Thursday, 28 September 2017

Salaamu Watwana!

Mtunzi: ELlias K. Mwalongo (Kanton)
SIMU: +255769313224,
E-Mail:mwalongoelias7@gmail.com
_______________________

Shukrani nyingi kwa Mungu aliyeniumba na kuendelea kunipigania hadi siku hii ya leo. Tumaini langu ni kwake pekee.
Wapendwa, wana wa ulimwengu huu shupavu,ukipanda mahindi unatarajia kuvuna mahindi lakini pia unaweza usivune ila huwezi kuvuna korosho! Majaribu katika maisha ni mtaji wa kujivunia maana yamejaa utukufu na neema tele tele!
Ni vigumu sana kumzuia kuku asitage, hata ukimfungia mlango atataga tu hata kama ni porini. Hivyo hakuna anayeweza kuzuia mipango ya Mungu ndani ya maisha yako.
Wapendwa, msione kuku kachinjwa mkaanza kumparamia mjinome minofu, hali hamjui ni visu vingapi vimemchinja kuku huyo. Vingine huwa vina kutu, mtapata tetenasi bure.
Si kila mnachokiona kinang`aa mkadhani kipya, vingine ni vibovu kabisa ila vimepakwa rangi tu ili kuficha ubovu wake na kukuvutia wewe. Angalieni wapendwa msije mkaruka mwiba mkakanyaga msumari, halafu make chini hatakama kuna tope.
Ya dunia ni mengi, mengine hayawahusu. Kazaneni na yanayowahusu, maana kushuparia yasiyowahusu mtachelewa kufanya yanayowahusu.
Muweni makini na wale wanaokalia vigoda na kuanza kuhadithia ya wenzao, maana utakapoondoka watawawahathia wengine ya kwako. Tena hawajazoea kusema ya kweli. Ukweli wanaupotezea, uongo na uzushi mara moja utafika mtaa wa saba. Mbaya zaidi, yao wanayatia mfuniko na ya wenzao wanayachezea mdundiko.
Wacha nifunge ginywa langu niache kubwabwaja, lakini kabla sijakoma, wacha nimalizie aya hii moja ya mwisho.
Wapendwa, tufanye kazi. Kazi ni kazi. Usidharau kazi ya mwenzako hali humchangii hata mia ya kula, wala hujui anavaa nini au anakula nini na maisha yake yanaenda vipi. Tuheshimu kazi zetu na kazi za wenzetu. Tuongeze juhudi katika kazi, kupata na kukosa ni matokeo ya juhudi zetu, tusikate tamaa.


NAWATAKIENI KILA LILILO JEMA NA KUDRA ZA MWENYEZI ZIWE MHIMILI WA MAISHA YETU SOTE.

_________AHSANTENI_________


 Maoni na ushauri wako ni mhimu sana kwangu kusonga mbele.

Friday, 15 September 2017

SALAMU ZANGU KWAKO SABRINA

_____________Simulizi Fupi_______________
Salamu Zangu Kwako
Sabrina
Mtunzi: Elias K. Mwalongo(Kanton)
Ruaha Catholic University (RUCU)-Iringa
Simu: +255-769-313-224

____________________________
Ni kipindi kirefu sasa kimepita, sijaiona sura yako Sabrina. Barua nyingi nilizokuandikia, zote umezipuuzia. Nimejaribu kukupigia simu walau nikusalimu  na kama hutaki kuisikia sauti yangu basi walau uisikie sauti ya mwanao akilia kwa uchungu kukukosa mama yake, lakini hukutaka kupokea na mara nyingine uliona nakusumbua ukakata simu yangu kwa jeuri.
Kama ni kuumia, Sabrina umeniumiza nimechakaa niko hoi kabisa. Kila nikisoma zile meseji zako mbili za mwisho ulizonitumia kwa njia ya simu yangu,pale nilipokutakia hali, najikunyata nadhoofika moyoni nalia na kutetemeka mwili mzima. Sitakujakuzifuta  meseji hizi, wacha ziendelee kuniliza. Huenda umesahau ulivyoniandikia, nanukuu kutoka katika simu yangu ya kiganjani, uliniandikia hivi: “we bwege ukome kabisa kunisumbua, hadhi zetu hizi unazionaje, zinalingana? Mwanaume gani unashinda umekalisha nyumbani kamafurushi? Mi mwanamke mzuri nahitaji matunzo, unauwezo wewe wakunitunza? Eboo! Umeshindwa, waachie wanaoweza kunihudumia. Acha kuniletea uchuro we fisi kongwe”. Niliupokea ujumbe wako huu, nilipomalizia kuusoma, tone la chozi lilidondokea kioo cha simu yangu. Ujumbe wako ulinipa hasira, nikairusha simu yangu chini kwa nguvu labda ingepasuka, lakini wapi, nilipotaka kuikanyaga kwa kisigino changu ili ipasuke kabisa, nikiwa nimeinua mguu juu, kabla sijashusha ikaanza kuimba ule wimbo wa Joseph Chamelion unaoitwa `Mama Neema`, nikajua tu kuwa ujumbe ulikuwa unaingia. Nikashusha mguu wangu kwa upole nikaichukua ili nione ujumbe huo. Kumbe na huu pia ulikuwa umetoka kwako ukiendelea kushindilia matusi. Yaani Sabrina uliona haitoshi, kabla sijakujibu ukaongeza ujumbe mwingine ukinambia, “kila mmoja aishi kivyake, sitaki unifatilie maisha yangu. Kama ni mapenzi mimi na wewe yaliisha kitambo. Mimi nina maisha yangu na wewe uishi maisha ya kwako. Ukiendelea kunisumbua, nitakuja kukufanyia kitu kibaya hutanisahau maisha yako yote.”
Hapo ndipo ulipokomea ujumbe wako wa pili. Kila nikikukumbuka narudia kuusoma, najikuta machozi yanatiririka mashavuni mwangu nakudondoka chini tone moja moja.
Sabrina mpenzi, wacha nikuite tumpenzi japo sasa sistahili tena kukuita hivyo. Katika ujumbe wako umenitishia kunifanyia kitu kibaya endapo nitaendelea kukufatilia, ni kipi hicho kitu kibaya zaidi ya hiki ambacho umenifanyia? Kama ni kuniua, Sabrina njoo unimalizie nijinafuu na suluba ninazopata.
Hivi kweli Sabrina umesahau kabisa tulikotoka? Hukumbuki hata moja kati ya yale tuliyoyapanga kuyafanya maishani mwetu? Uliahidi hutaniacha niteseke, utakuwa nami katika kufurahi na katika suluba za dunia hii, au siwewe ni Sabrina mwingine? Umesahau kabisa upendo wote nilio kuonyesha?.
Kibarua changu kidogo cha udereva wagari la shule, kilitulisha na kutuwezesha kulipa pango la nyumba, tulikula tulivyotaka, tulivaa vizuri, mwanetu mdogo naye akapata matunzo aliyostahili na mambo mengine wala hayakwenda mrama. Nilipoachishwa kibarua hicho japo kwa hila tu za wanadamu wenye wivu, Sabrina ulibadirika ukawa mbogo. Je ulinipendea vishilingi vyangu vilivyotuwezesha kujivinjari? Ni kweli hukuniweka moyoni? Kukupenda kote kumbe nilikuwa najipendekeza tu. Nayakumbuka maneno yako mazuri ya kimahaba ambayo hukuacha kunitamkia. Ninayakumbuka vema kwani maneno hayo hatimaye yamebadirika kuwa matusi ya kunidharau. Sabrina, hivi kweli wewe wakuniita mimi bwege, leo wewe unaniita mimi fisi kongwe. Nilipokuwa muwele ulinipetipeti nakunikanda mgongoni lakini leo unaniona furushi kweli.
Sabrina, mimi ni yuleyule mpenzi wako niliyekupenda na bado nakupenda. Nilipotoka kwenye pilika za maisha ulinipokea kwa furaha na bashasha, tena furaha iliyosindikizwa na kumbatio la mahaba na kuhamasishwa na busu la upendo. Mimi ni yule yule, labda umesahau ulivyokuwa ukijilaza kifuani pangu na kunibembeleza kwa maneno mazuri huku ukiahidi kuwa nami katika hali yoyote ya maisha.
Sina kibarua tena, wala sina pesa za kusaza. Wenye pesa zao wanakutunza, bila shaka sasa unajinoma. Bila shaka, unakula unachotaka, unalala kwa starehe, hutembei kwa miguu tena. Huenda umesahau sasa umasikini wa kwetu wa kula ugali wa sembe, viazi, kande na matembele. Siamini kama Sabrina unachota maji mtoni tena kama ulivyokuwa ukifanya huku kwetu. Naamini kila kitu kwako kipo katika mstari, na maisha yako murua. Hongera sana Sabrina kipenzi changu niliyekupenda kwa dhati.
Mimi peke yangu ningeweza kujizila nikaendelea kuganga na maisha niwezavyo lakini umemsahau na mwanetu Marcelina. Binti yetu angali mdogo pato la ujana wetu,   kwa hakika kumlea peke yangu sitaweza. Mwanetu Marcelina ni damu yetu sote lakini umembwaga umeenda. Nimekuwa baba yake na mama yake. Akilia ni kazi yangu kumbembeleza, hakika nimekuwa yaya mzoefu sasa. Nilipokupigia simu na kukusihi urudi tumlee mwanetu ulinitukana matusi ya nguoni. Leo naandika barua hii ili nikusalimu tu. Naomba pokea salamu zangu Sabrina. Utakapo kujua hali yangu, si shwari hata kiduchu. Nimekuwa mtu wa kujiinamia chini na kudondosha machozi kwaajili yako. Sikukukosea lolote kwa hakika, umasikini wangu na maisha duni vimekufanya uone sina maana kwako. Asante Sabrina, asante sana.
Nikikupigia simu hupokei, na wakati mwingine unaikata kwa jeuri. Nikituma ujumbe haujibiwi, basi nakuandikia barua hii ili walau nikusalimu. Natamani salamu hizi zikufikie. Kama na salamu hizi hazitakufikia au hutaisoma barua hii ya salamu basi walau hata asome mtu mwingine yeyote kisha akufikishie salamu walau ujue tu kuwa mimi Baba Marcelina nakusalimu.
Nakukumbuka sana Sabrina, japo umeona sina thamani, umenitupa mimi na mwanangu Marcelina kisa pesa za wenyenazo. Nilikupenda nakukujali sana, lakini sasa penzi letu limetumbukia nyongo. Naomba pokea salamu zangu Sabrina Nakutakia maisha mema, nami naendelea kuganga kwa uwezo wa Jalali. Panapo majaaliwa tutaonana.

____________TAMA TAMA TAMATINI______________


Wasiliana nami mtunzi kwa maoni na ushauri ili kazi zangu ziendelee kuboreshwa na kuwa hitaji haswa na wasomaji wangu. Ahsante!

Wednesday, 6 September 2017

NISAMEHE JUDDY
Na Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo
Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU)
Simu: 0769313224



Nafadhaika moyoni na nafsi inasononeka kwa uchungu mkubwa ulionikumba. Ninajiona ni mkosefu na kila mwanadamu ninayemwona anastahili kunisomea hukumu ya kosa langu nililolifanya. Ninajiona kabisa nimemkosea Mwenyezi na tawala zake zote. Nimeikosea jamii yangu yote na ninastahili adhabu nzito. Nimekukosea mpenzi wangu Juddy na ninastahili hukumu yoyote toka kwako. Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Najisikia soni mbele ya yeyote ninayepishana nae. Natembea kichwa chini ili kuficha soni mbele ya macho ya walimwengu. Hata yule ambaye hatambui kuwa nina kosa mimi ninahisi nimemkosea mno. Juddy kipenzi changu natambua kuwa ninastahili adhabu mimi.
Hata hivyo ninachukua kalamu yangu ya risasi na karatasi, ninapiga magoti chini, tena chini kabisa sakafuni ili niandike kwa ufanisi nikikuomba msamaha. Ninayaandika haya ambayo ninatamani yakufikie lakini sijui msamaha wangu utafikaje huko uliko. Sijui nitumie anuani gani ili barua yangu ya msamaha ikufikie huko.
Mpenzi, tulikotoka ni mbali na tumeyapitia mengi ya kutufurahisha na yakutuhuzunisha. Kauli zangu za kutaka nijenge maisha na wewe zilikufanya ukanikubali na ukaamua kuzama katika mahusiano nami. Nilikusihi utulie ubaki nami, nilikuasa mengi ya kujenga, nawe kwa moyo radhi ulitii. Ulinipa heshima zote, ulinijali na kunilinda, ulinipa nafasi kubwa ndani ya moyo wako.  Nilijinafasi haswa. Hata hivyo sikutilia maanani upendo wako. Bado niliendelea kujivinjari na wengine ambao sikuweza kujificha. Nikisema upendo wangu ulitoka moyoni nitakuwa nakuongopea. Hakika nilikutamani kama nilivyo watamani wengine. Ukagundua mwenendo wangu, hata hivyo ulizidi kuwa mwaminifu kwangu. Ulivumilia mengi na kuyapuuza mapungufu yangu. Maneno ya mashoga zako wala hukuyajali uliendelea kunijali. Leo nimekupoteza kipenzi changu ninajuta na kujilaumu. Ninajiona mkosefu ninayestahili adhabu. Sijui kwanini sikuwa na huruma hata nikakufanyia yote hayo. Ulijitahidi kunionyesha mapenzi ya dhati lakini sikuwa tayari. Uliponipenda kwa dhati mimi nilikupuuza na kukuchukulia kama watu wengine niliowatamani.
Ninaikumbuka vema siku ile, uliponijia kwa furaha na bashasha, ukanirukia na kunikumbatia ishara tosha kwamba ulikuwa na jambo la kufurahisha ulitaka kuniambia. Naamu jambo ulikuwa nalo na halikuwa dogo. Kwa furaha zote ulinambia kuwa ulikuwa na mimba yangu. Jambo hili lililokupa furaha, mimi lilininyima raha kabisa. Uligundua kuwa sikufurahishwa na taarifa hiyo. Nilibadirika ghafla nikaondoka na kukuacha peke yako. Niliingia chumbani na kujilaza kitandani. Mara ukaingia chumbani na kuniita kwa sauti ya upole. Bila kuitika wala kusema lolote nilivaa viatu na kutoka nje nikawasha gari na kwenda kujivinjari na wenzangu. Nilikufedhehesha sana mpenzi wangu, lakini wala sikujali maumivu yako.
Nilirudi usiku ukiwa umelala lakini ulinifungulia mlango nikaingia ndani. Sikula chakula ulichoniandalia, kwa jeuri niliingia moja kwa moja chumbani nikalala bila hata kukuongelesha. Hakika nilikutesa sana. Nilikuona ukiteseka na kushindwa kupata usingizi lakini wala sikujali.
Kulipopambazuka nilikuacha ukiwa umejiegesha kitandani, nikajiandaa haraka na kutokomea mtaani katika vibarua vyangu vya kila siku.
Uamuzi ulioamua kuuchukua siku hiyo hakika ulinifanya nikulilie. Juddy sikuwahi kulia kwaajili yako lakini siku ile nililia machozi yakanitiririka kwaajili yako mpenzi. Nilifurukuta na kuilaumu nafsi yangu lakini sikuwa na namna, sikuweza kulizuia jambo ambalo lilikuwa limeshanikumba.
Ni kweli nilikuumiza sana, nilikushuhudia ukilia na kushindwa kula. Siku hii uliamua kwenda kwa daktari na kutoa mimba maana ulijua kuwa taarifa ya kuwa ulikuwa umeshika mimba ndiyo iliyonifanya nibadirike na kuwa mbogo. Naye daktari alizipokea za mchuzi na kuianza shughuli ya kukiua kiumbe kisicho na hatia kilichokuwa tumboni mwako. Najua ulidhamiria kuitoa mimba ili unifurahishe, lakini kumbe ulikuwa unaelekea kuniliza. Mchakato ulifanikiwa, kiumbe cha Mungu tumboni mwako kilisagwasagwa, kilikatwakatwa na kutolewa nje kisha kikatumbukizwa kwenye dishi fulani bovu na kisha kutupwa chooni kama uchafu. Maskini mwanangu nikampoteza! Nawe uliendelea kuugulia kidoda, maumivu yalikuzidi, damu nyingi ilikutoka mfululizo hata kukusababishia ukapoteza maisha!
Nimekupoteza mpenzi wangu Juddy kwa uzembe na nimempoteza mwanangu aliyekuwa akinawili tumboni mwako. Lengo lako lilikuwa kunifurahisha mimi lakini ndo umenifanya nilie kwaajili yako.
Natamani kama vile ufanyike muujiza, siku zirudi nyuma ndo iwe siku ile unaponiambia kwa furaha kwamba una mimba yangu, nami niipokee taarifa kwa furaha na bashasha nikushukuru na kukununulia zawadi nono. Natamani ndo zirudi zile siku ulizonipenda na kunithamini nami nithamini upendo wako, nikupende kwa dhati, nijitoe mzima mzima kwaajili yako bila kujibakiza. Lakini nimechelewa.
Nimegundua kuwa nimekuwa mkosefu kwa kila aliye mbele yangu. Ninastahili kuadhibiwa laikini ninapiga magoti chini naandika barua hii nikiomba radhi mbele yake Mungu na tawala zake zote, mbele ya walimwengu wote na zaidi sana mbele yako kipenzi changu Juddy. Hakika naomba NISAMEHE JUDDY, sikudhamiria yatokee haya ambayo yametokea. Natamani ombi langu hili la kuomba kusamehewa likufikie huko uliko ili ujue jinsi moyo wangu unavofukuta kwa uchungu. Hakika barua hii ikikufikia na ukaisoma NAOMBA UNISAMEHE JUDDY.



TAMATI

NITAKUPENDA DAIMA

Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU) Simu: 0769313224 ____________ Laazizi wangu wa moyo, nat...