BINTI YAKO AMEROGWA
Mtunzi: Elias K. Mwalongo
(Kanton)
Ruaha Catholic University (RUCU)
Simu: +25576933224 Tar. :
09/03/2017
```````````````````````````````````````````````````
Jamani mama Atu, ivi kwani umesahau
siku ile ulipojifungua, ukamzaa binti yako ulivyo furahi? Sisi majirani zako
tulipopata habari zako hatukubaki nyuma. Tukaja mbio mbio tukupe mkono wa `hongera`
kwa kuwa umeanza kuitwa Mama. Tulijua mkono mtupu haulambwi, basi
tukajibebesha, pakiti za sukari ya mtoto, pakiti za chumvi, vifurushi vya unga,
na vifurushi vingi tele tukatua kwako, tukakwambia “hongera wifi yetu, umekuwa
mama sasa”. Hatukuwa na shaka sisi juu ya malezi yako kwa mwanao. Tangu angali
mdogo tulikusihi umlee vizuri mwanao naye atakuja kukulea umri utakapokuelemea.
Hongera kwa juhudi zako. Tulikushuhudia, ukithubutu hata kumchapa bakora
alipokuwa akikosea, ndio malezi. Ulimfundisha mengi kwa kweli. Ulimtuma sehemu
alienda mara na kurudi kwa wakati. Akikutana na ndugu au watu waliomzidi umri,
ulimfundisha awasalimu kwa adabu. Asante sana, tulijinoma `shikamoo` zake.
Alikuwa mtoto mzuri, mtulivu, mwenye heshima na staha. Hakika fahari
ulijinyakulia Mama Atu, maana jema alitendalo mtoto ni fahari kwa mzazi.
Shule
umempeleka kama kawaida, tena shule za maana, sio za kubabaisha. Kwa tabia yake
matokeo yake pia yalikuwa mazuri, sifa zake tulizisikia kwa wanetu maana mwanao
alikuwa kiboko yao darasani. Fahari ilioje Mama Atu uliifaidi. Mwanao
akafahamika shuleni na hata mtaani huku, kwa tabia njema na ufaulu mzuri
darasani. Heko sana mama Atu kwa malezi uliyompa mwanao. Kidato hicho kikaisha,
akaingia cha pili, hali akizidi kuwatupilia mbali wenzake kwenye mitihani.
Tusio na kinyongo wala roho mbaya tulikwambia “hongera Mama Atu”, kisha
tukamgeukia binti yako Atu, pato lako mashuhuri la ujanani tukamwambia, “Kazana
mwanetu”. Kidato cha tatu akaingia huku matumaini yetu kwake yakibaki kuwa
makubwa. Mhula wa kwanza sifa zake za tabia ziliendelea kuvuma hapa mtaani
kwetu, japo mwishoni mwa mhula katika mtihani wake hakuwa wa kwanza tena, maana
alipitwa na Tekla binti wa Shomeho, huku Daniel yule mtoto wa Mtotofu
akiwaongozea, kwa kushika namba wani.
Tulidhani wamekosea kusahihisha au wamekosea kujumlisha alama au labda
wamechanganya alama hizo lakini wala, hizo zilikuwa alama zake mpya zilizo
halali. Tulibaki mdomo wazi kumshangaa binti yako, anakoelekea kimasomo.
Kama
kawaida yetu sisi, halilali jambo, taarifa tukazipata nasi tukazileta kwako na
kuzitua kama zilivyo. Wengine wakatwambia, binti yako hata tabia imebadirika.
Tulipoduwaa ndo wakapigilia zaidi, mara wakasema binti yako ana kiburi, mara
wengine wakasema, Atu, anadharau, mara wakasema anamajivuno. Tukabaki kuwa
wasikilizaji. Wakatuvunja ukimya walipotwambia eti binti yako anajihusisha
kimapenzi na mwanafunzi mwenzake wa kidato cha nne na kijana mmoja fundi ujenzi
hapa kijijini. Masalale! Kauli ilitutisha tukajua Atu atapotea. Kwa kihelehele
chetu tukafunga kanga kiunoni tukaja mbio tukusihi UMKANYE MWANAO. Tukarudi
tumelowa matusi. Ulitutusi tulipokusihi umkanye mwanao maana anakoelekea
kubaya. Ulituzodoa, ukatubinulia midomo usitake kuzingatia ushauri wetu.
Tuliambiwa tukaja kukwambia, ukatutusi, hata matusi ya nguoni ili tukome kabisa
kukufatilia. Mama Atu, tunakumbuka yale matusi yako eti, “mtakwisha kuni zenu
kwa kutupikia machegea, na hatutalia gizani kwa kuwaogopa majirani. Yenu
mwayatia mfuniko yangu mwayachezea mdundiko. Hakika, Mola nipe radhi mie kuishi
na watu kazi….” Haya Mama Atu!. Uliona kuishi na sisi kazi, tulipokuasa uliona
tunakufatilia, haya sasa binti yako hatamaniki.
Binti
yako uliyejivunia sasa AMEROGWA. Ulimfundisha kusalimia, sahizi hatuambulii
salamu yoyote toka kwake. Tukimuita japo kwa nia njema, anatubinulia midomo.
Wageni tukifika kwako, binti yako anatudharau. Yeye nyumbani hakukaliki,
anashinda anazurula wapi, sisi hatujui. Halafu, jamani Mama Atu, na hizo nguo
ambazo mwanao anavaa mbele za watu unamnunulia wewe mwenyewe? Anatulia aibu
sisi wazazi wake. Sura yake masikini, kwani pale zamani alikuwa mweupe hivi au
amejichubua? Jamani, ivi ni Atu yuleyule tuliyemletea, pakiti za sukari siku
ile? Ndiye yule tuliyekuja kumsalimu kwa furaha na bashasha tukampakata
mikononi mwetu nasi tukajisikia fahari? Ni yule yule Atu alikuwa akiongoza
mitihani darasani na kuwapita wanetu? Ndiye Atu yule aliyevuma kwa sifa kemkem
hapa mtaani?. Halafu naomba kuuliza, kama ni unoko wacha niwe mnoko tu, Atu
alikuwa akisoma darasa moja na binti yangu Faraja, binti yangu alipitwa na Atu
kila mtihani maskini, na sikutaka hata kulinganisha, nilimchukulia mwanangu
kama kilaza ukimlinganisha na wako. Lakini eti, Atu ana cheti cha kidato cha
nne? Ana cheti cha kidato cha sita? Au kote huko mbali mno, mtihani wa kidato
cha nne alifanya?? Kulikoni Mama Atu?? Binti yangu Faraja, alihitimu hadi
kidato cha sita, na sasa na chakarika kukusanya visenti binti yangu amalize
chuo. Isitoshe hata mkopo amekosa, lakini kwa namna yoyote ile atasoma, hata
bagia nitatembeza, nipate chochote mwanangu asome. Tabia yake bado inaridhisha,
namtegemea atakuja kunisaidia umri utakaponielemea. Mama Atu mimi nilimkanya
alipoonesha kubadili tabia na kufata mikumbo, nilikaa naye na kumuelimisha
mengi juu ya maisha haya. Wewe ulikaidi, ulisahau kuwa anaweza kubadirika.
Dunia imemroga, Utandawazi umemroga, Digitali imemroga, Makundi mabaya
yamemroga. Sasa yuko hapo alipo, amechoka hatamaniki, japo umri wake bado mdogo
lakini anapakata mtoto wake mchanga, ambaye sisi hadi leo hatujui baba yake ni
nani. Mdharau mwiba mguu huota tende, endelea kumlea binti yako, mlee pia na
mjukuu wako maana hakuna namna. Tulipokuasa tulikuwa na nia njema na sio
kukufatilia. Kila mmoja anavuna alichokipanda Mama Atu. Tukutakie kila la kheri
na maisha mema.
___________________________
KWA MAONI NA USHAURI, WASILIANA NA MTUNZI WA TUNGO HIZI ELIAS MWALONGO - 0769313224

No comments:
Post a Comment