MAKALA ZA KANTONI ZILIZOTOLEWA KATIKA GAZETI LA MWENGE KWA MATOLEO TOFAUTI TOFAUTI.
KALIA KIGODA MWANAKWETU, BURUDIKA NA TUNGO MWANANA TOKA KWA MWANDISHI WAKO WA SIKU NYINGI
ELIAS MWALONGO
(KANTON)
“WATOTO
WA SIKU HIZI, HOVYO KABISA!!”
Kuna kauli nyingi
zinazoweza kusikika mitaani zinazowashutumu vijana wa karne hii.Kuna kauli kama
za “watoto wa siku hizi hawasikii” au
“watoto wa .com hovyo kabisa”. Hiyo kauli ya `.com` ni ya kisasa kidogo
ukiilinganisha na hiyo nyingine ya `watoto wa siku hizi`.
Nakumbuka kauli hiyo
nilikuwa naisikia tangu nikiwa mdogo(mtoto) kwenye miaka ya 90,91.Nilikuwa
nawasikia watu wazima wa nyakati hizo wakilalamika kuhusiana na watoto wa
nyakati hizo(sisi) yaani tulikuwa hatusikii.Malalamiko hayo yalikuwa yanakwenda
hata kwa vijana wa wakati huo.Walikuwa wakilalamikiwa na kuwa tabia zilizokuwa
zinahesabiwa kuwa mbaya siku hizo.Nakumbuka moja kati ya tabia hizo iliyokuwa
inalalamikiwa kwa upande wa wasichana wa nyakati hizo ilikuwa ni uvaaji wa
suruali.Watu wengi wa sasa wanaweza kushangaa kama uvaaji wa suruali ni
tatizo.Lakini ndivyo ilivyokuwa japo kwa sasa tunachukulia ni vazi la kawaida
kwa wasichana,hatushangai.
Binti
aliyekuwa anavaa suruali alionekana kama Malaya sana siku hizo na alionekana
kama aliyeshindikana, siku hizi ni kawaida,Lakini tatizo la watoto na vijana
kulalamikiwa limekuwa likiongezeka na kuwa kubwa zaidi kila kukicha na kweli
tabia za ajabu za watoto na vijana zimekuwa zikistaajabisha sana.
Siku hizi si ajabu
ukasikia kesi za vitoto vya miaka 6-10 vikicheza kamali,vikiiba,vikijihusisha
na madawa ya kulevya pia hata kujihusisha katika mapenzi.Vitoto vya kiume
unaweza kukuta vikivaa “kata K,modo” na mavazi mengine
yasiyo ya heshima.Wasichana nao wana yao mengi tu.Vibinti vidogo tu unaweza
kuvikuta vinavaa vimini mitaani bila aibu,vingine vinajiuza na mbaya zaidi
havitaki kusoma shule.Na matukio mengine mengi ambayo kila mmoja anaweza
kuyashuhudia katika jamii yake.
Unaweza
kujiuliza, hawa watoto na vijana wanazitoa wapi hizi tabia za ovyoovyo! Wengine
wanasema “utandawazi” Wengine wanasema eti ni “nyakati za mwisho” ilimradi kila
mtu amesema lake.Lakini je ni kipi chanzo cha tabia hizi mbaya?Je watoto
wenyewe wanajitafutia?Je kuna mahali wanajifunza? Watoto hawa wameonekana
kanakwamba wao wenyewe wamekuwa wakijibadilisha toka uzuri kwenda ubaya.Jambo
ambalo wao hubebeshwa lawama kwa tabia hizo na kuonekana kero katika jamii
zao.Mimi sikubaliani na majibu hayo hata kidogo!
Kuna
nadharia moja inasema “kuku hawezi kutaga yai bovu,ila uatamiaji wake ndio
unaoamua kuwa yai liwe bovu au liwe bora.Kama kutakuwa na umakini katika
uatamiaji basi hakuna hata yai moja litakalokuwa bovu au kuharibika.Nikija
kwenye suala la tabia za watoto na vijana,hakuna tofauti.Hakuna ambaye hafahamu
kuwa watoto hawajileti,au kujiamulia kuzaliwa hapa duniani. Sio yeye
atakayeamua azaliwe au laa.Hiyo ni kadiri ya kanuni ya maumbile na haina
ubishi.Na mtoto akishazaliwa,binadamu wa kwanza kukutana naye ni wazazi wake
hasa mama.Lakini pia utafiti wa kibaolojia unaonyesha kuwa mtoto anapokuwa
tumboni mwa mama yake anaweza kujifunza tabia za mama yake hasa kwa kusikiliza
anavyoongea.Hivyo mama akiwa na matusi na mtoto hujifunza hivyohivyo.Mama akiwa
mlevi wakati wa ujauzito na mtoto kuja kuwa mlevi ni asilimia tisini.Pia baada
ya kuzaliwa, mtoto hukua mikononi mwa wazazi wake hasa mama, kwa kuwa wakati
mwingi anakuwa nae.Hivyo basi, kama wazazi watakuwa na tabia mbaya mbaya
hatutashangaa na watoto wao wakiwa hivyohivyo.Lakini sikuhizi katika familia
nyingi watoto hulelewa na mahousegirl.Je,
hii si hatari kwa malezi ya mtoto?Mtoto ataiga tabia za housegirl badala ya kuiga tabia za wazazi wake.Kama housegirl ni msagaji, Malaya,shoga,mwizi
n.k.Je, mtoto ataiga nini?Ndipo wataibuka watoto wenye tabia za ovyo ambazo
hata wazazi wanazishangaa.Wataendelea kuibua lawama nyingi kwa watoto na vijana
hawakumbuki kuwa “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”.Hivyo kwa mtazamo wangu naona
mtu wa kwanza kulaumiwa kwa tabia mbaya za watoto na vijana na mmomonyoko wa maadili
kiujumla Mzazi/mlezi ndio awe wa kwanza kunyoshewa kidole.Kwani katika malezi
ya mtoto kuna walimu watatu,wa kwanza ni mzazi,wa pili ni mwalimu wake
shuleni,na watatu ni ulimwengu ambao utamfundisha yule aliyekosa malezi ya
walimu wawili waliotangulia.Kwahiyo kauli za “vijana wa sikuhizi hovyo
kabisa”zisiwalenge vijana au watoto moja kwa moja,bali tuangalie hawa vijana
wanalelewaje katika jamii zao!!
Na; Elias K. Mwalongo(KANTON)
Ruaha Catholic University(RUCU)
+255769313224
“KANISA
KATOLIKI LIMETUKANWA SANA”
Ndugu msomaji,
usije ukanikuda roba, haya wala si maneno yangu.Ni nukuu ya maneno ya mwanzo
kabisa ya hotuba ya Askofu Evaristo Chengula wa Jimbo Katoliki la
Mbeya,Tanzania aliyoongea wakati akitoa ufafanuzi wa tamko la jukwaa la
wakristo kuhusu suala la kuchoka kutukanwa kuchokozwa na kuonewa kwa Kanisa
Katoliki.Askofu Chengula alisema sio dhana ya kulipiza kisasi bali ni kuwa watu
wa sala, kitubio na ikiwezekana kukaa na kuzungumza na wanaofanya chuki na
Kanisa katoliki na kufanya uharibifu wa mali za watu na serikali.
Askofu Chengula alitoa ufafanuzi huo katika semina ya
Makatekista na walimu wa dini iliyofanyika katika ukumbi wa vijana Jijini Mbeya
tarehe 2-2-2013, ambao walitaka kujua ukimya huo utadumu mpaka lini hali
wanachokozwa,wanatishiwa maisha na na vitu kuharibiwa.Alisema kuwa licha ya
kanisa kutukanwa,kuchokozwa na kuharibiwa mali na hata kufikia hatua ya
kuwapiga risasi baadhi ya viongozi wa kanisa,Kanisa katoliki halitajibu zaidi
ya kuendelea kusali Rozari Takatifu, kufanya kitubio na kuendelea kufunga ili
kushinda majaribu yasiyompendeza Mwenyezi Mungu.
“Kanisa Katoliki limetukanwa
sana,limefanyiwa uchokozi na uharibifu mkubwa na sasa wameanza kutupiga na
bunduki,huku vikitolewa vitisho vya kuuawa mapadre na maaskofu waziwazi.Lakini
tunaposema Kanisa limechoka kutukanwa msibebe bunduki, bali muwe watu wa sala
na kuwaombea wanaofanya hayo ili watubu na wamrudie Mwenyezi Mungu”.Aliongeza
“Muwe watu wa sala,mapatano na wakakamavu.tusali Rozari katika nyumba zetu
tufanye kitubio na tuwe watu wa kufunga na kumshinda shetani, hiyo ndiyo silaha
pekee na ikibidi kutokana na kuchoka huku tuwe tayari kuzungumza na hao
wanaotuchokoza.”
Aidha, alitoa ushauri kwa serikali
na mamlaka husika kutoruhusu kujenga nyumba za starehe karibu na shule au vyuo
kwani ndio chanzo kikubwa cha ongezeko la vitendo vya kikatili vya utoaji mimba
n watoto wanaookotwa katika madampo ya taka katika vyuo na mashule.Alisema
haiwezekani shule na starehe.Hivyo kujenga majumba ya starehe ni kumjengea
mwanafunzi mazingira magumu ya ushawishi na ndio matokeo ya kushindwa kuendelea
na masomo vizuri.
Hata hivyo aliwaagiza mapadre,
watawa wa kike na wakiume, makatekista na walimu wa dini kuongeza jitihada za
dhati kutembelea mara kwa mara wanafunzi na wanachuo kuwapatia ushauri licha ya
kuendelea kutoa mafundisho ya dini ili waweze kufuata maadili mema.Katika
semina hiyo mambo mbalimbali yalizungumzwa kuhusu muhtasari wa mafundisho ya
dini kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu,ambapo Katibu mtendaji wa idara ya
katekesi kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania,Pd. Raphael Madinda alitoa mada
kuhusu umhimu wa wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi kuridhia kuingizwa katika
mtaala wa Elimu nchini. Pd. Madinda alisema mmomonyoko wa maadili na kuibuka
kwa vurugu, migomo na migogoro mbalimbali hata kusababisha maandamano
mashuleni,chanzo kikubwa ni ukosefu wa mafundisho ya dini ambayo humjenga
mwanafunzi kumuogopa Mungu na kuishi kwa kufuata,sheria za nchi, maadili na utu
wema.
Alitoa wito kwa waamini wa kanisa Katoliki
kujitokeza kwa wingi kutoa mafundisho ya dini kwa wanafunzi kuanzia ngazi za
awali, msingi, sekondari, vyuo na vyuo
vikuu ili jamii iweze kurejea katika
maisha ya upendo, amani, utulivu, upatanisho, haki na kuvumiliana,mambo ambayo
yanaendelea kuporomoka kwa kasi ya ajabu nchini Tanzania.
Katika semina hiyo,Pd. Innocent
Sanga amesema changamoto kubwa wanayokabiliana ni ukata katika kuwawezesha
walimu na makatekista kufundisha katika shule mbalimbali kwani jiografia ya
maeneo ya mkoa wa Mbeya ni milima na mabonde na shule hujengwa umbali mrefu
unaohitaji vyombo vya usafiri na fedha za kujikimu jambo ambalo wanaendelea
kulitafutia ufumbuzi wakati wakiendelea kujitoa.
Hata hivyo Askofu Chengula wakati akigawa
vitabu vya muhtasari wa mafundisho ya dini mashuleni amewapongeza mapadri kwa
kuendelea kutoa mafundisho ya dini kwani hilo ndilo jukumu kubwa la kanisa
kufundisha katekismu, Neno la Mungu maisha ya kisakramenti na huduma nyingine
za kiroho ya kimwili.
Na; Elias K. Mwalongo(KANTON)
Ruaha Catholic University(RUCU)
+255769313224
KEKI
ISIYOOZA
Huenda mimi na
wewe tumekuwa tukijitahidi mara kwa mara kutengeneza keki bora lakini
hazidumu.Tunatengeneza kwa ufasaha tukidhani zitadumu lakini zinaoza
ovyoovyo.Fuatilia sasa hatua hizi za kutengeneza KEKI ISIYOOZA;
Chukua
kiasi kikubwa cha uchangamfu.Angalia kwanza kwa makini kisiwe kikubwa
sana.Changanya na bakuli moja la upendo katika chombo kiitwacho Biblia.Ongeza
walau vikombe vikubwa viwili vya ukarimu.Weka kijiko kimoja kikubwa
cha tabasamu.Koroga
mchanganyo wako kwa makini,koroga kwa nguvu kwa dakika kumi ili viungo hivyo
vijichanganye vizuri.Kisha ongeza kikombe kidogo cha nia,koroga vyote pamoja
kwa dakika mbili.Kisha chukua chujio ya uwazi,chuja mchanganyo wako ili
kuondoa takataka za ubinafsi,choyo,wivu,dharau,umbea,uvivu,chuki,kiburi,unafiki na
takataka nyingine ambazo huenda ziliingia kwa bahati mbaya wakati unaandaa
viungo.Ukiisha chuja takataka hizo kung`utia mbali huko na uzisahau
zisijechafua keki yako baadae.Kisha acha mchanganyo wako kwa dakika kumi au
zaidi ili utulie kabisa.Kisha oka keki yako kwenye jiko la heshima,ili iive
taratiiiibu kwa joto la sala.Baada ya nusu saa fungua jiko
lako,chukua kitambaa cha imani na utumie kuipua keki
yako.Ikiwa bado ya moto kabla haijapozwa na baridi ya unafiki,iweke kwenye
chombo chenye matundumatundu ili harufu nzuuuri ya upendo iweze kupenya na
kuenea katika chumba.
Kiweke chombo
hicho sehemu ya uwazi ili harufu nzuri ya keki iweze kuenea kwa watu wengi
zaidi nao wafurahi kwa tabasamu la umoja.
Japo najua watu
watakunyoshea kidole,watakusodoa na kukuvunja moyo utakapokuwa unafurukuta
kutafuta viungo vya keki yako,wala usife moyo.Wengine
watakusimanga,watakubinulia midomo,wengine watatamani kukutemea mate,usijali!
walimwengu ndivyo walivyo.Yatakapokukuta haya nakusihi ufunge mshipi ujizatiti
upige hatua maadamu umedhamiria na unajua unachofanya.Keki yako ikisha iva
ndo kabisa watajaa kijicho,watakukunjia
ndita bila kosa,rafiki zako watageuka adui zako ila huenda usigundue maana
wakijaa unafiki wanakuwa sivyo walivyo.Usoni watatabasamu huku mioyo
ikiwa imekunja ngumi tayari kukuvizia na kukubonda uzime kama kibatali.
Ukishafanikiwa
watajaa jeuri,wengine hawatapenda hata kukusikia ukiwaambia
“shikamoo,mambo,vipi,poa,shwari,niaje” hata mengine yenye maana sawa na haya.
Siku
zote ukifanikiwa si wote watakupigia makofi kwa lengo la kukupongeza.Wengi
watakaokununia ni wale wa karibu yako.Nakusihi ukazane kutengeneza keki
isiyooza maana inampendeza hata yeye aliyekuumba.Maneno na masimango ya watu
yasivurugie mipango yako na kukurudisha nyuma kirahisi.Masimango na wivu wao
vikusaidie kupiga hatua mbele zaidi ili uwaache watembee vichwa chini kwa
soni.Maana maisha ni mchezo wa Sandakalawe mwenye kupata anapata.Talanta zetu
ni tofauti,ukikosa moja haimaanishi huna zote,uliyopewa wewe jivunie maana
mwenzako amekosa.Itumie talanta hiyo kwa makini na uaminifu ili ilete manufaa
kwa wote.
Na; Elias K. Mwalongo(KANTON)
Ruaha Catholic University(RUCU)
+255769313224
SOTE TUNASAFIRI
Mpendwa
msomaji, yamkini mimi na wewe ni mashuhuda wa majanga yanayotukumba hasa katika
dunia ya leo. Leo dunia inatutunishia misuli,inatutishia na kutugaragaza
ovyoovyo.Tunazika ndugu zetu tele wanaotutangulia mbele ya haki kutokana na
vita,maangamizi,njaa,magonjwa na wengine wanajipiga kitanzi kutokana na kukata
tamaa ya kuendelea kuishi.Leo vyombo vyetu vya habari vinatujuza idadi ya maiti
mahututi,mateka,wakimbizi,wala rushwa,biashara feki,divisheni ziro,madawa ya
kulevya,ufisadi,migomo,ongezeko la wajane na yatima na matimbwili kadha wa
kadha yanayotupiga danadana na kutufanya tutoe machozi kila uchwao.Haki, amani
na usawa walizotuachia waasisi wetu vimegeuka karaha tupu.Hata hivyo tushukuru
Mungu mimi na wewe bado tunavuta pumzi kwenye dunia hii ambayo wengi wetu
wameikatia tama.Lililopo mbele yetu sasa ni kufunga mshipi, kunusuru roho zetu
na za wenzetu ili maisha yaendelee.
Mara nyingi ugumu wa maisha
tunaoulalamikia ni wa kujitakia wenyewe.Sikuhizi watu wengi tunafikiria maisha
ni leo tu,tunasahau kuwa kesho nayo siku.Na ili kuiandaa hiyo kesho tukisema
tuanze kuwakalisha kwenye semina babu zetu na bibi zetu, tutakuwa tunapiga
kwenzi kinyago.
Hivyo basi ni
jambo la busara tuanze kuwaandaa vizuri vijana na watoto,tukiwajenga vema
katika misingi ya malezi bora kiutu,kielimu na kinidhamu.Mazingira pekee ambayo
hili linaweza kufanyika ni katika mashule.Harakati hizo za kujinusuru na ugumu
wa maisha zianzie shule ya msingi,sekondari mpaka vyuo vikuu.Vijana wafundishwe
mambo ambayo yatawafanya wawe na mchango katika jamii zao na nchi kiujumla na
sio kukumbatia bahasha nyingi zilizojaa vyeti ambavyo haviwasaidii zaidi ya
kuwapa maujiko tu.Katika makongamano mbalimbali ndio nafasi muafaka wa kujenga
kizazi kipya kitakachopiga teke rushwa na ufisadi.
Kunaongezeko kubwa la
vijana mitaani wanaolalamika kuwa hawajapata ajira serikalini.Lakini wengi wao
ukiwaona ni kweli wanastahili kutoajiliwa.Na kwa namna hiyo basi kelele za
kulilia ajira hazitakoma na ugumu wa maisha utaendelea kushika kasi.Nakusihi
kijana wa leo utegemee sana kipaji chako na ujasiliamali, kuliko kuililia
serikali kama vile inakuangalia wewe tu.Tunamifano dhahiri ya watu walio kuwa
na maisha duni katika jamii zetu lakini leo maisha yamewanyokea hata tunawaona
si wenzetu tena.Je,hawa wametokeje kama sio kujituma tuu!Kwakuwa inawezekana
kabisa kijana mwenye nguvu na akili timamu kujitegemea,basi nawasihi vijana
fungeni mikanda,maisha lazima yaendelee!!Mida ya kuomba imekwisha na tabia ya
kuombaomba au kudokoa vya watu ife.Kwa kuwa unayemwomba na yeye anashida zake
ndio maana anapigania kupata na unayemdokolea hujui amepataje,ukikamatwa
utabondwa mawe au utachomwa moto uwe majivu kijingakijinga tu.Ili haya
yasiendelee kutukumba vijana wa leo,basi vijana,KUFA NA KUPONA, MAISHA LAZIMA
YAENDELEE!!
Na; Elias K. Mwalongo(KANTON)
Ruaha Catholic University(RUCU)
+255769313224
IMANI ZA WAZAZI JUU YAWATOTO
WAO.
“…..nusu ya kwanza ya misha yetu
huharibiwa na wazazi na nusu inayobaki huharibiwa na watoto wetu”. Ni
kauli iliyosemwa na mshauri wa masuala
ya ndoa na malezi Bi. Jenifa James kauli hii ni ngumu ikiwa hukuwahi kufikiria
juu ya malezi ya watoto .
wazazi na walezi popote duniani
wanatambua hakuna jukumu zito kama la kulea watoto.Ni kazi ngumu ambayo haina
likizo.Ndiyo si ajabu kuona watoto wengi wakitelekezwa lakini haya yote haya
wazuii wazazi makini kulea watoto kuwapatia watoto wao huduma ya elimu,
afya,mavazi, malezi na mengineyo mrngi ikiwa ni pamoja na usalama wa maisha
yao.
Kumekuwa na imani kadha wa kadha za
wazazi katika tamaduni mbalimbali juu ya watoto wao.Wazazi au walezi wanapolea
watoto wao hupitia vipindi tofauti ambavyo hubadili mitazamo yao.
I.Watoto
huimarisha ndoa.
Wanandoa wachanga hutamani sana kupata watoto wakiamini kuwa ndoa
itakuwa imara zaidi.Naamu ndivyo ilivyo,watoto huwa kiungo kizuri cha ndoa
kinachokazia muungano wa wazazi kwani kila mmoja hujiona anamchango kwa
mwenzake.
LAKINI,Wazazi
wanapaswa wawe na busara,maana katika
ndoa nyingi watoto wamegeuka mtihani na kutishia kuvunjika kwa
mahusiano(ndoa)
II.Wazazi
wa leo si bora kama wa jana.
Japo si wote
lakini sehemu kubwa ya malezi ya watoto imekuwa inaleta utata na kusuasua kana
kwamba wazazi wamejiondoa katika jukumu hilo.Katika hali hiyo jamii pia
imechangia sana, maana inataka wazazi walee watoto wao katika democrasia,kujali
kila hisia ya mtoto,kuwaacha watoto waamue wapendavyo,kinyume cha hapo mkono wa
sheria utaingilia kati.Hali hii hupelekea watoto kuyumba kimaadili wakijiona
wako sahihi kwakuwa wako huru.
III.Ndoa
isiyyo na watoto haina furaha.
Wanandoa wengi
hawana watoto,wanaishi kwa amani uvumilivu na kupendana.Furaha inaweza
kupatikana kutokana na maamuzi ya kuamua kufunga kizazi,kuchelewa kupata watoto
n.k.
LAKINI;Ukweli
unasimama tena,wanandoa wasio na watoto hawana furaha ya kweli.
IV.Mtoto
mmoja hatoshi.
Watafiti Olson
naDefrain wanasema;”…mtoto mmoja hana gharama katka kumtunza na habani sana
uhuru wa wazazi kuishi wapendavyo na ni rahisi kuishi kwa starehe”
LAKINI;Ikumbukwe
kuwa ni rahisi mtoto mmoja kudeka,kunyimwa uhuru wa kucheza na wenzake kwa hofu
ya kudhuriwa,na ndio maana wazazi wengi wa Afrika wa zamani na wale
wasiobadirika kirahisi walihimiza uzo wa watoto wengi ili kuepuka presha za
kupanda na kushuka.
V.Malezi
huwa rahisi kadiri mtoto akuavyo.
Hii ni imani
iliyoenea lakini inapotosha ukweli halisi.Kadiri watoto wakuavyo ndio malezi
huwa magumu zaidi.Tukiacha kipindi cha balehe,kipindi cha kuelekeza watoto
wakuaji,wanaokutana na maarifa ya kila uchao katika ulimwengu wa dijitale ni
jukumu kubwa zaidi.
VI.Malezi
huishia watoto wanapoanza kujitegemea na kuondoka nyumbani.
Hii nayo ni
imani inayopotosha uhalisia.Wazazi wenye watoto wakubwa ni shahidi wa jambo
hili.Hupumzika warudipo enzi za ujana wao kabla ya watoto.LAKINI;
Maranyingi
wazazi hao hujikuta wakiishi na watoto,wanapopewa talaka,wanapokosa
ajira,wanapofukuzwa kazini,nyakati za migogoro na nyakati za kuachiwa jukumu
jipya la kulea watoto wa watoto wao yaani wajukuu wao.
Hitimisho.
Ni vema wazazi
wa jana,leo na kesho wakumbuke kuwa kazi ya malezi inashukurani kidogo,ni
jukumu la uhai wote na halina malipo.Hivyo wazazi wakumbuke kuwa “mbwa
hajifunzi kuwinda uzeeni” na “samaki mkunje angali mbichi” jinsi watakavyo
wanyoosha watoto wao wangali wadogo ndivyo watakavyofarijika zaidi baadae na
kuyaona matunda mema ya watoto wao.
WATOTO NI ZAWADI
KWENU, SIMAMENI IMARA KATIKA MALEZI ILI BAADAE WAWE FARAJA KWENU!
Na; Elias K. Mwalongo(KANTON)
Ruaha Catholic University(RUCU)
+255769313224






No comments:
Post a Comment