Tuesday, 4 April 2017

DAMU YANGU IMEMWAGWA NA MAMA`NGU-Mtunzi: Elias K. Mwalongo(Kanton)





DAMU YANGU



IMEMWAGWA NA MAMA`NGU



~~~~~~~~~~~~~~~~+++++++++~~~~~~~~~~~~~~~~~




Mtunzi:



Elias K. Mwalongo (Kanton)

S. L. P 977 Njombe

Simu No: 0769313224


Facebook: Elias Mwalongo

Twitter: Elias Mwalongo

Instagram: Elias Mwalongo

______________________

Chapa Ya Pili, Oktoba 2016



Haki zote zimehifadhiwa. Huruhusiwi kuiga, kupiga chapa, kutafsiri au kukitoa kitabu hiki kwa jinsi yoyote ile pasipo idhini ya mwandishi wa kitabu hiki au mhariri wake. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika.







~~~~~~~~~~~~~++++++++++~~~~~~~~~~~~~









Kitabu hiki nimekiandika kwa heshima ya wale ndugu zangu ambao ninauhakika hawatakisoma. Wale ambao miili yao ilisharudishwa mavumbini ilikotoka na roho zao zimemrudia Mwenyezi aliyeziumba:





Marehemu: Elias Mwalongo (Babu)

Cassiana Mwabena (Bibi)

Kalistus Mwalongo (Baba)

Justine Mwalongo (Baba Mdogo)

Osmunda Mwalongo (Shangazi)

Expeditha Mgaya (Binamu)











~~~~~~~~~~~~~++++++++++~~~~~~~~~~~~~



Na Mtunzi:

Elias K. Mwalongo (Kanton)





                



                   Utangulizi



Katika kupambana na maisha ya hapa duniani, yametusibu mengi  na mengine yanaendelea kutusibu kila uchwao. Mengine yanatutia machozi na kutufanya tuone hatustahili kuendelea kuishi na mengine yanatufanya tutabasamu na kuona maisha yana maana kubwa kwetu. Kila mmoja wetu anapatwa na yote, ya kumfurahisha na ya kumtia simanzi. Ndugu jamaa na marafiki zetu tunaoishi nao wanaweza kuwa sababu ya furaha yetu au huzuni. Inaumiza sana moyoni endapo ndugu yako wa karibu anayeonyesha kukupenda na kukujali, nawe ukamtumaini, halafu siku ya siku yeye ndiye anayefanya njama za kukutoa roho.

Ndani ya kijitabu hiki, DAMU YANGU IMEMWAGWA NA MAMA`NGU, nimeandika simulizi ya kusisimua, ambapo Rebeka, binti mdogo wa darasa la tano, anauawa kikatili na kukatwakatwa vipandevipande na mama yake wa kambo ambaye alikuwa anaishi naye kwa furaha akionyesha kumpenda kwa dhati.

Hakika ukisoma simulizi hii utaiafiki kauli yangu niliyoitaja katika kitabu changu kilichopita kinachoitwa MACHO YANGU YANANIDANGANYA, kuwa nyumba nzuri si mlango fungua uone ndani, na usimwamini yeyote, amini kivuli chako.

Hakika Kikulacho ki nguoni mwako na rafiki yako unayemchekea ndiye adui yako! Wacha nisikucheleweshe, jisomee mwenyewe uone mambo…!

Simanzi iliyotufika mtaani kwetu



Ilikuwa siku ya Jumatatu asubuhi na mapema nikiwa chumbani kwangu, ghafla nilisikia kelele za yowe kutokea kwenye nyumba ya jirani. Nilishitushwa na kelele hizo, nikasogea kwenye dirisha la chumba changu ili nisikilize vizuri. Nilisikia, “uwiii, uwiii,uuuuwi mama yetu jamani tutabaki na nani…jamani Mama Rebeka, umemwacha mwanao atatunzwa na nani…uuuuwi….” Nilijawa hofu nikaogopa hata kutoka mlangoni. Nilibaki mle chumbani nikifikiria kwa hofu. Lakini nilikuwa nimekwisha kujua ni Mama Rebeka aliyefariki. Lakini nilikuwa kama siamini kuwa ni yeye kwani kuna kipindi alikuwa anaumwa lakini alishapona kabisa na aliruhusiwa kurudi nyumbani. Pia mume wake alisafiri kikazi akijua hali ya mke wake ni njema kabisa na anaendelea vizuri.

Huku nikiendelea kusongwa na mawazo yaliyosukwa na hofu kubwa nilisikia kelele za yowe zinazoashiria kuwepo na msiba ziliongezeka ghafla, kumbe hata majirani sasa walikuwa wanaanza kumiminika pale nyumbani pale kwa Marehemu Mama Rebeka. Nami nikapiga moyo konde, nikafungua mlango wa chumba changu nikatoka taratibu nikipepesa macho huku nikiwa nimejawa na mshangao kwa yale yaliyokuwa yanaendelea asubuhi ile pale mtaani kwetu. Nikaungana na watu wengine waliokuwa wanaelekea kule nyumbani kwa Mzee Mlowe ambaye pia alifahamika kama Baba Rebeka. Tulipofika tulikuta tayari watu wengi wamejaa pale uwanjani, wote wakiwa na nyuso za huzuni. Pembeni hivi karibu na bustani watu wengine wanaume walikuwa wametingwa wanachakarika kusogeza miti ya kujengea jukwaa. Pale uwanjani ulikokwa moto na wengi walikuwa wameuzunguka moto maana kulikuwa na baridi sana asubuhi ile.









Mimi nikiwa pale uwanjani jirani na moto nilikuwa nasikiliza kwa makini minong`ono ya watu waliojaa pale nje huku mimi nikiwa kimya sichangii hoja yoyote maana sina uhakika kama ni Mama Rebeka aliyefariki na nini kimemsibu. Mama mmoja ambaye ni jirani yetu na ambaye mtoto wake Gloria nilikuwa nasoma nae darasa moja, kwa sauti ya chini ya wasiwasi na majonzi alisema, “…mama huyu ameteseka sana kwa homa yake. Walimwambia ana Maleria, mara vidonda vya tumbo, mara kisukari, mara kifua kikuu,japo alitibiwa akapona na aliruhusiwa kufaanya hata kazi ndogo ndogo za nyumbani. Hata hivyo jana jioni nilipitia kumsalimu aliniambia hali yake inabadirika, anahisi kuishiwa nguvu, na maumivu kwa mbali mwili mzima. Nilimsihi apumzike kwanza halafu kama hali itazidi kuwa mbaya asubuhi nitamsindikiza hospitalini akapimwe. Ilipofika saa kumi na moja alfajiri nikajaribu kumpigia simu nikakuta haipokelewi. Nikajua huenda amezidiwa, nikakurupuka mbio hadi hapa nikabisha hodi mara kadhaa bila kujibiwa nikaamua kuingia tu, masalale! nikamkuta amejilaza kitandani kimya kama vile amelala fofofo nikajaribu kuita mara kadhaa tena kwa sauti baadaye hata kwa kumtikisa lakini ilikuwa ni kazi bure. Hakufungua hata jicho kunitaza kwa mara ya mwisho, hakutamka hata neno la kuniaga, wala hakutikisa kiungo chake cha mwili hata kimoja hata kunipungia mkono wa `kwaheri`. Nilipoendelea kuita kwa sauti kubwa ambayo sasa ilikuwa inageuka kuwa kilio hakuamka wala kutikisika badala yake aliamka Binti yake wa pekee Rebeka, ambaye alikuwa amelala fofofo kwenye kitanda kilichokuwa pembeni kidogo mle chumbani. Kelele zangu ziliishia kumuamsha Rebeka na kushindwa kumuamsha Mamake licha ya kumtikisa kwa nguvu, kumbe Roho yake ilikuwa imesharudi kwa aliyeiumba na mwili wake ulikuwa ukingoja saa ya kurudishwa udongoni ulikotoka. Ili kujiridhisha nikajaribu kusikiliza mapigo ya moyo wake, nikaishia kusikia mapigo ya moyo wangu yaliyokuwa yanakwenda kasi kutokana na woga. Ghafla moyo wangu ulikufa ganzi, nikalia kumpoteza rafiki yangu mpendwa, nikalalama moyoni nikatamani hata kujipiga masumbwi na mimi nife, kwa woga nikapiga yowe mara kadhaa ndipo majirani wakaanza kutiririka na sasa hapa pamejaa…” Mama Gloria alimaliza kwa kusema, “Kabinti kake jamani, sijui katalelewaje” Mara nikaona Mama Gloria akisumbuka kufutafuta mchozi yaliyokuwa yakitiririka mashavuni mwake. Tuliposikia yaliyokuwa yamejiri, sote tulipigwa na butwaa kwani siku zilizopita tulikuwa tukimwona Mama Rebeka akiwa mzima kabisa. Homa zake zilizomsumbua kwa kipindi cha nyuma zilikuwa zimeshapona.

Wakati ule tukiwa tumejaa pale nje, ndugu wa marehemu walikuwa ndani ya chumba fulani wakilia kwa uchungu wa kumpoteza ndugu yao. Watu wengine walikuwa wametingwa na pilika pilika za kutuandalia chai sisi tuliofika msibani pale asubuhi ile. Watu wengine niliwaona wakiwa wanachota maji toka kisimani kuleta pale msibani.

Ilipofika saa nne asubuhi Baba Rebeka alifika pale nyumbani ambapo sasa palikuwa pamefurika ndugu na majirani wakibubujika machozi. Alikuwa amearifiwa jioni kuwa hali ya mke wake imebadilika, si nzuri tena hivyo aliahirisha safari yake akaanza kurudi. Ilipofika alfajiri alitumiwa ujumbe na majirani kwa njia ya simu kuwa alikuwa amempoteza mke wake, hivyo alipofika hakushangaa umati ule wa watu kwani alikuwa anajua kinachoendelea. Alishuka kwenye gari akiwa amevaa miwani myeusi na kofia. Mkononi alishika leso nyeupe, bila shaka ilikuwa ya kufutia machozi. Alipokelewa na baadhi ya ndugu zake wakampeleka moja kwa moja ndani ya chumba ambacho  walikuwa wamehifadhi mwili wa marehemu Mama Rebeka.

Baadaye mimi nikaungana na wale waliokuwa wanajengajukwaa. Tukaendelea kujenga jukwaa mpaka saa sita hivi mchana ambapo sasa watu wengine walitakiwa kukaa kwenye jukwaa hilo kwani watu walikuwa wamejaa mno. Wakati tukitengeneza jukwaa watu wengine walikuwa wakichonga jeneza na wengine walikuwa wanachimba kaburi. Pia wanawake wengine majirani walikuwa  wakiandaa chakula cha mchana kwaajili ya watu wote waliofika pale msibani.

Ikafika saa nane na nusu hivi baada ya chakula cha mchana, jeneza lenye mwili  wa marehemu likawekwa pale uwanjani, kisha baba mmoja akatangaza kuwa ulikuwa ni muda wa kuaga mwili wa marehemu ikiwa ni maandalizi ya mazishi.

Basi alitangulia mume wa marehemu akiwa amemshikilia mkono mtoto wake aliyekuwa akiangua kilio hali hajui nini kinaendelea kwani alikuwa bado mdogo. Wakafuata wazazi wa marehemu yaani babu na bibi wa Rebeka, wakafuata kaka, dada na wadogo zake marehemu. Baada ya ndugu wote wa marehemu kuisha tukafuata sisi majirani.

Baada ya sisi sote kutoa salamu zetu za mwisho jeneza likafungwa kisha wanaume fulani wakalibeba tayari kwa kuelekea makaburini. Tukaanza kwenda makaburini huku tukipokezana jeneza lile mara kwa mara. Karibu watu wote tukaongozana msururu mrefu kuelekea makaburini kwenye mazishi.Wanawake wengine walianzisha nyimbo mbalimbali za mazishi.Tulipofika tukaliweka jeneza nje ya kaburi pembemeni kidogo. Watu waliokuwa wanafuata nyuma yetu wakafika wote wakazunguka pale kaburini huku wengine wakisimama juu ya makaburi mengine yaliyokuwa jirani

Mazishi yaliendelea huku watu wengine hasa ndugu wamarehemu na baadhi ya majrani wakiwa wanalia kwa sauti. Wanawake wengine walikuwa wa kushikiliwa kwani walikuwa wakilia kwa sauti, wakijipigapiga, wakijiangusha chini na kugaagaa, wakijiviringisha na kujitupa chini, puu! Baada ya kuzika wanawake fulani walianza kulia kwa nguvu, wakijidondosha juu ya kaburi la mama Rebeka. Nilimgundua dada mmoja wa makamu ambaye alikuwa ni mdogo wake wa marehemu ambaye alikuwa ametoka kuhitimu elimu yake ya chuo kikuu anasubiri ajira. Nilifanikiwa kumuona Baba Rebeka akiwa amemshikilia binti yake, Rebeka kwa mikono miwili huku akiwa amejiinamia kama mtu mwenye msongo wa mawazo na majonzi. Nilipozidi kumuangalia vizuri nilimwona anajifuta machozi kwa leso nyeupe aliyokuwa ameishika kwa mkono wake wa kushoto. Mimi niliendelea kuyashuhudia haya nikiwa nimesimama juu ya kaburi fulani lililokuwa upande wa juu.

Ukafika wakati wa kuweka mataji juu ya kaburi. Taji la kwana liliwekwa na mwongozaji wa ibada ile ya mazishi. Akafuata mume wa marehemu akiongozana na binti yake pekee. Wakafuata wazazi wa marehemu, kisha wakafuata kaka dada na wadogozake marehemu. Kisha wakamalizia ndugu wengine wa marehemu kama mjomba, binamu, shangazi, na wengineo. Baadaye mtu mmoja ambaye bila shaka alikuwa ni ndugu wa marehemu alisoma historia fupi ya marehemu. Nakumbuka alisema kuwa, marehemu alizaliwa mwaka 1986, amefariki akiwa na miaka 28. Alikuwa ni mkulima wa kawaida. Aliacha mume na mtoto mmoja. Mungu aipimzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.

Kisha ukatangazwa utaratibu wa kuondoka kuelekea nyumbani kwa wafiwa kunawa mikoni(kula chakula) basi tukaanza kurudi taratibu huku wengine wakiendelea kulia na wengine wakiwa wamenyong`onyea wanaomboleza kwa huzuni.Wanawake wengine wakiwa wamejifunika kanga vichwani huku wakilia kimyakimya. Tulipofika pale nyumbani tulipokelewa kwa maji ya kunawa, kisha tukagawiwa sahani za vyakula na kuonyeshwa sehemu za kukaa. Wakati huu kulikuwa na ukimya pale nyumbani maana sote tulikuwa na uchungu wa kuondokewa na mwenzetu ghafla vile.





Twiwalala

Jioni ile watu walikuwa bado wamefurika pale nyumbani baada ya kula chakula cha jioniambacho tulikipata mida ya sa moja hivi jioni. Watu tulikusanyika makundimakundi tukiota moto. Baadaye tulianza kuimba nyimbo mbalimbali kama ilivyo kawaida ya misiba mingine. Nyimbo zilipozidikutunogea baadae tulianza hata kucheza. Kila wimbo ulipoisha ulianzishwa mwingine, na mimi nilikuwa nazifahamu kwani nilikuwa nimeshawahi kuzisikia mara nyingi tu. Baadae ukaanzishwa wimbo ambao nilikuwa naupendelea zaidi, unaitwa “Twiwalala”, maana yake “tunapapasa au tunatafuta”. Ulipoimbwa wimbo huu ni kama vile nilisahau kuwa nipo msibani maana nilifurahi sana, tulicheza sana huku tukiwa kama vile tunatafuta kitu kilicho potea. Nakumbuka tuliimba hivi: Twiwalala u mama vesu(twiwalala) u mama vesu asivoneha(twiwalala) umama vesu ahele whiya(twiwalala) Maana yake, Tunamtafuta mama yetu (tunatafuta)  mama yetu haonekani (tunatafuta)  mama yetu ameenda wapi(tunatafuta)…” Kama ilivyo kawaida ya wimbo huu ukiimbwa,tulianza kwenda tunatafuta hadi makaburini usiku ule huku tukiimba kwa sauti na vile tukienda tunakimbia viatu vilikuwa vikisikika tukipiga na makofi kwa kufuata mapigo ya viatu, na sisi ndo tuliendelea kuimba kwa hisia. Tulikimbia huku tunapapasa kuzunguka kaburi mara kadhaa huku yowe zikisikika kati yetu, uuuuwii, uuuuuwii! Kwa mwendo uleule tulioendea tukaanza kurudi nyumbani. Haya yote tuliyafanya saa tano kama sio saa sita hivi usiku.

Tuliporudi wengine waliendelea kuimba nyimbo nyingine, ila mimi na wengine tukaanza kusinzia tukatafuta sehemu ya kujilaza hadi jogoo walipoanza kuwika. Asubuhi ile tulikunywa chai tuliyokuwa tumeandaliwa na baada ya hapo watu wengine walianza kutawanyika kurudi kwao. Mimi nilikawia kidogo kuondoka.

Baada ya Msiba kuisha

Siku tatu baada ya msiba wa mama Rebeka, ndugu wote walikusanyika, ili kufanya tathimini ya tukio hilo lililowakumba na kuwatia simanzi ndugu wote hata majirani pia. Wazo kuu katika kikao hicho ni juu ya pengo lililoachwa na marehemu na hasa katika jukumu la kumlea Rebeka binti pekee wa marehemu, pato la ujanani. Walisema kuwa baba Rebeka hataweza kumtunza binti yake kwakuwa alikuwa bado ana umri mdogo. Hivyo walikubaliana kuwa Rebeka akae na bibi yake. Tangu siku hiyo Rebeka aliaza kuishi na bibi yake. Kutokana na akili yake ya kitoto Rebeka alisahau kabisa tukio la kifo cha mama yake hata akamzoea bibi yake kwani kila wakati walikuwa pamoja. Rebeka aliendelea kuwa mchangamfu mwenye busara na mwepesi kuchangamana na wenzake katika michezo yao ya kitoto.

Baba Rebeka alionekana ni mwenye kukosa furaha kila siku kutokana na kifo cha mke wake kipenzi, aliyempenda kwa dhati, akafunga naye ndoa ya kikatoliki watu wakasherehekea. Walianza kuishi kwa furaha, na kupanga maisha yajayo. Maisha yao yalianza kung`ara, na upendo ulitawala. Na Kwa neema ya Mwenyezi Mungu walijaliwa kupata mtoto wao wa kwanza, pato bichi la ujanani. Rebeka binti mnyenyekevu, mwenye sura ya upole, mwenye tabasamu la kujipatia marafiki tele. Kumbe Mungu ndiye mpaji na mnyimaji, akawanyima nafasi ya kuendelea kufurahia ndoa hiyo iliyokuwa ikinawili siku hadi siku. Astarehe kwa amani mbinguni Mama Rebeka!.

Miezi minne baadaye

Miezi minne ilipita, ikawa bado haifahamiki kama baba Rebeka ataoa mke mwingine au laa. Rafiki zake wengi walikuwa wakimshauri kuwa aoe tena mke mwingine kwani umri wake ulikuwa bado unaruhusu, alikuwa ni kijana mchapa kazi mwenye mvuto na heshima zake. Licha ya ushauri na maoni ya watu mbalimbali Baba Rebeka hakuonyesha dalili zozote za kukubaliana na ushauri wao au kukataa. Japo watu walikuwa wanasemasema kuwa lazima ataoa mwingine tu. Kumbe lisemwalo lipo, kama halipo basi liko njiani linakuja na bila shaka litafika.

Baada ya miezi sita tangu kifo cha mama Rebeka, baba Rebeka akajipatia mke mwingine na bila kukawia akaenda kumtambulisha kwa wazazi wake kwamba ndiye atakayebadili nafasi ya Mama Rebeka. Wakati wako Sebuleni yeye Baba Rebeka, Babu na bibi Rebeka, aliingia Rebeka akiwa hajui hili wala lile alishtuka kuona sura ya baba yake baada ya kupoteana kwa muda mrefu kwani baba yake alikuwa ni mfanyabiashara huko mjini, na ni mara chache tu aliweza kufika kusalimu wazazi pale kijijini.

Kwa furaha na bashasha Rebeka alimrukia baba yake akamsalimu na kung`ang`ania ampakate. Hapo Baba Rebeka alimkumbuka sana mke wake kipenzi. Alionekana kuwa mnyongeghafla, lakini akapiga moyo konde, akajikaza kisabuni, akaanza sasa kutabulisha. Akasema, “Wazazi wangu wapenzi, baba na mama, baada ya kuondokewa na mke wangu, mama Rebeka, sasa Mungu amenijalia, nimempata huyu ambaye natumaini ndiye atakayenifuta machozi na kunisahaulisha msiba uliopita. Anaitwa Debora, binti pekee wa Mzee Linus na mama Theodora wa mjini Makambako. Ninamatumaini makubwa naye. Amesoma japo si sana. Natumaini atanilelea vizuri binti yangu Rebeka, na kunipatia wadogo zake Rebeka. Naomba wazazi wangu, mmpokee kwa furaha aingie katika ukoo wetu” Wazazi wake walitazamana kisha, baba yake akaanza kusema kwa busara, “Mwanetu umechukua uamuzi ulio bora, hongera sana kwa kumpata Debora ambaye mtatunzana mkiaminiana na kuheshimiana.Umefanya vema maana peke yako usingeweza kumlea binti yako huyu, ukizingatia ni mtoto wa kike. Sisi wazazi wako maadamu sisi ndio tuliotangulia kuliona jua, tutashirikiana pamoja nawe, usiwe na shaka”. Akamgeukia Debora, mke mpya wa baba Rebeka akamwambia, “Karibu sana Debora katika ukoo wetu. Sisi ni wazazi wako pia, tutakuwa nanyi bega kwa bega mtuzane na kuthaminiana katika maisha yenu. Umlee vema Rebeka ili baadaye aje atusaidie sote.” Debora huku akitabasamu, alitikisa kichwa juu-chini, kuonyesha kukubaliana na maneno yale yaliyoongelewa.Mazungumzo yaliendelea kwa kitambo kidogo kisha, baba Rebeka akaondoka na mke wake wakamwacha Rebeka na kwamba watakuja tena kumchukua baada ya wiki moja.

Debora awa gumzo!

Wiki moja ilipotimia walienda kumchukua Rebeka kwa bibi yake na kuanza kuishi naye. Maisha ya Rebeka na ma`mdogo wake yalikuwa murua hata ndugu na majirani  walitambua hilo. Debora alimpenda Rebeka kama binti yake wa kumzaa. Rebeka naye aliishi na ma`mdogo wake kwa furaha kwani alimzoea na kumchukulia kama mama yake kabisa. Hali hii ilimpelekea Rebeka kusahau kuhusu marehemu mama yake mzazi.

Miaka miwili baadaye hali yao ya kimaisha ikiendelea kuwa shwari kidogo, baba Rebeka alinunu gari la kutembelea pia alifungua duka mjini Makambako. Rebeka nae alikuwa ameshaingia shule ya msingi yuko darasa la pili. Ma`mdogo alikuwa akimnunulia Rebeka nguo, viatu, pipi, soda, sambusa, ubuyu na zawadi nyingi kedekede. Licha ya mazuri yote waliyokuwa wakifurahia, familia hii ilikuwa imepata pigo jingine ambapo iligundulika kuwa Debora, alikuwa tasa, hivyo hakuweza kushika mimba. Kwa kujitambua hivyo Debora alijitahidi kuonyesha upendo wake kwa Rebeka. Daima alipenda kuongozana naye katika matembezi yao hata katika mapumziko. Alitamani na yeye siku moja apakatemtoto wa kumzaa yeye mwenyewe lakini haikuwezekana kwa kuwa alikuwa tasa.

Hata hivyo hali hii ilimpelekea Debora ajiona ni mwenye mapungufu makubwa na asiyestahili kati ya jamii yake. Alipokuwa akikutana na wenzake waliokuwa wakikutana na wenzake waliomsalimu kwa furaha na mizaha naye alijitahidi kutabasamu kwa uso wa furaha huku akijitahidi kuficha simanzi iliyokuwa inautafuna moyo wake. Alipokuwa akitembea huku na kule alihisi macho ya wapita njia wote yanamwangalia yeye kwa dharau, kumbe wala wengine walikuwa hawajui tatizo lake la utasa. Aliumia sana moyoni maana alihisi kila mtu anamnyoshea kidole yeye na kumbeza, na kumbinulia midomo, kumbe sivyo. Rafiki zake waliomtembelea nyumbani aliwapokea kwa furaha lakini moyoni alijaa simanzi, alikuwa dhaifu moyoni. Hata  hivyo alijitahidi kwa kila namna kuficha simanzi na uvuguvugu wa moyo wake. Alicheka na marafiki zake, ndugu na majirani japo moyo wake ulisinyaa kwa hofu ya maneno ya ndugu zake. Hata hivyo aliendelea kumlea Rebeka kwa furaha na kwa upendo.

Siku zikazidi kusukumana na miezi ikienda kwa kasi , maneno ya watu yakaanza kumfikia bila chenga. Walikuwa wakiulizani, huyu wifi yetu vipi, mbona hatuoni dalili kama siku moja atanyonyesha kama sisi? Huyu wifi yetu vipi, bado anajipanga tu? Na maneno mengine mengi yalisikika yaliyozidi kumuumiza sana moyoni. Ndugu wengine wakawa wanasema, “Baba Rebeka ametuletea nuksi kwenye ukoo wetu. Hili ni balaa halijawahi kutokea kwenye ukoo wetu. Kabla ya balaa hili halijaenea, amrudishe kwao”. Maneno haya na mengine mengi ya kejeli yaliyoendelea kuvuma mitaani yaliendelea kumsononesha. Ndugu na majirani walionekana kutompenda tena, walimjengea fitina na kumfanyia kila jeuri pengine angeweza kujiondokea mwenyewe. Lakini hakuondoka aliendelea kuishi  pale akimlea Rebeka ambaye sasa alikuwa darasa la tano.

Alianza kugundulika wazi sasa kuwa daima alikuwa na msongo wa mawazo. Rebeka nae aligundua kuwa upendo wama`mdogo wake ulikuwa umepungua kwa kiasi kikubwa. Aliona hamjali tena kama hapo awali.

Baba Rebeka alionekana kutojali sana tatizo la mke wake, aliamua kukubaliana na hali halisi. Maneno ya wanandugu aliyapotezea na kuendelea na shughuli zake maadamu Debora alikuwa anamlelea binti yake wa pekee. Vile vile Baba Rebeka alimtumainia binti yake kuwa ndiye mrithi wa mali zake. Alitoa matumaini kabisa ya kuoa mke mwingine na kujitafutia watoto kwani aliona kama vile amepatwa na mkosi. Katika umiliki wa duka lake na gari aliandika REBEKA, ambalo lilikuwa jina kamili la binti yake.

Debora alijitahidi kuvumilia, aliyahimili maneno na machukizo ya ndugu na majirani na kuendelea kumpenda Rebeka kwa dhati kama vile mtoto wake wa kumzaa, lakini yakamshinda, maskini!



Kikulacho ki nguoni mwako

Baada ya miezi michache Debora alionyesha wazi kuwa aliishusha thamani ya Rebeka. Alionekana kutompenda sana kama hapo awali. Rebeka naye aligundua kuwa upendo kati yake na mam`dogo wake ulikuwa umeshuka,japo hakujua ni kwanini. Rebeka alijaribu kujisogeza na kuwa jirani na mam`dogo wake hata hivyo mdogo wake alionyesha kutomjali kama vile mwanzo.

Baba Rebeka alikuwa akiendelea kuwapenda Debora na Rebeka binti yake wa ujanani. Kasi ya maneno ya watu juu ya utasa wake yaliendelea kumpa simanzi. Pia kitendo cha Baba Rebeka kuandika majina ya Rebeka katika kila mali aliyomiliki ikiwe magari, duka, na vyombo mbali mbali kilimfanya Debora kuumia zaidi kwani hakuwa na mtoto wa kumzaa ambaye jina lake lingeandikwa kumiliki mali za baba yake, wala yeye mwenyewe hakuandikwa katika mali yoyote.

Alimwonea wivu sana Rebeka ambaye alikuwa bado binti mdogo wa miaka 12 akisoma darasa la tano katika shule fulani ya bweni. Rebeka hakujua kuwa anajengewa chuki na mam`dogo wake.

Wahenga husema, kikulacho ki nguoni mwako, rafiki yako ndiye adui yako. Kauli hizi zilijidhihirisha katika familia hii ambayo sasa ilikuwa imejaa wivu, fitina, chuki na sikitiko la moyo. Debora alijaribu kujitahidi kuonyesha furaha na kumchangamkia Rebeka lakini moyo wake ulikuwa umefura hasira , umekunja ngumi, tayari unajiandaa kupambana na familia yake. Hata hivyo hakupenda ifahamike kuwa amejenga chuki moyoni mwake. Hivyo aliendelea kujisogeza karibu na Rebeka kinafiki tu huku akiendelea kumnunulia vitu vidogovidogo kama vile madaftari, kalamu, ubuyu, pipi hata nguo pia alimnunulia.

Maneno ya watu yaliendelea japo sasa walisema, “inaonekana Debora amelipokea tatizo lake la utasa, amerdhika ameamua kumchukua Rebeka kama mtoto wake wa kumfariji. Kumbe maskini wa Mungu, Macho yanadanganya, nyumba nzuri si mlango, fungua uone ndani! Debora alifanya vile akiwa na lake jambo!





Ziara ya Debora shuleni kwa Rebeka



Huku akiendelea kuficha chuki iliyokuwa moyoni mwake na usoni akionesha kuendelea kumpenda Rebeka siku moja aliamua kwenda kumtembelea shuleni kwake akiwa amembebea nguo, madaftari na fedha ambazo alimwachia za matumizi, japo Rebeka mtoto mdogo vile hakuhitaji pesa nyingi za matumizi. Alipofika shuleni pale alipokelewa vizuri akaonana na Rebeka, akaomba nafasi ya kuongea nae kwa muda mfupi kama mzazi. Kisha akaonyeshwa mazingira ya shule hiyo  na chumba cha Rebeka hata kitanda chake. Alikuwa analala bweni B chumba namba 3 kitanda cha juu jirani kidogo na dirisha. Baada ya maongezi hayo ambayo hayakuchukua hata muda wa saa moja, huku akijionyesha ni mwenye furaha, aliagana na walimu na kisha kuondoka kurudi nyumbani huku Rebeka akirudi darasani kuendelea na vipindi. Rebeka alifurahi sana kutembelewa na mama mdogo wake siku ile kwani hakutegemea, pia kwakuwa alimletea fedha za matumizi. Ziara ya Debora shuleni kwa Rebeka ilimfariji sana Rebeka, alijawa na furaha na kuhisi upendo wa Debora kwake ulikuwa unaongezeka. Kumbe usilolijua ni kama usiku wa giza nene na kitanda usichokilalia hujui kunguni wake. Ziara hiyo ilikuwa na lake jambo, si bure!

Ziara ya kwenda kumsalimu Rebeka, kumtembeza kwenye mazingira ya shule kumwonyesha bweni analolala hadi kitanda chake lilichukuliwa kama jambo la kawaida na hakuna aliye hamaki au kupata mashaka yoyote lakini kumbe zilikuwa ni njama za kufanya mauaji. Kumteketeza binti Rebeka binti wa watu jamani! Kwakuwa hakuna aliyeshitukia njama hizo, basi mikakati ya maangamizi iliendelea kufanyika.



 “Mama ananiniita!”



Siku iliyofuata Debora alitafuta vijana wa kiume watatu. Akawaomba wakutane wazungumze juu ya suala hilo. Walipokutana akawapa maelekezo yote. Aliahidi kuwapa kiasi cha shilingi laki nne kila mmoja endapo watafanikisha zoezi hilo. Vijana hao bila kusita wala kuomba muda wa kufikiria juu ya hilo wakasema wako tayari kuifanya kazi hiyo kwa umakini, kwa usahihi bila kukosea kwani wanauzoefu mkubwa wa kazi hiyo.

Maandalizi yalifanyika, fedha walipewa, mbinu zilipangwa na siku tatu baadaye, siku ya Jumatano usiku wa sa tano na nusu hivi walikutana sehemu fulan hao vijana watatu pamoja na Debora. Siku hiyo baba Rebeka hakuwepo nyumbani alikuwa amesafiri, kufuata bidhaa kwaajili ya biashara yake. Wote walikuwa wamevaa nguo nyeusi na kujifunika hadi kichwani ili wasigundulike kirahisi. Debora alikuwa mikono mitupu huku akiwaongoza vijana wake waliokuwa wamebeba zana mbalimbali walizoona zitawafaa katika katika shughuli hiyo waliyokuwa wanaiendea.Mmoja alikuwa amebeba panga lenye makali sana, mwingine alibeba visu viwili kikubwa na kidogo wakati mwenzao alibeba shoka na kirungu fulani si kikubwa sana.

Wakiongozwa na Debora walienda mpaka pale shuleni. Walisogea taratibu mpaka pale alipokuwa anakaa mlinzi wa shule hiyo. Walipofika walikuta amejiegesha pale kibandani mwake akiwa amesinzia. Wakaamua kurudi nyuma kidogo kisha kupitia njia nyingine, wakaenda moja kwa moja bwenini kwa Rebeka wakiongozwa na Debora ambaye alikuwa tayari analifahamu bweni hilo. Wakasogea taratibu pale dirishani ambapo kitanda cha Rebeka kilikuwa jirani.Kulikuwa kimya kuonyesha kuwa wanafunzi wote walikuwa wamelala.Hata mlinzi naye alikuwa amesinzia pale kibandani kwake. Debora akasogea pale dirishani kisha kwa sauti ya chini chini akaita “Rebeka!Rebeka” Rebeka akashituka kwani alikuwa amekwishagundua kuwa ni sauti ya mam`dogo wake anayempenda. Akaitika “Abee!” Debora akasema, “njoo hapa dirishani mwanangu!” Rebeka alipotaka kuamka na kutaka kusogea dirishani, aliitwa na mwenzake aliyekuwa  kitanda cha jirani, akamwuliza “Rebeka unaenda wapi?” Yeye akasema, “mama ananiita!” basi akasogea dirishani na akafungua dirisha ili amsikuilize mama yake mdogo ambaye alimsikia akimwita mara mbili.



 Alipotaka tu kuchungulia nje, wale vijana watatu wakamshika kwa nguvu, wakamvutia nje kupitia pale dirishani na kabla hawajamtua chini, wakambonda na shoka kichwani mara mbili wakiwa bado wamemshikilia juujuu, akakata roho palepale binti Rebeka maskini.

Kisha wakaubeba begani mwili wa marehemu Rebeka kisha wakatokomea kwenye msitu fulani uliokuwa jirani ambao ulikuwa umefunikwa na giza nene. Huku wale waliokuwa wamelala mle ndani wasijue kilichokuwa kikiendelea nje ya bweni lao kwani walilala fofofo.

Huko porini walimkatakata vipande Rebeka binti wa watu asiyekuwa na hatia yoyote. Kisha nao wakatokomea, wakaenda zao, baada ya kufanya mauaji hayo ya kinyama. Debora nae alirudi nyumbani ikiwa ni sa saba usiku. Alipofika nyumbani alienda kulala.

Asubuhi yake kama kawaida yake akaendelea na shughuli zake akijitahidi kuficha uhalifu alioufanya usigundulike kwa kumtazama tu usoni. Alikuwa akitafutiza furaha na tabasamu kwa kuongeaongea na watu na kucheka nao. Yeye aliwambia wale vijana wake watatu kuwa hilo liliofanyika iwe siri yake yeye na wao tu. Maskini Debora, alisahau kuwa: Msiri wa siri ya moyo ni mwanasiri mwenyewe. Msiri huiweka siri sirini mwake na  pango la siri ni moyo. Moyo wenyewe  umeumbwa kisirisiri, hata ukiupasua hauwezi kukwambia siri ya mwanasiri. Siri ni siri kwa upande mmoja tu wa mwanasiri, ikisha sikika kwa wengine hiyo si siri tena. Pia siri ni siri endapo inataka yenyewe kuwa siri vinginevyo ni kucheza madange tu.

Hakuna marefu yasiyo na ncha na mbio za sakafuni huishia ukingoni.



Kindumbwendumbwe shuleni



Kilizuka kindumbwendumbwe baada ya kuona Rebeka hajaonekana pale asubuhi, iwe bwenini kwake, wala sehemu nyingine yoyote. Na zaidi ilipofika mida ya saa mbili ambapo wale wanafunzi walitakiwa kufanya usafi na hasa kufagia viwanja vyao, madarasa na kudeki vyoo. Wachache walienda porini kuvunja matawi ya miti wayatumie kama mifagio. Ghafla zilisikika yowe kutoka huko porini, wanafunzi wote waliokuwa huko walirudi wanakimbia wakiwa wamejaa woga na hofu, wanahema wengine hadi kulia kabisa kwa kile walichokishuhudia. Wengine walikimbia japo hawakujua kulikoni. Basi mwalimu aliyekuwa zamu siku hiyo akashuhudia pilikapilika hizo akawauliza nini kimetokea, binti mmoja aliyefahamika kwa jina la Jane alieleza alichokiona huko porini, akasema, “Mwalimu, nipokuwa navunja mfagio kule porini nikaona damu, nilipotaka nigeuke nimwite rafiki yangu Felista nimwambie nikakuta….” Akashindwa kumalizia akaanza kulia, basi mwalimu huku na yeye akiwa na hofu akasema twende ukaonyeshe. Wakaenda wakakuta ni mwili wa mtu aliyechinjwa kama kuku na kukatwakatwa asigundulike alikuwa nani. Basi mwalimu aliamuru kengele igongwe na wanafunzi wote wakusanyike. Wakati wanafunzi wanakusanyika mwalimu  alienda kuwambia baadhi ya walimu wenzake kuhusu mkasa uliotokea.Walifanya hesabu ya wanafunzi ikaonekana Rebeka hayupo pale shuleni. Hapo walikuwa wameshaita polisi kuja kuchunguza tukio hilo. Pia Mwalimu mkuu alimpigia simu Baba Rebeka na kumtaka afike pale shuleni pamoja na mke wake. Baba Rebeka kwakuwa alikuwa kwenye shughuli zake za kibiashara alipopata taarifa hiyo iliyomshitua aliondoka na kwenda nyumbani kumchukua Debora ili waende wote huko shuleni. Alipofika nyumbani alimkuta Debora akiwa anafua nguo, alimpokea kwa furaha ya kulazimisha ili tu kuficha uhalifu ambao alikuwa ameufanya usiku. Alipoambiwa kuwa wanahitajika shuleni wote wawili, Debora alipigwa na butwaa, aliishiwa pumzi kabisa. Kichwani alikuwa na maswali mengi, lakini wazo lake kuu lilikuwa, “yametimia, siri imefichuka”. Huku akionyesha kuwa na mshaka makubwa na kushindwa kujificha.Basi wakaondoka kuelekea shuleni kama walivyokuwa wameitwa na Mwalimu mkuu. Walipofika shuleni wanafunzi wote walikuwa ukumbini, polisi pamoja na walimu wote na baadhi ya wafanya kazi walikuwa wakifanya uchunguzi wa ile maiti iliyopatikana porini. Ilikuwa imeshafahamika wazi kwamba  ule ulikuwa ni mwili wa Rebeka maana wanafunzi wote walikuwepo isipokuwa yeye. Hivyo  Debora na Baba Rebeka walipofika tu walipelekwa ofisini kwa mwalimu mkuu ili wataarifiwe kwa utaratibu juu ya tukio hilo. Debora alizidi kupata mashaka moyoni endapo atagundulika kuwa ndiye  mhusika mkuu katika tukio hilo la mauaji ya Rebeka. Basi wazazi wa Rebeka walielezwa juu ya tukio hilo la mauaji ya binti yao. Baba Rebeka akainamishwa kichwa chini baada ya kusikia yaliyomkuta binti yake mpendwa. Huku Debora akionyesha kupigwa na butwaa na kubaki anawayawaya.  Taratibu zilipokamilika Baba Rebeka alipiga moyo konde kulipokea tukio hilo lakini ilimuwia vigumu. Hata hivyo ilimpasa kujitahidi kuvumilia. Polisi waliahidi kufanyia utafiti na kubaini wahusika wa tukio hilo.

Taratibu za kuusafirisaha mwili wa marehemu kwenda nyumbani zilifanyika. Baadhi ya wanafunzi na baadhi ya walimu waliongozana kusindikiza msiba ule. Huko nyumbani nako maandalizi ya msiba yalikuwa yakiendelea . Masiba ulipokelewa nyumbani kwa vilio visivyo pimika. Ndugu na jamaa walilia, waligaa gaa chini, kilio chenye masikitiko kumlilia binti Rebeka, binti mpole mnyenyekevu, aliyekuwa kipenzi cha watu nyumbani na shuleni kwake. Kila mmoja aliguswa na msiba ule na hasa kwakuwa alikuwa ameuawa kikatili vile. Baba Rebeka, nae hakuwezakulivumilia hili, alibubujika machozi kumlilia binti yake kipenzi pato lake la ujanani. Alijaribu kuvuta kumbukumbu, akamkumbuka mke wake kipenzi aliyefariki kwa homa kule kijijini, akakumbuka jinsi alivyojipanga ajipatie mke mwingine lakini akampata Debora aliyekuwa tasa asimzalie hata mtoto mmoja. Alipuuza maneno na kejeli za watu akiweka matumaini yote kwa Rebeka binti yake ambaye sasa alikuwa amekutwa na balaa hilo. Alilia sana asikubali kufarijiwa na yeyote.

Debora nae alijiangusha chini na kugaa gaa, akalilalia jeneza lililokuwa na mwili wa Rebeka, akalia kwa nguvu kwa mfululizo huku machozi yakimtoka kama mtoto mdogo. Alilia kwa kwikwi, akijipiga piga kama vile ana kifafa. Hakika, nyumba nzuri si mlango fungua uone ndani. Debora alilia vile si kwasababu Rebeka alikuwa amefariki bali kwasababu siri ilikuwa imefichuka. Alilia akijiuliza, itakuwaje endapo atagundulika kuwa ndiye mhusika mkuu wa mauaji yake ya kinyama. Isitoshe jamii nzima ilijua kuwa Rebeka alipendwa sana na Debora.



Msiba ulipokelewa kijijinI





Basi siku iliyofuata msiba ulisafirishwa kwenda kijijini kwao ambako mazishi yalifanyika.Huko kijijini taarifa ya mauaji ya binti huyu ilimsikitisha kila aliyeisikia.Watu wengi walikilaani kitendo hicho, waliombea wahusika wakamatwe mapema wawekwe wazi hata kutangazwa kwenye vyombo vya habari.

Rebeka alisindikizwa katika safari yake ya milele, alizikwa pembeni mwa kaburi la mama yake ambaye alikuwa alishafariki miaka mingi tu iliyopita.Ilitimia kauli yake aliyoitamka siku ile pale bwenini kuwa “MAMA ANANIITA” Mazishi yalifanyika, maombolezo ya msiba ule yahudhuriwa na watu wengi kuliko msiba wowote uliowahi kutokea pale kijijini. Walifika walimu wake na baadhi ya wanafunzi wake. Ndugu na jamaa waliokuwa wanaishi mbali na karibu wote walifika msibani. Rafiki zake aliokuwa akicheza nao michezo ya kitoto kama sandakalawe, mdunguano, madange n.k. Wote wakiwa na nyuso za huzuni na kutiririka machozi. Watu walitoa rambirambi kwa wingi kwani waliguswa sana na tukio hilo la kinyama. Msiba ulipoisha, waombolezaji wakatawanyikana kurudi makwao lakini wengi wakisema, “alaaniwe aliyemwua binti wa watu asiye na hatia”. Ndugu nao walitawanyika kurudi kwao, huku moyoni wakiwa na hamu ya kujua tu ni nani aliyemwua binti yao mpendwa.

Baada ya mambo kuisha huko kijijini Baba Rebeka na Debora alirudi Makambako walikokuwa wanaishi. Hamu ya Baba Rebeka ilikuwa ni kutaarifiwa tu ni watu gani walimwua binti yake. Japo alifikiria kuwa lazima mhusika alikuwa na njama zake tu au alikuwa na fitina na wazazi wake maana haikuwa rahisi kwa mtoto kama yule kuwa labda aligombana na mtu kufikia hatua ya kumwua kikatili vile. Debora alijaribu kuficha hofu iliyokuwa imemtanda moyoni mwake na kumfanya daima akose raha. Alikuwa akijaribu kutoa maneno ya kumfariji Baba Rebeka ausahau msiba ule na kwamba ni mapito tu hapa duniani na kila mtu anapitia. Lakini maneno ya Debora yalionekana kutokuwa na mashiko mbele ya Baba Rebeka ambaye muda wote alikuwa ni mtu mwenye mawazo akijisikia kama vile ni mkosi umempata. Pia kwakuwa Debora hakuwa na uwezo wa kushika mimba na aliweka matumaini yake juu ya binti  yake, sasa aliona kuwa hata Debora ni nuksi tu pale nyumbani. Furaha, raha na mizaha ndani ya familia ile sasa viligeuka kuwa karaha na kero tupu.

Siku zikazidi kusukumana, miezi nayo ikasogea kwa kasi Baba Rebeka alijaribu kufuta kumbukumbu juu ya binti yake lakini haikuwezekana hata kidogo, daima alimkumbuka binti yake. Alikuwa akichukua picha za marehemu binti yake na kuziangalia mara kwa mara. Kila alipoangalia alitiririka machozi kwa uchungu. Na muda mwingine alikuwa anachukua picha ya marehemu Mama Rebeka na Rebeka binti yake, aliziangalia na kukumbuka namna alivyoishi naye alijikuta hana thamani yoyote, ni mtu mwenye nuksi tupu hapa duniani. Alimtazama Debora na kuona naye kama alikuwa anamletea kero zaidi pale nyumbani. Alitamani hata amtafutie kosa ikiwezekana amtimue  arudi kwao, yeye abaki kivyake ajipange upya maana maisha yalikuwa yameshampiga teke.





Debora hatiani kwa unyama



Msiri wa siri ya moyo ni mwanasiri mwenyewe. Siri ni siri kwa upande mmoja tu wa mwanasiri ikishaenea kwa mwingine hiyo sio siri tena. Kauli hizi zilijidhihirisha siku ya jumamosi asubuhi, mwezi mmoja na nusu baada ya mazishi ya marehemu Rebeka aliyeuawa kikatili na kukatwakatwa vipandevipande. Siku hiyo wale vijana watatu waliohusika katika mauaji hayo walikamatwa na polisi. Waliulizwa kiundani juu ya tukio hilo, nao bila kuuma maneno walijieleza kila kitu. Walipomtaja Debora kuwa alikuwa mhusika mkuu wa tukio hilo la unyama, hata polisi walipigwa na butwaa na kwenda kumkamata mara. Walipofika nyumbani Debora alikuwa peke yake, bila maelezo wakamwambia “uko chini ya ulinzi!” Debora akapigwa na butwaa akasema moyoni mwake, “yametimia!”. Wakamsweka kwenye gari lao na kuondoka naye bila kuhitaji maelezo yake yoyote ya kujitetea. Walipofika kituoni walimpigia simu Baba Rebeka ambaye alikuwa kwenye biashara zake na kumweleza yote yaliyotokea. Alipigwa nabutwaa aliposikia kuwa Debora alikuwa mhusika mkuu wa tukio lile la mauaji ya binti yake. Alifura hasira ghafla kwa hofu akamwuliza afande, “…yaani…unataka kunambia huyo mbweha ndiye aliyemchinja binti yangu…?” Afande akamwambia, “Fika kituoni hapa basi mapema.” Baba Rebeka bila kuchelewa aliwasha gari lake na kwenda kituo cha polisi haraka. Njiani alikuwa na msongo wa mawazo alinusurika hata kusababisha ajali. Aliwaza mengi lakini furaha yake ni kwamba alikuwa amempata mbaya wake, aliyemwua binti yake. Aliwaza atamfanyia nini Debora, alitamani kama aende na panga akammalizie hukohuko lakini nafsi ilisita, alitamani achukue sumu akamnyweshe, alitamani abebe kisu au shoka akamchakaze Debora, lakini nafsi yake ilisita kufanya yote hayo.

Alipofika kituo cha polisi alikuwa amejaa hasira juu ya Debora. Afande alimsihi Baba Rebeka apunguze ghadhabu . Kisha wakamwelekeza kila hatua waliyofanya hadi kuwapata wahusika hao wa mauaji. Hivyo watuhumiwa baada ya adhabu kali za viboko visivyo na hesabu na kuburuzwa walihukumiwa kifungo cha maisha kilichoambatana na adhabu kali za kila mara. Hapo Baba Rebeka hakutamani kuiona sura ya Debora tena, akasema, “ningejua kuwa yeye ndo mhusika aliyemwua binti yangu, ningerahisisha ningemmaliza kulekule nyumbani.” Akamalizia kwa kusema, “acheni afie hukohuko huyo mbweha, sitamani hata kuiona sura yake tena”. Basi baba Rebeka aliondoka na kwenda zake nyumbani. Kule  nyumbani habari zilikuwa zimeshaenea kuwa Debora amefanya unyama ule. Kila mmoja alimlaani Debora na kutotamani kumuona tena. Usiku ule Baba Rebeka hakuweza kulala pale nyumbani kwake kwani alikuwa peke yake. Aliamua kuwasha gari lake na kuondoka jioni ileile na kwenda kijijini kwa wazazi wake. Alipofika kijijini wazazi wake walimpokea kwa masikitiko. Walipoanza kusimuliana habari za kukamatwa kwa Debora ambazo hazikuwa habari mpya pale kijijini. Watu walifedheheka sana kwa kitendo cha Debora kumwua Rebeka, kwani walikuwa wanajua kuwa walipendana sana. Wazazi wake na watu wengine wengi walijitokeza kumfariji baba Rebeka, walimsihi asahau yaliyopita na kuganga yajayo. Alijitahidi kufanya hivyo lakini kila mara alipotazama picha ambazo walipiga kama familia alitiririka machozi. Baada ya siku tatu alirudi mjini kuendelea na kazi zake za kibiashara, Debora naye akiendelea kusota kifungoni kwa kosa la mauaji ya mtoto asiye  na hatia. Hakika kikulacho ki nguoni mwako, rafiki yako ndiye adui yako.Usimwamini yeyote, amini kivuli chako. Debora aliaminika sana, lakini hakuna aliyejua kile alichokuwa anakiwaza juu ya Rebeka.



Rebeka binti aliyepata mauti bila hatia,  astarehe kwa amani katika makao ya milele mbinguni. Amina!.

Mama Rebeka, astarehe kwa amani, mwenyezi Mungu amsamehe mapungufu yake amstahilishe katika makao ya milele Mbinguni. Amina.


~~~~~~~~~~~~~~~~~TAMATI~~~~~~~~~~~~~~~~
SASA UNAWEZA KUJIPATIA NAKALA YAKO YA SIMULIZI HII KWA TSH.3000/-TU. WASILIANA NA MTUNZI.


SIMULIZI NYINGINE ZILIZOTUNGWA NAMI

ELIAS K. MWALONGO (KANTON)

NI KAMA VILE.

POKEA BARUA YANGU BELINDA-(AUDIO-1000)

KUMBE JIRANI YANGU MCHAWI-5000/-

DADANGU MCHUMBA`NGU

MACHO YANGU YANANIDANGANYA-3500/-

USIMWAMINI YEYOTE

NITAKUFA NA MTU – 1500/-

BINTI YAKO AMEROGWA

BAADHI YA VITABU VYANGU VINAPATIKANA:

1.     PERAMIHO BOOKSHOP

2.     SONGEA BOOKSHOP

3.     NDANDA BOOKSHOP

4.     NJOMBE BOOKSHOP

5.     TMP BOOKSHOP-TABORA

6.     ST.ALOIS BOOKSHOP-MBINGA

7.     ST.KILLIAN BOOKSHOP-MBINGA

8.     KANTON PRINTING - IRINGA

~~~***~~~

AU KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NAMI

MTUNZI NA MWANDISHI WA VITABU HIVI

KWA No. 0769313224

~~~AHSANTE!~~~

Na. Elias Kalistus Mwalongo

(KANTON)

1 comment:

  1. Baada ya kuwa na uhusiano naye kwa miaka saba, aliachana nami. Nilijaribu kila niwezalo kumrudisha lakini yote yalikuwa bure. Nilitamani arudi vibaya sana kutokana na mapenzi niliyonayo kwake na nilimsihi kwa moyo wangu wote, nilimpa ahadi lakini alikataa. Niliwasiliana na mganga aitwaye DR Dawn, ambaye angeweza kunisaidia kuniroga ili kumrejesha lakini mimi ni mtu ambaye sikuwahi kuamini uchawi, sikuwa na jinsi zaidi ya kujaribu. Nilimtumia barua pepe mganga huyo na akaniambia kwamba hakuna tatizo lolote, kwamba kila kitu kitakuwa sawa baada ya siku mbili na kwamba mpenzi wangu wa zamani angerudi kwangu baada ya siku tatu. Alipiga uchawi na cha kushangaza, siku ya pili, ilikuwa karibu 4:00 PM. Mpenzi wangu wa zamani alinipigia simu, tukasuluhisha tofauti zetu na sasa tuna furaha pamoja. Yeyote anayeweza kuhitaji usaidizi wa mtangazaji huyo anaweza kumtumia barua pepe kwa ( dawnacuna314@gmail.com ) au /WhatsApp kwa: +2349046229159

    Kwa uchawi wa kuungana tena.
    Kwa ujanja wa ujauzito.
    Kushinda bahati nasibu.
    Kushinda kesi mahakamani.
    Mimea ya kutibu, kila aina ya magonjwa kama,
    VVU UKIMWI Kansa malengelenge na zaidi.

    ReplyDelete

NITAKUPENDA DAIMA

Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU) Simu: 0769313224 ____________ Laazizi wangu wa moyo, nat...