Thursday, 28 September 2017

Salaamu Watwana!

Mtunzi: ELlias K. Mwalongo (Kanton)
SIMU: +255769313224,
E-Mail:mwalongoelias7@gmail.com
_______________________

Shukrani nyingi kwa Mungu aliyeniumba na kuendelea kunipigania hadi siku hii ya leo. Tumaini langu ni kwake pekee.
Wapendwa, wana wa ulimwengu huu shupavu,ukipanda mahindi unatarajia kuvuna mahindi lakini pia unaweza usivune ila huwezi kuvuna korosho! Majaribu katika maisha ni mtaji wa kujivunia maana yamejaa utukufu na neema tele tele!
Ni vigumu sana kumzuia kuku asitage, hata ukimfungia mlango atataga tu hata kama ni porini. Hivyo hakuna anayeweza kuzuia mipango ya Mungu ndani ya maisha yako.
Wapendwa, msione kuku kachinjwa mkaanza kumparamia mjinome minofu, hali hamjui ni visu vingapi vimemchinja kuku huyo. Vingine huwa vina kutu, mtapata tetenasi bure.
Si kila mnachokiona kinang`aa mkadhani kipya, vingine ni vibovu kabisa ila vimepakwa rangi tu ili kuficha ubovu wake na kukuvutia wewe. Angalieni wapendwa msije mkaruka mwiba mkakanyaga msumari, halafu make chini hatakama kuna tope.
Ya dunia ni mengi, mengine hayawahusu. Kazaneni na yanayowahusu, maana kushuparia yasiyowahusu mtachelewa kufanya yanayowahusu.
Muweni makini na wale wanaokalia vigoda na kuanza kuhadithia ya wenzao, maana utakapoondoka watawawahathia wengine ya kwako. Tena hawajazoea kusema ya kweli. Ukweli wanaupotezea, uongo na uzushi mara moja utafika mtaa wa saba. Mbaya zaidi, yao wanayatia mfuniko na ya wenzao wanayachezea mdundiko.
Wacha nifunge ginywa langu niache kubwabwaja, lakini kabla sijakoma, wacha nimalizie aya hii moja ya mwisho.
Wapendwa, tufanye kazi. Kazi ni kazi. Usidharau kazi ya mwenzako hali humchangii hata mia ya kula, wala hujui anavaa nini au anakula nini na maisha yake yanaenda vipi. Tuheshimu kazi zetu na kazi za wenzetu. Tuongeze juhudi katika kazi, kupata na kukosa ni matokeo ya juhudi zetu, tusikate tamaa.


NAWATAKIENI KILA LILILO JEMA NA KUDRA ZA MWENYEZI ZIWE MHIMILI WA MAISHA YETU SOTE.

_________AHSANTENI_________


 Maoni na ushauri wako ni mhimu sana kwangu kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment

NITAKUPENDA DAIMA

Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU) Simu: 0769313224 ____________ Laazizi wangu wa moyo, nat...