Friday, 27 January 2017

KAZI YANGU ITANILISHA-MTUNZI: ELIAS K. MWALONGO(KANTON)



KAZI YANGU



I T A N I L I S H A
(DIWANI YA KANTON)

  


ISBN  978 9976 67 189 6



~~~~~~+++~~~~~~


 
MTUNZI;

Elias K. Mwalongo (Kanton)

KAZI YANGU ITANILISHA
@Copyright by: Elias K. Mwalongo
S. L. P 977 Njombe
0769313224
E.mail: mwalotz@gmail.com                        
Facebook: Elias Mwalongo
Twitter: Elias Mwalongo
Instagram: @mwalongoelias

Wahariri

1.Pd. Lucas Komba
   Seminari Kuu Peramiho
2. Frt.Witney Selig Ngahi
    Seminari Kuu Peramiho
3. Ndg. Oswald Ngonyani
    Mhariri Mkuu Peramiho Publications

Kimechapwa Na;

Kanton Printing
S.L. P 977 Njombe
0769313224
E.mail: mwalotz@gmail.com


Chapa Ya Kwanza, Februari 2016

Haki zote zimehifadhiwa.Huruhusiwi kuiga, kupiga chapa, kutafsiri au kukitoa kitabu hiki kwa jinsi yoyote ile pasipo idhini ya mwandishi wa kitabu hiki au mhariri mhariri wake.Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika.



***

Diwani yangu hii ya KAZI YANGU ITANILISHA, nimeiandika kwa heshima ya wale wote ambao wamekuwa wakinihamasisha katika fani hii ya uandishi. Naamini wao ndio walionitia moyo hata nikafikia hapa. Ningetamani kuwaandika majina yao yote katika ukurasa huu maana ninawakumbuka vema, lakini hilo sitaliweza, hivyo nitajitahidi niandike baadhi yao tu ambao ni:

Pd. Atanas Mgimba
Pd. Ladislaus Mgaya
Frt. Sergio Kaberege
JohnBaptist Ngatunga
Dotto Rangimoto Chamchua
Gasto Mtitu
Godfrey Songolo
Joseph Chatanda
Simon Mgaya
Eligia Mwalongo
Antonia Mtega



***

+Katika makao ya milele mbinguni, Astarehe kwa amani baba yangu mpendwa;
KALISTUS MWALONGO,
aliyenitoka mwaka 2002 ningali siwezi kujikimu.        
         

                                                            ***
KAZI YANGU ITANILISHA  ni kitabu kinachopembua kwa uzito masuala nyeti ya maisha ya kizazi hiki. Katika kitabu hiki cha mashairi, kuna majibu ya maswali mengi yanayomsakama Mtanzania wa leo. Masuala hayo ni kama vile kifo, mapenzi, utandawazi, tamaduni na kadhalika. Wanazuoni mnaweza kupata pia mawazo mengi juu ya umhimu wa kuwaheshimu wazazi,katika shairi la “Asante Sana Mama”,”Asante Sana Baba” na “Asanteni Sana Wazazi”. Pia kuna umhimu wa kutokata tamaa katika maisha,hasa unaposhindwa kupata mafanikio unayoyasumbukia kwa mudda mrefu katika shairi la “Huenda Kesho N`tapata”
Nimeguswa pia na mashairi yanayoelezea juu ya siasa zisizo na ukweli katika utendekaji wake na udanganyifu uliojaa na kutuama katika siasa za nchi zetu zinazoendelea. Haya unayapata katika shairi la “Msing`ate Kucha” na lile la “Nani Atatupa Pole”.
Hali kadhalika mtunzi wa kitabu hiki amefaulu kwa kiasi kikubwa kabisa kujitawanya katika nyanja za msingi zinazomgusa binadamu.Mambo ya kiroho,kijamii, na hata kisiasa yapo katika kitabu hiki.Mambo ya utandawazi yanayowaharibu vijana na hata watu wazima na wazee wa nyakati hizi yanaelezwa na kupewa ufumbuzi katika kitabu hiki. Kuacha tamaduni zetu zilizofunzwa na wazee wetu na kukimbilia kuiga tamaduni za kigeni pasipo kuelewa na kujielewa, ni janga kwa jamii zetu.
Basi mpendwa msomaji, uhondo ndio huu. Yapo mengi sana yatakayokufaa wewe katika maendeleo chanya ya fikra na hata katika nyanja za kisiasa kiroho na hata kijamii. Kwenu ninyi nyote, yaliyomo humu ni mchango mkubwa katika mabadiliko muhimu kwako na kwa nchi yetu.Yapo mengi ya kuwafaeni katika maisha toka kitabu hiki cha KAZI YANGU ITANILISHA.
Na;
Frt. Witney Selig Ngahi
Seminari Kuu Peramiho


                                                              
UTANGULIZI

Ni ukweli usiopingika kuwa katika maisha yetu hapa duniani tunatofautiana kwa kiasi kikubwa hasa katika kujikimu.Wapo watu wengine ambao hali zao kiuchumi ni njema, mifuko imetuna, chakula nyumbani hakipigi chenga tena chakula kizuri.Wapo wanaotinga suti za bei mbaya na kutundika tai shingoni,viatu vya kiwi vilivyochongoka mbele.Wana masimu makubwa, ya kupangusa. Hawatembei kwa miguu,wanamashangingi na maprado ya kufa mtu. Wanakunywa vinywaji vya gharama sio ulanzi wa shilingi mia nne kama tunavokunywa sisi. Sawa ni vyao na wala tusiwaonee kijicho.Lakini wapo wenzangu na mimi kapuku kabisa, tukibahatika kula leo hatuna uhakika wa kula kesho. Mavazi yetu ndo usiseme, ni aibu tupu mbele za watu. Hatujali kwa kulala ilimradi ikifika kesho na sisi tuwe bado tunapumua. Sisi ambao huenda tunastahili hata kuitwa majina mabaya kama vile machokoraa. Sisi ambao mtu akitupatia lifti japo kwenye baiskeli wakati wa jua kali la kiangazi tunamwona ni mkombozi wetu, mtu akitupatia mihogo miwili tutafune wakati tuna njaa yetu tunamwona ndiyo Mungumtu. Ni dhahiri thamani yetu ni duni sana mbele za wenzetu.
    Lakini ndugu, licha ya tofauti hizi zote haimaanishi tubaguane, tugombane, tusengenyane, tunyosheane vidole, tuzodoane au tudharauliane. Wapo watu waliobobea na ambao ni hodari wa kujadili ya wenzao tena yasiyowahusu badala ya kuendelea na yao. Yetu wanayachezea mdundiko yao wanayatia mfuniko. Kule kwetu watu wa tabia hiyo wanaitwa Wambea. Waswahili wanasema, “Sitalia gizani kwa kuwaogopa majirani”. Wambea shauri yao wenyewe, watakwisha kuni zao kwa kunipikia machegea, wengine wamemaliza ndala zao kwa kutusimanga wongo mitaani.
Katika kuiandika Diwani yangu hii,nimegusa nyanja mbalimbali za maisha. Lakini hasa nimejikita katika kuongelea kipato cha mtu ambacho humfanya awe na maana mbele za watu au laa. Nimejaribu kuhamasisha kila mmoja kukazana kujituma katika kazi yake ambayo ndiyo humpa shibe. Maana, MTU KITU. Asiyekuwa na kitu hata thamani yake hutoweka, huonekana hana thamani mbele ya wenyenavyo. Yapo yapo mambo yanayoweza kutufanya walau mara moja tutabasamu lakini yanayotuliza ndio yamezidi. Lakini hatuna namna inatupasa kupambana na pilika pilika za maisha haya hadi kieleweke, kwani wangapi wamefanikiwa.
Zipo sera zinaibuka kila kukicha hasa hapa kwetu Tanzania, na sisi ndio tunazishobokea na kuzipigia makofi tukidhani zote zitatufaa. Wakisema “KILIMO KWANZA” tunatabasamu na kupigia makofi. Lakini mbona somo la kilimo limefutwa darasani? Tunasema tukuze vipaji vya vijana lakini somo la Stadi za Kazi shuleni tunalibeza na kulifuta kwenye mitaala shuleni. Watu wa dini tofauti wanavyovurugana wanapigana bunduki wanarushiana mikuki na kumwagiana tindikali tunashikilia vichwa tunahuzunika, tunaita na vikao vya dharura hali Dini haifundishwi mashuleni, watu hawashiki imani yao badala yake wanaleta ubabe.
Wanafunzi ndio wasomi tunategemea mabadiliko katika jamii lakini wengi wao hamna kitu, miaka inaisha anarudi kama alivyoenda, zaidi wanaongezeka miili na kuota ndevu. Je wanafundishwa nini darasani? Kilimo? Hapana! Uchumi? No! Ujasiliamali? No, kwanza haipo hata kwenye Silabasi.Watanzania wenzangu, Mimi naona HAPA TUMECHEZA FYONGO!
Mimi nisikuchoshe jisomee mwenyewe ufaidi uwasimulie na wenzako mambo yamo ndani ya kitabu hiki. Ukimaliza kusoma kitabu hiki bila shaka utatamka pamoja nami kuwa KAZI YANGU ITANILISHA.

Na;
Elias K. Mwalongo (Kanton)
Ruaha Catholic University

ILI KUPATA NAKALA HALISI YA KITABU HIKI WASILIANA NA MWANDISHI KWA SIMU NO. +255769313224
UTAMJULISHA ULIPO NAYE ATAKUELEKEZA NAMNA YA KUKIPATA.
ASANTE SANA

No comments:

Post a Comment

NITAKUPENDA DAIMA

Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU) Simu: 0769313224 ____________ Laazizi wangu wa moyo, nat...