KUMBE JIRANI YANGU
MCHAWI
MTUNZI: ELIAS K. MWALONGO(KANTON)
RUAHA CATHOLIC UNIVERSITY(RUCU)
+255769313224
KALIA KIGODA MWANAKWETU, UHONDO NDIO HUU WENZAKO WANANUFAIKA, UKISUSA KALAGABAHO, SISI TWAFURAHIA SIMULIZI HIZ NAMNA HII NA MWANDISHI WETU MARIDADI, "KANTON"
SURA YA KWANZA
Tangu siku ile sijawahi kabisa kupata lepe la usingizi. Nimekuwa mtu wa shuruba na kujiinamia chini nisijue nini nifanye.Nikijaribu kulala chali nitazame juu ambako naamini ndiko aliko mwenyezi sipati nafuu, nikilala kiubavu nitazame pembeni huko nayo nagundua kuwa haisaidii, nikijaribu kulala kifudifudi nifumbe na macho nisikumbuke yote yaliyonisibu maishani na kunifikisha hapa kifungoni, bado nagundua kuwa ni kazi bure. Nikiamua kuamka na kujiketisha chini niegame ukutani huku nikijiinamia. Nafurukuta nawayawaya natamani kama nijifinye au nijipige teke. Mapigo ya moyo yanaenda kwa kasi yanapiga kama saa ya ukutani pwi-pwi-pwi. Makamasi yananifura kama mbeta ya ulanzi wa masika. Machozi yananitiririka mashavuni mwangu hadi chini yanatua huku yakilowanisha shati langu. Moyo umekufa ganzi hata nahisi kama vile unataka kumrudia aliyeuumba na mwili wangu huu kushuka mavumbini ulikotoka.
Nahangaika masikini Elias mimi kupoteza mawazo juu ya mazishi ya mwanangu Sabrina, binti yangu mdogo, wa pili kuzaliwa. Binti yangu mashuhuri aliyenifanya nijivune hapa kijijini na kuonekana wa maana. Mazishi ya binti yangu yananirudisha mbali nilikotoka na mikasa ya maisha iliyonikumba. Masikini mimi ninakumbuka kifo cha Salma dada yake Sabrina, narudi nyuma tena namkumbuka marehemu mwanangu Sostenes mdogo wao wa mwisho niliyempoteza angali mdogo kabisa. Tena ninakumbuka sana siku ile nilipotupa udongo kwenye kaburi la mke wangu kipenzi Salome, binti wa kipangwa niliyempata kwa shida nikalipa na mahali ya mafahali mawili kisha nikamuweka ndani awe mama wa wanangu, naye nilimpoteza angali kijana kabisa akaongozana na binti yake mkubwa Salma wakaniacha nafurukuta nalia na moyo wangu. Najaribu kufurukuta nisikumbuke ndo kwanza picha ya matukio hayo inanijia vizuri kabisa. Uvumilivu unanikabili na kunishinda nguvu, wacha nichukue kalamu yangu niwaandikie walau mjifunze kitu ili siku yatakapowakuta na nyinyi msihukumiwe kifungo cha maisha na kusota kifungoni huku kama mimi.
Ninakumbuka vishindo vya siku ile nikiwa kitandani usiku wa manane nimepumzika na mke wangu mpendwa. Vishindo vilivyosikika kuanzia kwenye dirisha la chumba changu vikazunguka nyumba yangu hadi upande wa pili kwenye chumba cha wanangu. Kwa hofu nikamwamsha mke wangu aliyekuwa amelala fofofo asikilize na yeye vishindo hivyo. Jinsi nilivyomwamusha ndivyo vishindo vilivyozidi kusikika kwa nguvu vikisogea tena jirani na dirisha la chumba chetu. Mwili ulitetemeka, kijasho chembamba kikanimiminika, na nywele zikanisimama. Mimi na na Mama Salma tukapiga moyo konde, yote tukamwachia mwenyezi maana yeye ndiye mpaji na mnyimaji. Vishindo vikaishia dirishani kwetu vilikoanzia na ghafla vikatoweka, kukawa kimya kabisa. Nilijaribu kufikiria ni nini kilikuwa kinatokea lakini sikupata jibu. Tulibaki tumedhoofika kwa hofu na mashaka. Tulijaribu kulala lakini haikuwezekana kwani hatukupata usingizi kabisa. Nilijaribu kuwasha tochi ya simu yangu, nikamulika kuanzia kwenye mlango wa chumba chetu sikuona kitu chochote, nikamulika kwa kona ya chumba chetu nikamwona mende mmoja tu akipotelea kwa sanduku la nguo la Mama Salma, nilimulika chumba kizima sikuona cha pekee, basi nikaizima tochi yangu. Baadae tulianza kunong`ona kwa sauti ya chini sauti iliyokuwa imejaa hofu na mashaka makubwa. Baadaye tulikaa kimya kwa kitambo kirefu. Macho yangu yalianza kuwa mazito, usingizizi ukaanza kuninyemelea kwa mbali. Ghafla nikaamshwa na jogoo wa Ndeluvale aliyewika kwa sauti kubwa. Ndeluvale yule jirani yangu mhunzi na fundi wa kutengeneza mikeka, na vikapu. Alikuwa na kuku wengi sana na walikuwa wakilala juu ya mti uliokuwa unapakana kati ya nyumba yangu na yake. Yule jogoo alipowika nikashtuka toka usingizini. Nikachukua simu yanu ya Tecno, nikaiwasha ili nitazame muda. Ilikuwa sa kumi na moja na dakika ishirini na tatu alfajiri. Kule kusinzia kulinisahaulisha vituko vilivyotokea usiku wa manane, sasa nikawa macho na taratibu kumbukumbu zikaanza kunirudia, nikakumbuka vizuri mimi na Mama Salma tulivyohangaika usiku kwa hofu na mioyo kutupwitapwita. Nikageuka kumtazama Mama Salma aliyekuwa amelala pembeni yangu, giza lilinizuia sikuweza kumtazama vizuri, nikataka niwashe tochi ya simu yangu ila nikaamua kuacha kwani kwa mbali nilikuwa namsikia akikoroma. Niliendelea kutafakari huku nimejiegesha kitandani nisione dalili ya kupata usingizi tena. Baada ya dakika chache nilianza kuhisi mwanga ukiongezeka mle chumbani tokea dirishani, kumbe kulikuwa kunaelekea kupambazuka. Haikupita kitambo kikubwa Mama Salma naye akavuta pumzi ndefu kisha akageuka alale vizuri basi nikamwamsha kwani muda nao ulikuwa umetokomea. Akanitazama kwa mbali kwa kutumia mwanga ule ulioanza kupenyeza dirishani alfajiri ile. Baada ya muda nikaanza kumkumbusha kuhusu tukio la usiku lililotuogofya. Tulijaribu kuulizana ni nini kilichotutisha usiku lakini hakuna aliyeweza kugundua. Basi tukaamua kupotezea.
Niliamka nikatoka chumbani kwangu nikaanza kutoka taratibu kuelekea sebuleni. Kabla sijafika mlango wa kutokea nje nikashitushwa na kelele za mlango uliobamizwa chumbani kwa wanangu. Nikageuka haraka, masalale! Kumbe alikuwa ni Salma binti yangu wa kwanza. Nikamwuliza kulikoni mwanangu? Akajibu, baba Sostenesi anaumwa. Nikarudi haraka chumbani kumwita Mama Salma, ili aende akaangalie watoto. Akakurupuka haraka alijifunga kanga kiunoni, akavaa ndala zake na kukimbia hadi chumbani kwa Salma na wadogo zake. Alipofika alimkuta Sostenes akiwa amejilaza kitandani kwake, kitanda kilichokuwa pembeni mwa kitanda walichokuwa wanalalia dada zake Salma na Sabrina. Akamwuliza anaumwa nini, yeye katika umri wake mdogo hakuweza kueleza akasema tu kuwa hajisikii vizuri na mwili mzima ulikuwa unauma. Walijitahidi kumshawishi asimame lakini hakuweza kuhimili peke yake alihitaji kushikiliwa. Alikuwa amenyong`onyea hawezi kusimama peke yake. Basi tukahangaika masikini sisi tukampeleka dispensari yetu ya kata kwa pikipiki. Tulipofika tulipokelewa vizuri na manesi wawili. Tukawakabidhi mgonjwa wetu nasi tukaketi kwenye veranda kwanye benchi tukisubiri kuambimbwa mwanetu alikuwa anaumwa nini hasa.
Kule nyumbani Salma na Sabrina walikuwa wameenda shuleni. Tukaendelea kunong`ona pale nje mimi na mke wangu Salome. Mara mlango ulifunguliwa na nesi mmoja akatoka akatuambia kuwa mgonjwa wetu alikuwa anazidiwa na vipimo walivyokuwa navyo haviwezi kusaidia kujua tatizo la mgonjwa wetu, hivyo walitushauri tumpeleke hospitari ya wilaya ili tukasaidiwe huko. Maskini sisi, kipatochetu chenyewe ni duni. Basi tukachukua akiba yetu ya pesa tukaanza safari kuelekea hospitari ya wilaya ya kipindi hicho ambayo sasa ni hospitari ya mkoa wa Njombe. Tukiwa kwenye gari kuelekea hospitarini mwanetu Sostenes alitukatisha matumaini. Nilimwangalia mwanangu, nikaona mwanangu macho yamemtoka pima, mdomo wake mdogo na mwembamba ulikuwa umelegea na uko wazi, mapigo ya moyo yalipiga taratibu kama saa ya ukutani ambayo betri imeisha nguvu yake. Macho ya mwanangu yalinitazama mimi bila kukonyeza mithiri ya mtu anayetaka kumaanisha kitu. Nikahisi kama vile mwanangu anataka kumaanisha `kwaheri`. Nilitamani hata nijipige teke nikome kufikilia kuwa mwanangu ananiaga lakini ndivyo ilivyokuwa. Niliendelea kumkodolea macho mwanangu kama yeye alivyonikodolea bila kukonyeza, lakini tulivyoendelea kutazamana vile mara nikaona macho yake yakazidi kusinyaa na kuwa madogo hadi yakafumba. Masalale! Moyo ulinidunda kwa nguvu na kwa woga. Nikamtikisa mwanangu alikuwa amelegea yuko hoi hana hali. Nikajaribu kusikiliza mwendo wa mapigo ya moyo kama ni ya haraka au taratibu, chaajabu niliishia kusikiliza mapigo ya moyo wangu mwenyewe. Kumbe sasa nilikuwa sijampakata mwanangu bali maiti ya mwanangu. Machozi yalianza kunitiririka mashavuni. Mama Salma sasa ilikuwa ni kilio na yowe. Tulihuzunika sisi tukalia na kuomboleza juu ya mwanetu aliyetutoka hali hatujui alikuwa anasumbuliwa na tatizo gani. Basi tuligeza gari na kuanza kurudi nyumbani. Sasa safari yetu ilikuwa ni ya kusafirisha maiti kupeleka nyumbani badala ya kusafirisha mgonjwa kwenda hospitari.
Tulifika kijijini kwetu mida ya jioni sana, tukakuta maandalizi ya msiba yanaendelea kufanyika kwani tuliwataarifu ndugu na jamaa kwamba mwanetu kipenzi ametutoka. Nasi tulipofika tulikuta ndugu wengine wakiwa wanalia kwa uchungu mkubwa, uchungu wenye masikitiko ya kumpoteza mwanetu kipenzi, mwanetu pekee wa kiume, mrithi wetu na tumaini la familia yetu. Msiba ulipokelewa maiti ikawekwa kwenye chumba maalumu nasi wafiwa tukaingia humo kuomboleza. Maandalizi yaliendelea, ndugu jamaa na majirani walifika kwenye msiba tukaomboleza pamoja. Moto ulikokwa nje uwanjani, watu walipika vyakula, michango mingi ilitolewa nao majirani kwa mioyo minyofu waliomboleza pamoja nasi usiku mzima hadi asubuhi. Siku hii ya pili ilikuwa ni siku ya mazishi ya mwanangu Sostenes. Ilikuwa ni siku ya mwisho ya kuona sura ya mwanangu. Ilinipasa nianze kusahau tabasamu lake, kicheko chake na upole wake uliojionyesha hata kwa mwonekano wa sura yake.
Maandalizi yalikamilika, mwanangu Sostenes akafungwa kama pipi kwenye sanda, akadumbukizwa kwenye jeneza dogo la saizi yake. Ilipofika saa nane mchana, jeneza likawekwa nje uwanjani, mwenyekiti wa msiba ule Mzee Ndeluvale ambaye alikuwa jirani yangu akatangaza kuwa maiti itaanza kuangwa tukianzia sisi wazazi wa marehemu, dada zake na ndugu wengine watafata hadi jamaa wote waishe. Agizo hilo lilifuatwa. Mimi nikawa wa kwanza kujongea mbele ya jeneza kuitazama sura ya mwanangu kwa mara ya mwisho. Nilisogea kwa ujasiri lakini ujasiri ukaniisha, chozi likanishuka. Nikachukua leso yangu mfukoni nikaanza kufuta machozi yaliyokuwa yakinititika mashavuni mwangu nikimlilia mwanangu. Mama yake ndo kabisa hakuweza kustahimili maumivu, aliishiwa nguvu asiweze hata kusimama peke yake alishikiliwa na ndugu wengine wakamkokota taratibu amtazame mwanae kwa mara ya mwisho. Sabrina. Dada yake mdogo wa marehemu Sostenes naye alilia kwa uchungu mkubwa, watu wakamshikilia upande kwa upande na kumsogeza jirani na jeneza la Sostenes mdogo wake. Huku akilia kwa kwikwi aliiangalia sura ya mdogo wake kwa mara ya mwisho kisha akapelekwa pembeni. Ndugu wengine wa marehemu nao wakapita kuuaga mwili wa ndugu yao Sostenes kisha majirani na wageni wote walifika kujumuika nasi wakapita kumwaga mwanangu kipenzi aliyekuwa amenitoka angali mtoto. Wakati zoezi hili likiendelea, Salma dada wa marehemu Sostenes aliyekuwa pembeni akadondoka ghafla na kupoteza fahamu. Watu wakambeba wakamweka kwenye kivuli wakampepea kwa muda mrefu lakini haikusaidia, akapelekwa hospitalini ambako alilazwa akahudumiwa vizuri na wauguzi.
Wakati ukafika wa kwenda makaburini kumzika mwanagu Sostenes. Sikuamini yaliyokuwa yakitokea siku ile. Niliona kama vile ni ndoto ninayoiota alasiri ile, lakini ulikuwa ndo ukweli wenyewe. Watu wakalibeba lile jeneza lililokuwa na mwili wa mwanangu huku wakipokezana baada ya kila kitambo kidogo. Hatimaye wakafika nalo makaburini, wakaliweka jeneza pembeni mwa kaburi lililokuwa limeshaandaliwa. Katekista aliongoza sala ya mazishi, kisha zoezi la kumzika mwanangu likafuata. Jeneza liliingizwa kaburini taratibu hadi likatua kwenye sakafu ya kaburi lile. Wakachota mchanga na kuniletea ili mimi niwe wa kwanza kutupa mchanga kaburini japo kiganja kimoja. Nikasisimuka mwili, taratibu nikachota ule mchanga nikaumimina taratibu kwenye kaburi la mwanangu Sostenes. Jinsi nilivyozidi kumimina ule mchanga ndivyo na machozi yalivyozidi kunitiririka na mengine kumiminika hadi ndani ya kaburi la mwanangu. Nilipomaliza nikaondoka taratibu ili kumpisha mke wangu naye amzike mwanaye. Haikuwa rahishi Mama salima kuchukua kiganja cha mchanga na kumimina kwenye kaburi la mwanae, basi wanawake Fulani walimshikilia na kumsaidia hadi akatupa mchanga ndani ya kaburi la mwanae. Akafuata Sabrina japo naye kwa kushikiliwa. Ndugu wengine wakafuata na baadaye wengine wakalishambulia kaburi la mwanangu kwa kutupia mchanga kwa kutumia spedi na kushindilia kwa visigino vyao. Mimi nikiwa nimesimama pembeni niliwaza moyoni mwangu, nikajaribu kukumbuka mwanangu, machozi yakaanza kutoka tena. Kaburi lilipojaa wakaanza kushindilia kwa mikono. Mama Salma, mama wa marehemu alilia kwa nguvu hadi nikamwonea huruma japo mimi mwenyewe nilishikwa na uchungu sana kumpoteza mwanangu.
Kisha tukaweka mataji kwenye kaburi la mwanangu, nilianza mimi akafata mama yake akafuata Sabrina dada yake na kisha wajomba, binamu, shangazi na ndugu wengine wakafuata. Mazishi yalipomalizika mtangazaji, mzee Ndeluvale akatangaza kuwa watu warudi nyumbani kwa wafiwa wakanawe mikono, akimaanisha wakale chakula. Basi watu wakaanza kurudi, mimi nilikawia kidogo, nilitamani kama nibaki kaburini lakini ilinilazimu niondoke.
Tulipofika nyumbani chakula kilikuwa kimeandaliwa, watu wakala wakashiba na kusaza. Mimi sikuweza kula mchana ule. Nilianza kufatilia kujua hali ya binti yangu Salma aliyekuwa amepoteza fahamu wakati wa kwenda kuaga maiti ya mdogo wake. Hali ya binti yangu ilikuwa shwari, nikatiwa matumaini.
Usiku watu waliobaki kukesha na kuomboleza pamoja nasi, walikuwa wakiimba nyimbo za aina nyingi. Baadhi ya nyimbo hizo nilikuwa nazifahamu na nyingine zilikuwa ngeni kabisa kwangu. Nyimbo nilizokuwa nazifahamu ni kama vile ule unaoitwa Twiwalala:
Uliimbwa hivi:
Moooja, mbili tatu twende twiwalala, (We twiwalala) x 2
Ve twiwalala umwanavesu(We twiwalala)
Umwana vesu asivoneha (We twiwalala)
Umwana vesu ahele hwina (We twiwalala)
Moooja, mbili tatu twende twiwalala, (We twiwalala) x 2
Pia waliimba ule wimbo wa “Parapanda italia,” pia na nyimbo nyingine nyingi zilizomtaja na marehemu mwanangu. Tulifarijika kwani watu waliguswa na kifo cha mwanetu hata wakashiriki nasi katika tukio hilo. Uliipoimbwa wimbo wa `twiwalala` sikusita kusimama na mimi kuimba. Kwa kawaida wimbo huu unapoimbwa kwenye msiba watu huanza kucheza kwa kuruka na kuzungukazunguka wakipapasapasa kama vile wanatafuta kitu kilichopotea na kwa wakati ule hakika ulikuwa ni wakati wa kumtafuta mwanangu Sostenes. Hivyo nilijumuika nao kupapasa kumtafuta mwanangu.
Tulicheza tukaruka tukiimba huku tukipiga yowe, huuuuwi, huuuuwi! Mara tukaanza kuondoka kuelekea makaburini. Akina mama fulani waliokuwa wanaimbisha walitangulia mbele, mimi nilikuwa katikati ya watu wengine, nami nilikuwa nikiimba kwa sauti kwani wimbo ule nilikuwa naufahamu vizuri na nilikuwa naupenda. Tukashuka ule mteremko mara tukakata kona, tukapitiliza vile vichaka vilivyo jirani na makaburi hatimaye tukaingia eneo la makaburini usiku ule huku tukiimba kwa sauti na kupiga yowe. Hapo sasa na mimi nikaharakisha nikawa mbele jirani na wale akina mama waliokuwa wanaimbisha. Kwa mbali niliweza kuona eneo ambalo tulimzika mwanangu. Tulivyozidi kusogea kwa mbali niliona kama kitu cheusi mfano wa kifurushi kikitoweka kutoka pale lilipo kaburi la mwanangu. Nilishituka ghafla nywele zikasimama, mapigo ya moyo yalienda kwa kasi, moyo ukadunda duf-duf-duf kijasho chembamba kikaanza kunitoka. .................
Endelea kukalia kigoda mwanakwetu, tuendelee sura ya pili, usiikose tafadhari
KALIA KIGODA MWANAKWETU FATILIA SURA YA PILI BAADA YA HII
ReplyDelete