Thursday, 26 January 2017

SISI HATUANDIKI UPUMBAVU!!




 HATUANDIKI UPUMBAVU!!

Mtunzi na Mwandishi
ELIAS KALISTUS MWALONGO
(KANTON)
RUAHA CATHOLIC UNIVERSITY(RUCU)
+255769313224 

@2017



Mpendwa Muungwana  na mzalendo wa nchi hii, SALAAMU……………………!

Tukiwa tunaelekea kuumaliza mwaka huu 2016, na tukiwa tumejaa matumaini ya kuanza mwaka mwingine 2017 kwa amani, naomba nitumie fulsa hii adimu kutoa tathmini yangu juu ya fani ya uandishi. Ninajikita katika fani hii maana ndio kipaji alichonijalia mwenyezi, lakini sasa fani hii hasa hapa kwetu Tanzania naona imebutuliwa mateke inachechemea huenda tukaiua sisi wenyewe, kwakuwa hatusomi walivyoandika wenzetu na kuvitendea kazi, na hasa kama mwandishi unamfahamu ndio kabisa anabezwa na kazi yake hainunuliwi,haisomwi na hatimaye anakata tamaa.

Mpendwa, unatuchukuliaje sisi tunaochukua kalamu, tukaketi chini na kuwaandikia tungo zetu(MASHAIRI, SIMULIZI,TENZI, MAKALA n.k) kwa mfano mimi je,unanichukuliaje? Ukisikia safari hii nimetunga kitabu kinaitwa MACHO YANGU YANANIDANGANYA, je wewe unanichukuliaje?

Nakuhakikishia kwamba sisi waandishi hatupotezi muda tukakaa chini halafu tuandike UPUMBAVU. Hata kama tunafahamiana na daima maongezi yetu kila siku ni ya kawaida kabisa lakini mwenzio ninajambo ninaloliweka katika maandishi, naomba uniunge mkono. Sidhani kama kuna mtu atajitetea hapa, wewe mwenyewe unayesoma makala hii ni mvivu mkubwa wa kusoma kazi za wenzako. Ukiona Whatsup, au Facebook mtu ameandika maelezo marefu unapotezea, je unadhani huyo mwenzako ameandika UPUMBAVU. Ametumia muda akakuandikia habari hiyo ikufikie, wewe unasababu gani ya kupotezea? Kila siku unalalamika maisha magumu, wanajitokeza watu wanaandika mbinu za kujinafuu na ugumu wa maisha wewe unapotezea tu kama kawaida yako. Ndugu yangu, hebu acha dharau hizo, sisi HATUANDIKI UPUMBAVU.

Unatamani kujitetea? Kama nimekuonea nipigie simu namba hii +255769313224, au kama upo Iringa hapa njoo tuonane ujitetee. Lakini kabla hujachukua uamuzi huo wacha nikudhihirishie kuwa sisi waandishi umetudharau sisi na vyote tunavyoviandika, hebu nambie kama umesoma vitabu vifuatavyo: Kama ndio  njoo jitetee nitakununulia mirinda ya baridi, na kama sio ukome kutudharau sisi waandishi…!

Je umewahi kukiona na kukisoma kitabu kiitwacho JINSI JINI ALIVYOLISUMBUA PENZI LANGU kilichotungwa na GODWILL SANGA wa chuo kikuu cha KAMPALA –Dar?

Je umewahi kusoma vitabu viitwavyo “MARAFIKI NA MAADUI WA WATOTO” na “BORA KUWA KOBE” vilivyotungwa na Frt. Isaya Nyambo wa SEMINARI KUU PERAMIHO?

Tena, umewahi kusoma mashairi mazuuuuri yaliyopo katika kitabu kilichotungwa na EZRA ESSAU MHONDA kiitwacho “JASHO NA MACHOZI YA DAMU YALINITOKA?   

Umewahi hata kukiona tu Kitabu kilichotungwa na binti mdogo tu YUSTINA DANDA, amehitimu kidato cha nne mwaka huu, simulizi nzuri ya kusisimua iitwayo FURAHA BAADA YA MACHOZI?

Bado, Je umewahi kusoma simulizi yoyote kati ya hizi, “THE ADVENTURE OF ANALIZE,” au “TUNDU LA KAA” zilizotungwa na katoto kadoooogo kabisa ka kidato cha tatu huko St.Monika-Njombe. Au kama kawaida yako kudharau huhitaji hata kununua kakitabu ka-shilingi 2000 tu ukafaidika kimaisha? Kwani viroba bei gani? Castle lager nayo bei gani?, sigara je?  Au unadhani huyu mtoto ameandika UPUMBAVU.

Kama hiyo haitoshi, hata vitabu vyangu mwenyewe je umewahi viona? Au ukisikia matangazo ya vitabu vyangu unanibeza, hutamani hata kuviona unadhani nimeandika UPUMBAVU?.

Umewahi kusoma kitabu change kipi kati ya hivi, MACHO UANGU YANANIDANGANYA, DAMU YANGU IMEMWAGWA NA MAMA`NGU, KARAHA TUPU!, MORE THAN A FRIEND, OLE WAKO MIMI NIFUKUZWE SHULE NITAKUFA NA MTU, WHO CARE?, GAUNI LA MTUMBA, HAPA TUMECHEZA FYONGO?

 Umewahi kukisoma chochote kati ya hivyo vyote? Jitetee sasa! Na je unampango gani wa kunispoti ili nitoe simulizi inayofata iitwayo KUMBE JIRANI YANGU MCHAWI? Huna mpango wowote ndugu yangu! Kwahiyo unadhani mimi miaka yote hii tangu mwaka 2005 nikiwa darasa la saba nimeanza kuandika, wewe unadhani mimi naandika UPUMBAVU? Acha dharau zako! Siandikii dhiki, ni kile nilichojaliwa na Muumba, kimejibanza moyoni, katu siwezi mimi nikaacha kuandika tena kuandika kwa ufasaha kutokana na changamoto za maisha zinazotupiga danadana. Ila sasa fani hii imekuwa ni fedhuri na baladhuri, wewe unayesoma makala hii huitamani.

Hafu wacha nisisahu, umewahi hata kusoma makala zangu magazetini? Yani hukomi tu kutudharau sisi waandishi?

Wengine wakiona nimevaa suti wanajua nimeuza vitabu vingi nimenunua suti! Ebo!

Wakiona nakula mnofu wanajua nimeshauza kitabu cha KARAHA TUPU nimepata bukumbili ndo najivinjari. Ebo!

Wengine ni wivu tu, kitabu anatamani lakini akinunu anadhani mimi nitajenga mjengo kisa buku jero yake ya kitabu cha OLE WAKO MIMI NIFUKUZWE SHULE, kwahiyo hanunui ili kunikomoa. Kazi bure!

Wapendwa, mwaka huu unaelekea ukingoni, sawa tu. Mwenyezi atujalie shufaa, mwaka ujao ikibidi kuanzia sasa baada ya kuisoma makala hii, jenga tabia ya kusoma kazi za wenzako, sisi hakika HATUANDIKI UPUMBAVU. Usituonee wivu kwamba ukituungisha kitabu kimoja tutatoka kimaisha, vipi usiponunua na ukashuhudia tumetoka! Si utatamani ufe kwa wivu. Tuungeni mkono jamani, ili kuandika kwetu tusiwe kama tunapiga kwenzi kinyago tunaumiza vidole vyetu,

Huenda umemsikia LAZARO SAMWELI wa chuo kikuu SAUT MWANZA anatangaza kitabu chake kiitwacho NGUZO TATU ZA MAISHA, Ivi wewe unadhani huyu jamaa atakuwa ameandika UPUMMBAVU? Unazifahamu wewe hizo nguzo tatu za maisha? Huzijui ndio maana kila siku unalia maisha magumu, hela haipatikani, mara unamlaumu Magufuli. Si uache dharau uagize kitabu hicho cha NGUZO TATU ZA MAISHA kama nilivoagiza mimi! Alaaaa!

Halafu na huyu rafiki yangu BULIBA MAGAMBO, wa chuo kikuu cha DAR ES SALAAM ameanza kutangaza kitabu chake kiitwacho HITIMU NA “A”-ZIJUE MBINU ZA KUWA BORA NA WA KWANZA DARASANI. Chaajabu wewe ni mwanafunzi na kila siku masomo yanakukamata unatamani umalize tu kusoma au uache  na pengine darasani ndo hivo tena hali yako mbaya, halafu unavoona kitabu kimeandikwa “HITIMU NA “A”-ZIJUE MBINU ZA KUWA BORA NA WA KWANZA DARASANI.” Unapuuzia unanunua kilichoandikwa CHEMISTRY BOOK FOUR, unaakili wewe? Si uchukue kwanza kinachokuelekeza mbinu za kusoma! Hata ujaze vitabu mabegi yako yote uliyonayo shuleni halafu hujui namna ya kuvisoma ni kazi bure, ndugu yangu. Sidhani kama bado hujanielewa!

Ila naongezea, ukome kutudharau sisi waandishi, maana sisi HATUANDIKI UPUMBAVU. Tunakaa chini tunatulia tukuase kitu fulani, wewe unatudharau. Ebo! Vitabu vyenyewe sh.ngapi hivi, buku jero inakuuma hadi unaacha kununu unaona bora ununu Safari lager ulewe upepesuke ujishushie heshima, nunua kitabu wewe acha viroba!





AHSANTENI SANA WAPENDWA…….!

No comments:

Post a Comment

NITAKUPENDA DAIMA

Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU) Simu: 0769313224 ____________ Laazizi wangu wa moyo, nat...