivyoishi naye alijikuta hana
thamani yoyote, ni mtu mwenye nuksi tupu hapa duniani. Alimtazama Debora na kuona
naye kama alikuwa anamletea kero zaidi pale nyumbani. Alitamani hata amtafutie
kosa ikiwezekana amtimue arudi kwao,
yeye abaki kivyake ajipange upya maana maisha yalikuwa yameshampiga teke.
Debora
hatiani kwa unyama
Msiri wa siri ya moyo
ni mwanasiri mwenyewe. Siri ni siri kwa upande mmoja tu wa mwanasiri ikishaenea
kwa mwingine hiyo sio siri tena. Kauli hizi zilijidhihirisha siku ya jumamosi
asubuhi, mwezi mmoja na nusu baada ya mazishi ya marehemu Rebeka aliyeuawa
kikatili na kukatwakatwa vipandevipande. Siku hiyo wale vijana watatu waliohusika
katika mauaji hayo walikamatwa na polisi. Waliulizwa kiundani juu ya tukio
hilo, nao bila kuuma maneno walijieleza kila kitu. Walipomtaja Debora kuwa
alikuwa mhusika mkuu wa tukio hilo la unyama, hata polisi walipigwa na butwaa
na kwenda kumkamata mara. Walipofika nyumbani Debora alikuwa peke yake, bila
maelezo wakamwambia “uko chini ya ulinzi!” Debora akapigwa na butwaa akasema
moyoni mwake, “yametimia!”. Wakamsweka kwenye gari lao na kuondoka naye bila
kuhitaji maelezo yake yoyote ya kujitetea. Walipofika kituoni walimpigia simu
Baba Rebeka ambaye alikuwa kwenye biashara zake na kumweleza yote yaliyotokea.
Alipigwa nabutwaa aliposikia kuwa Debora alikuwa mhusika mkuu wa tukio lile la mauaji
ya binti yake. Alifura hasira ghafla kwa hofu akamwuliza afande,
“…yaani…unataka kunambia huyo mbweha ndiye aliyemchinja binti yangu…?” Afande
akamwambia, “Fika kituoni hapa basi mapema.” Baba Rebeka bila kuchelewa
aliwasha gari lake na kwenda kituo cha polisi haraka. Njiani alikuwa na msongo
wa mawazo alinusurika hata kusababisha ajali. Aliwaza mengi lakini furaha yake
ni kwamba alikuwa amempata mbaya wake, aliyemwua binti yake. Aliwaza atamfanyia
nini Debora, alitamani kama aende na panga akammalizie hukohuko lakini nafsi
ilisita, alitamani achukue sumu akamnyweshe, alitamani abebe kisu au shoka
akamchakaze Debora, lakini nafsi yake ilisita kufanya yote hayo.
Alipofika
kituo cha polisi alikuwa amejaa hasira juu ya Debora. Afande alimsihi Baba
Rebeka apunguze ghadhabu . Kisha wakamwelekeza kila hatua waliyofanya hadi
kuwapata wahusika hao wa mauaji. Hivyo watuhumiwa baada ya adhabu kali za
viboko visivyo na hesabu na kuburuzwa walihukumiwa kifungo cha maisha
kilichoambatana na adhabu kali za kila mara. Hapo Baba Rebeka hakutamani kuiona
sura ya Debora tena, akasema, “ningejua kuwa yeye ndo mhusika aliyemwua binti
yangu, ningerahisisha ningemmaliza kulekule nyumbani.” Akamalizia kwa kusema, “acheni
afie hukohuko huyo mbweha, sitamani hata kuiona sura yake tena”. Basi baba
Rebeka aliondoka na kwenda zake nyumbani. Kule
nyumbani habari zilikuwa zimeshaenea kuwa Debora amefanya unyama ule.
Kila mmoja alimlaani Debora na kutotamani kumuona tena. Usiku ule Baba Rebeka
hakuweza kulala pale nyumbani kwake kwani alikuwa peke yake. Aliamua kuwasha
gari lake na kuondoka jioni ileile na kwenda kijijini kwa wazazi wake.
Alipofika kijijini wazazi wake walimpokea kwa masikitiko. Walipoanza
kusimuliana habari za kukamatwa kwa Debora ambazo hazikuwa habari mpya pale kijijini.
Watu walifedheheka sana kwa kitendo cha Debora kumwua Rebeka, kwani walikuwa
wanajua kuwa walipendana sana. Wazazi wake na watu wengine wengi walijitokeza
kumfariji baba Rebeka, walimsihi asahau yaliyopita na kuganga yajayo.
Alijitahidi kufanya hivyo lakini kila mara alipotazama picha ambazo walipiga
kama familia alitiririka machozi. Baada ya siku tatu alirudi mjini kuendelea na
kazi zake za kibiashara, Debora naye akiendelea kusota kifungoni kwa kosa la
mauaji ya mtoto asiye na hatia. Hakika
kikulacho ki nguoni mwako, rafiki yako ndiye adui yako.Usimwamini yeyote, amini
kivuli chako. Debora aliaminika sana, lakini hakuna aliyejua kile alichokuwa
anakiwaza juu ya Rebeka.
Rebeka binti aliyepata mauti bila hatia,
astarehe kwa amani katika makao ya milele
mbinguni. Amina!.
Mama Rebeka, astarehe kwa amani,
mwenyezi Mungu amsamehe mapungufu yake amstahilishe katika makao ya milele
Mbinguni. Amina.
~~~~~~~~~~~~~~~~~TAMATI~~~~~~~~~~~~~~~~
SASA UNAWEZA KUJIPATIA NAKALA YAKO YA SIMULIZI HII KWA TSH.3000/-TU. WASILIANA NA MTUNZI.
SIMULIZI NYINGINE ZILIZOTUNGWA
NAMI
ELIAS K. MWALONGO (KANTON)
NI KAMA VILE.
POKEA BARUA YANGU BELINDA-(AUDIO-1000)
KUMBE JIRANI YANGU MCHAWI-5000/-
DADANGU MCHUMBA`NGU
MACHO YANGU YANANIDANGANYA-3500/-
USIMWAMINI YEYOTE
NITAKUFA NA MTU – 1500/-
BAADHI YA VITABU VYANGU
VINAPATIKANA:
1.
PERAMIHO
BOOKSHOP
2.
SONGEA
BOOKSHOP
3.
NDANDA
BOOKSHOP
4.
NJOMBE
BOOKSHOP
5.
TMP
BOOKSHOP-TABORA
6.
ST.ALOIS
BOOKSHOP-MBINGA
7.
ST.KILLIAN
BOOKSHOP-MBINGA
8.
KANTON
PRINTING - IRINGA
~~~***~~~
AU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NAMI
MTUNZI NA MWANDISHI WA VITABU HIVI
KWA No. 0769313224
~~~AHSANTE!~~~
Na. Elias Kalistus Mwalongo
(KANTON)