KUMBE
JIRANI YANGU
MCHAWI
Mtunzi:
Elias
K. Mwalongo
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
KUMBE JIRANI YANGU MCHAWI
@Copyright by: Elias K.
Mwalongo
S. L. P 977 Njombe
Simu: +255769313224
E.mail: mwalongoelias7@gmail.com
Facebook: Elias Mwalongo
Twitter: Elias Mwalongo
Instagram: @mwalongoelias
Chapa Ya Kwanza, Januari,
1, 2017
Haki
zote zimehifadhiwa. Huruhusiwi kuiga, kupiga chapa, kutafsiri au kukitoa kitabu
hiki kwa jinsi yoyote ile pasipo idhini ya mwandishi wa kitabu hiki au mhariri
mhariri wake. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
SURA YA KWANZA
Tangu
siku ile sijawahi kabisa kupata lepe la usingizi. Nimekuwa mtu wa shuruba na
kujiinamia chini nisijue nini nifanye.Nikijaribu kulala chali nitazame juu
ambako naamini ndiko aliko mwenyezi sipati nafuu, nikilala kiubavu nitazame
pembeni huko nayo nagundua kuwa haisaidii, nikijaribu kulala kifudifudi nifumbe
na macho nisikumbuke yote yaliyonisibu maishani na kunifikisha hapa kifungoni, bado
nagundua kuwa ni kazi bure. Nikiamua kuamka na kujiketisha chini niegame
ukutani huku nikijiinamia. Nafurukuta nawayawaya natamani kama nijifinye au
nijipige teke. Mapigo ya moyo yanaenda kwa kasi yanapiga kama saa ya ukutani
pwi-pwi-pwi. Makamasi yananifura kama mbeta
ya ulanzi wa masika. Machozi yananitiririka mashavuni mwangu hadi chini yanatua
huku yakilowanisha shati langu. Moyo umekufa ganzi hata nahisi kama vile
unataka kumrudia aliyeuumba na mwili wangu huu kushuka mavumbini ulikotoka.
Nahangaika
masikini Elias mimi kupoteza mawazo juu ya mazishi ya mwanangu Sabrina, binti
yangu mdogo, wa pili kuzaliwa. Binti yangu mashuhuri aliyenifanya nijivune hapa
kijijini na kuonekana wa maana. Mazishi ya binti yangu yananirudisha mbali
nilikotoka na mikasa ya maisha iliyonikumba. Masikini mimi ninakumbuka kifo cha
Salma dada yake Sabrina, narudi nyuma tena namkumbuka marehemu mwanangu
Sostenes mdogo wao wa mwisho niliyempoteza angali mdogo kabisa. Tena ninakumbuka
sana siku ile nilipotupa udongo kwenye kaburi la mke wangu kipenzi Salome,
binti wa kipangwa niliyempata kwa shida nikalipa
na mahali ya mafahali mawili kisha nikamuweka ndani awe mama wa wanangu, naye
nilimpoteza angali kijana kabisa akaongozana na binti yake mkubwa Salma
wakaniacha nafurukuta nalia na moyo wangu. Najaribu kufurukuta nisikumbuke ndo
kwanza picha ya matukio hayo inanijia vizuri kabisa. Uvumilivu unanikabili na
kunishinda nguvu, wacha nichukue kalamu yangu niwaandikie walau mjifunze kitu
ili siku yatakapowakuta na nyinyi msihukumiwe kifungo cha maisha na kusota
kifungoni huku kama mimi.
Ninakumbuka
vishindo vya siku ile nikiwa kitandani usiku wa manane nimepumzika na mke wangu
mpendwa. Vishindo vilivyosikika kuanzia kwenye dirisha la chumba changu
vikazunguka nyumba yangu hadi upande wa pili kwenye chumba cha wanangu. Kwa
hofu nikamwamsha mke wangu aliyekuwa amelala fofofo asikilize na yeye vishindo
hivyo. Jinsi nilivyomwamusha ndivyo vishindo vilivyozidi kusikika kwa nguvu
vikisogea tena jirani na dirisha la chumba chetu. Mwili ulitetemeka, kijasho
chembamba kikanimiminika, na nywele zikanisimama. Mimi na na Mama Salma
tukapiga moyo konde, yote tukamwachia mwenyezi maana yeye ndiye mpaji na
mnyimaji. Vishindo vikaishia dirishani kwetu vilikoanzia na ghafla vikatoweka,
kukawa kimya kabisa. Nilijaribu kufikiria ni nini kilikuwa kinatokea lakini
sikupata jibu. Tulibaki tumedhoofika kwa hofu na mashaka. Tulijaribu kulala
lakini haikuwezekana kwani hatukupata usingizi kabisa. Nilijaribu kuwasha tochi
ya simu yangu, nikamulika kuanzia kwenye mlango wa chumba chetu sikuona kitu
chochote, nikamulika kwa kona ya chumba chetu nikamwona mende mmoja tu akipotelea
kwa sanduku la nguo la Mama Salma, nilimulika chumba kizima sikuona cha pekee,
basi nikaizima tochi yangu. Baadae tulianza kunong`ona kwa sauti ya chini sauti
iliyokuwa imejaa hofu na mashaka makubwa. Baadaye tulikaa kimya kwa kitambo
kirefu. Macho yangu yalianza kuwa mazito, usingizizi ukaanza kuninyemelea kwa
mbali. Ghafla nikaamshwa na jogoo wa Ndeluvale aliyewika kwa sauti kubwa.
Ndeluvale yule jirani yangu mhunzi na fundi wa kutengeneza mikeka, na vikapu.
Alikuwa na kuku wengi sana na walikuwa wakilala juu ya mti uliokuwa unapakana
kati ya nyumba yangu na yake. Yule jogoo alipowika nikashtuka toka usingizini.
Nikachukua simu yanu ya Tecno, nikaiwasha ili nitazame muda. Ilikuwa sa kumi na
moja na dakika ishirini na tatu alfajiri. Kule kusinzia kulinisahaulisha vituko
vilivyotokea usiku wa manane, sasa nikawa macho na taratibu kumbukumbu zikaanza
kunirudia, nikakumbuka vizuri mimi na Mama Salma tulivyohangaika usiku kwa hofu
na mioyo kutupwitapwita. Nikageuka kumtazama Mama Salma aliyekuwa amelala pembeni
yangu, giza lilinizuia sikuweza kumtazama vizuri, nikataka niwashe tochi ya
simu yangu ila nikaamua kuacha kwani kwa mbali nilikuwa namsikia akikoroma.
Niliendelea kutafakari huku nimejiegesha kitandani nisione dalili ya kupata
usingizi tena. Baada ya dakika chache nilianza kuhisi mwanga ukiongezeka
mle chumbani tokea dirishani, kumbe
kulikuwa kunaelekea kupambazuka. Haikupita kitambo kikubwa Mama Salma naye
akavuta pumzi ndefu kisha akageuka alale vizuri basi nikamwamsha kwani muda nao
ulikuwa umetokomea. Akanitazama kwa mbali kwa kutumia mwanga ule ulioanza
kupenyeza dirishani alfajiri ile. Baada ya muda nikaanza kumkumbusha kuhusu
tukio la usiku lililotuogofya. Tulijaribu kuulizana ni nini kilichotutisha
usiku lakini hakuna aliyeweza kugundua. Basi tukaamua kupotezea.
Niliamka
nikatoka chumbani kwangu nikaanza kutoka taratibu kuelekea sebuleni. Kabla
sijafika mlango wa kutokea nje nikashitushwa na kelele za mlango uliobamizwa
chumbani kwa wanangu. Nikageuka haraka, masalale! Kumbe alikuwa ni Salma binti
yangu wa kwanza. Nikamwuliza kulikoni mwanangu? Akajibu, baba Sostenesi
anaumwa. Nikarudi haraka chumbani kumwita Mama Salma, ili aende akaangalie
watoto. Akakurupuka haraka alijifunga kanga kiunoni, akavaa ndala zake na
kukimbia hadi chumbani kwa Salma na wadogo zake. Alipofika alimkuta Sostenes
akiwa amejilaza kitandani kwake, kitanda kilichokuwa pembeni mwa kitanda
walichokuwa wanalalia dada zake Salma na Sabrina. Akamwuliza anaumwa nini, yeye
katika umri wake mdogo hakuweza kueleza akasema tu kuwa hajisikii vizuri na
mwili mzima ulikuwa unauma. Walijitahidi kumshawishi asimame lakini hakuweza
kuhimili peke yake alihitaji kushikiliwa. Alikuwa amenyong`onyea hawezi
kusimama peke yake. Basi tukahangaika masikini sisi tukampeleka dispensari yetu
ya kata kwa pikipiki. Tulipofika tulipokelewa vizuri na manesi wawili.
Tukawakabidhi mgonjwa wetu nasi tukaketi kwenye veranda kwanye benchi
tukisubiri kuambimbwa mwanetu alikuwa anaumwa nini hasa.
Kule
nyumbani Salma na Sabrina walikuwa wameenda shuleni. Tukaendelea kunong`ona
pale nje mimi na mke wangu Salome. Mara mlango ulifunguliwa na nesi mmoja
akatoka akatuambia kuwa mgonjwa wetu alikuwa anazidiwa na vipimo walivyokuwa
navyo haviwezi kusaidia kujua tatizo la mgonjwa wetu, hivyo walitushauri
tumpeleke hospitari ya wilaya ili tukasaidiwe huko. Maskini sisi, kipatochetu
chenyewe ni duni. Basi tukachukua akiba yetu ya pesa tukaanza safari kuelekea
hospitari ya wilaya ya kipindi hicho ambayo sasa ni hospitari ya mkoa wa
Njombe. Tukiwa kwenye gari kuelekea hospitarini mwanetu Sostenes alitukatisha
matumaini. Nilimwangalia mwanangu, nikaona mwanangu macho yamemtoka pima, mdomo
wake mdogo na mwembamba ulikuwa umelegea na uko wazi, mapigo ya moyo yalipiga
taratibu kama saa ya ukutani ambayo betri imeisha nguvu yake. Macho ya mwanangu yalinitazama mimi bila
kukonyeza mithiri ya mtu anayetaka kumaanisha kitu. Nikahisi kama vile mwanangu
anataka kumaanisha `kwaheri`. Nilitamani hata nijipige teke nikome kufikilia
kuwa mwanangu ananiaga lakini ndivyo ilivyokuwa. Niliendelea kumkodolea macho
mwanangu kama yeye alivyonikodolea bila kukonyeza, lakini tulivyoendelea
kutazamana vile mara nikaona macho yake yakazidi kusinyaa na kuwa madogo hadi
yakafumba. Masalale! Moyo ulinidunda kwa nguvu na kwa woga. Nikamtikisa
mwanangu alikuwa amelegea yuko hoi hana hali. Nikajaribu kusikiliza mwendo wa
mapigo ya moyo kama ni ya haraka au taratibu, chaajabu niliishia kusikiliza
mapigo ya moyo wangu mwenyewe. Kumbe sasa nilikuwa sijampakata mwanangu bali
maiti ya mwanangu. Machozi yalianza kunitiririka mashavuni. Mama Salma sasa
ilikuwa ni kilio na yowe. Tulihuzunika sisi tukalia na kuomboleza juu ya
mwanetu aliyetutoka hali hatujui alikuwa anasumbuliwa na tatizo gani. Basi
tuligeza gari na kuanza kurudi nyumbani. Sasa safari yetu ilikuwa ni ya
kusafirisha maiti kupeleka nyumbani badala ya kusafirisha mgonjwa kwenda
hospitari.
Tulifika
kijijini kwetu mida ya jioni sana, tukakuta maandalizi ya msiba yanaendelea
kufanyika kwani tuliwataarifu ndugu na jamaa kwamba mwanetu kipenzi ametutoka.
Nasi tulipofika tulikuta ndugu wengine wakiwa wanalia kwa uchungu mkubwa,
uchungu wenye masikitiko ya kumpoteza mwanetu kipenzi, mwanetu pekee wa kiume,
mrithi wetu na tumaini la familia yetu. Msiba ulipokelewa maiti ikawekwa kwenye
chumba maalumu nasi wafiwa tukaingia humo kuomboleza. Maandalizi yaliendelea,
ndugu jamaa na majirani walifika kwenye msiba tukaomboleza pamoja. Moto
ulikokwa nje uwanjani, watu walipika vyakula, michango mingi ilitolewa nao
majirani kwa mioyo minyofu waliomboleza pamoja nasi usiku mzima hadi asubuhi.
Siku hii ya pili ilikuwa ni siku ya mazishi ya mwanangu Sostenes. Ilikuwa ni
siku ya mwisho ya kuona sura ya mwanangu. Ilinipasa nianze kusahau tabasamu
lake, kicheko chake na upole wake uliojionyesha hata kwa mwonekano wa sura
yake.
Maandalizi
yalikamilika, mwanangu Sostenes akafungwa kama pipi kwenye sanda, akadumbukizwa
kwenye jeneza dogo la saizi yake. Ilipofika saa nane mchana, jeneza likawekwa
nje uwanjani, mwenyekiti wa msiba ule Mzee Ndeluvale ambaye alikuwa jirani
yangu akatangaza kuwa maiti itaanza kuangwa tukianzia sisi wazazi wa marehemu,
dada zake na ndugu wengine watafata hadi jamaa wote waishe. Agizo hilo
lilifuatwa. Mimi nikawa wa kwanza kujongea mbele ya jeneza kuitazama sura ya
mwanangu kwa mara ya mwisho. Nilisogea kwa ujasiri lakini ujasiri ukaniisha,
chozi likanishuka. Nikachukua leso yangu mfukoni nikaanza kufuta machozi
yaliyokuwa yakinititika mashavuni mwangu nikimlilia mwanangu. Mama yake ndo
kabisa hakuweza kustahimili maumivu, aliishiwa nguvu asiweze hata kusimama peke
yake alishikiliwa na ndugu wengine wakamkokota taratibu amtazame mwanae kwa
mara ya mwisho. Sabrina. Dada yake mdogo wa marehemu Sostenes naye alilia kwa
uchungu mkubwa, watu wakamshikilia upande kwa upande na kumsogeza jirani na
jeneza la Sostenes mdogo wake. Huku akilia kwa kwikwi aliiangalia sura ya mdogo
wake kwa mara ya mwisho kisha akapelekwa pembeni. Ndugu wengine wa marehemu nao
wakapita kuuaga mwili wa ndugu yao Sostenes kisha majirani na wageni wote
walifika kujumuika nasi wakapita kumwaga mwanangu kipenzi aliyekuwa amenitoka
angali mtoto. Wakati zoezi hili likiendelea, Salma dada wa marehemu Sostenes
aliyekuwa pembeni akadondoka ghafla na kupoteza fahamu. Watu wakambeba
wakamweka kwenye kivuli wakampepea kwa muda mrefu lakini haikusaidia, akapelekwa
hospitalini ambako alilazwa akahudumiwa vizuri na wauguzi.
Wakati
ukafika wa kwenda makaburini kumzika mwanagu Sostenes. Sikuamini yaliyokuwa
yakitokea siku ile. Niliona kama vile ni ndoto ninayoiota alasiri ile, lakini
ulikuwa ndo ukweli wenyewe. Watu wakalibeba lile jeneza lililokuwa na mwili wa
mwanangu huku wakipokezana baada ya kila kitambo kidogo.
Hatimaye wakafika nalo
makaburini, wakaliweka jeneza pembeni mwa kaburi lililokuwa limeshaandaliwa.
Katekista aliongoza sala ya mazishi, kisha zoezi la kumzika mwanangu likafuata.
Jeneza liliingizwa kaburini taratibu hadi likatua kwenye sakafu ya kaburi lile.
Wakachota mchanga na kuniletea ili mimi niwe wa kwanza kutupa mchanga kaburini
japo kiganja kimoja. Nikasisimuka mwili, taratibu nikachota ule mchanga
nikaumimina taratibu kwenye kaburi la mwanangu Sostenes. Jinsi nilivyozidi
kumimina ule mchanga ndivyo na machozi yalivyozidi kunitiririka na mengine
kumiminika hadi ndani ya kaburi la mwanangu. Nilipomaliza nikaondoka taratibu
ili kumpisha mke wangu naye amzike mwanaye. Haikuwa rahishi Mama salima
kuchukua kiganja cha mchanga na kumimina kwenye kaburi la mwanae, basi wanawake
Fulani walimshikilia na kumsaidia hadi akatupa mchanga ndani ya kaburi la
mwanae. Akafuata Sabrina japo naye kwa kushikiliwa. Ndugu wengine wakafuata na
baadaye wengine wakalishambulia kaburi la mwanangu kwa kutupia mchanga kwa
kutumia spedi na kushindilia kwa visigino vyao. Mimi nikiwa nimesimama pembeni
niliwaza moyoni mwangu, nikajaribu kukumbuka mwanangu, machozi yakaanza kutoka
tena. Kaburi lilipojaa wakaanza kushindilia kwa mikono. Mama Salma, mama wa
marehemu alilia kwa nguvu hadi nikamwonea huruma japo mimi mwenyewe nilishikwa
na uchungu sana kumpoteza mwanangu.
Kisha
tukaweka mataji kwenye kaburi la mwanangu, nilianza mimi akafata mama yake
akafuata Sabrina dada yake na kisha wajomba, binamu, shangazi na ndugu wengine
wakafuata. Mazishi yalipomalizika mtangazaji, mzee Ndeluvale akatangaza kuwa
watu warudi nyumbani kwa wafiwa wakanawe
mikono, akimaanisha wakale chakula. Basi watu wakaanza kurudi, mimi
nilikawia kidogo, nilitamani kama nibaki kaburini lakini ilinilazimu niondoke.
Tulipofika
nyumbani chakula kilikuwa kimeandaliwa, watu wakala wakashiba na kusaza. Mimi
sikuweza kula mchana ule. Nilianza kufatilia kujua hali ya binti yangu Salma
aliyekuwa amepoteza fahamu wakati wa kwenda kuaga maiti ya mdogo wake. Hali ya
binti yangu ilikuwa shwari, nikatiwa matumaini.
Usiku
watu waliobaki kukesha na kuomboleza pamoja nasi, walikuwa wakiimba nyimbo za
aina nyingi. Baadhi ya nyimbo hizo nilikuwa nazifahamu na nyingine zilikuwa
ngeni kabisa kwangu. Nyimbo nilizokuwa nazifahamu ni kama vile ule unaoitwa Twiwalala:
Uliimbwa
hivi:
Moooja, mbili tatu twende
twiwalala, (We twiwalala) x 2
Ve twiwalala umwanavesu(We
twiwalala)
Umwana vesu asivoneha (We
twiwalala)
Umwana vesu ahele hwina (We
twiwalala)
Moooja, mbili tatu twende
twiwalala, (We twiwalala) x 2
Pia
waliimba ule wimbo wa “Parapanda italia,” pia na nyimbo nyingine nyingi
zilizomtaja na marehemu mwanangu. Tulifarijika kwani watu waliguswa na kifo cha
mwanetu hata wakashiriki nasi katika tukio hilo. Uliipoimbwa wimbo wa `twiwalala`
sikusita kusimama na mimi kuimba. Kwa kawaida wimbo huu unapoimbwa kwenye msiba
watu huanza kucheza kwa kuruka na kuzungukazunguka wakipapasapasa kama vile
wanatafuta kitu kilichopotea na kwa wakati ule hakika ulikuwa ni wakati wa
kumtafuta mwanangu Sostenes. Hivyo nilijumuika nao kupapasa kumtafuta mwanangu.
Tulicheza
tukaruka tukiimba huku tukipiga yowe, huuuuwi, huuuuwi! Mara tukaanza kuondoka
kuelekea makaburini. Akina mama fulani waliokuwa wanaimbisha walitangulia
mbele, mimi nilikuwa katikati ya watu wengine, nami nilikuwa nikiimba kwa sauti
kwani wimbo ule nilikuwa naufahamu vizuri na nilikuwa naupenda. Tukashuka ule
mteremko mara tukakata kona, tukapitiliza vile vichaka vilivyo jirani na
makaburi hatimaye tukaingia eneo la makaburini usiku ule huku tukiimba kwa sauti
na kupiga yowe. Hapo sasa na mimi nikaharakisha nikawa mbele jirani na wale
akina mama waliokuwa wanaimbisha. Kwa mbali niliweza kuona eneo ambalo
tulimzika mwanangu. Tulivyozidi kusogea kwa mbali niliona kama kitu cheusi
mfano wa kifurushi kikitoweka kutoka pale lilipo kaburi la mwanangu.
Nilishituka ghafla nywele zikasimama, mapigo ya moyo yalienda kwa kasi, moyo
ukadunda duf-duf-duf kijasho chembamba kikaanza kunitoka.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
SURA YA PILI
Nilijaribu
kuwatazama wale wanawake nilikuta wala hawashituki kana kwamba hawajaona
chochote, waliendelea kuimba kwa sauti na kupiga mayowe. Wala hakuna hata mtu
mmoja aliyeonyesha kushangaa kile nilichokuwa nimekiona mimi. Nikajua ni mimi
tu niliyekuwa nimeona na pengine nilitazama vibaya. Hivyo na mimi nikapotezea,
nikaendelea kucheza na kuimba kama wengine kanakwamba na mimi sikuona kitu
chochote cha kushangaza.
Tuliimba
tukaruka na kucheza kuzunguka kaburi la mwanangu Sostenes, tulipiga mayowe. Mimi
machozi yakanibubujika nilipomkumbuka mwanangu kipenzi, lakini nikapiga moyo konde.
Baada ya kuzunguka lile kaburi mara dufu kisha tukaanza kurudi tunaimba
nyumbani. Tulipoondoka kutokana na ukimya tuliouacha watu wengine walikuwa
wameshalala, na sisi tulipowasili tulikuwa tumechoka na muda umeyoyoma, wengi
wetu tukaenda kulala.
Mazungumzo
ya watu waliokuwa wanaota moto nje yalinishitusha kutoka usingizini.
Nilipojifunua blanketi usoni nikakutana na mwanga mkali wa asubuhi ile ambao
ulikuwa umetanda mle chumbani. Nikatazama saa yangu kumbe ilikuwa ni saa kumi
na mbili na nusu asubuhi. Nikaamka nikajiandaa ili nitoke nje. Nilipofungua
mlango tu, nilikutana uso kwa uso na Ndeluvale jirani yangu, alikuwa
akitabasamu kama vile alikuwa amefurahishwa na mazungumzo yaliyokuwa
yakiendelea pale nje huku wakiota moto. Lakini cha ajabu aliponiona tu, midomo
yake iliyofunguka huku meno yakiwa nje nje na macho yakionyesha kuwa ni mwenye
furaha ghafla vyote vilisinyaa, akafunga mdomo, meno hayakuonekana, macho
yalionyesha ni mwenye aibu kama vile mtu ambaye amekosea jambo. Mimi sikujali,
nikatoka pale nje nikawasalimia wote mikononi kwa upole tu nao wakapokea salamu
yangu wakiambatanisha na pole kwa msiba. Nikajumuika nao kuota moto na
kuendelea kusikiliza mazungumzo yao. Kufikia mida ya mchana watu wengi walikuwa
wameshatawanyika wamerudi kwao kuendelea na shughuli zao za kila siku. Na
ilipofika jioni wageni waliohitaji kulala ni baadhi tu ya ndugu zetu mana
wengine walikuwa wameondoka na kurudi kwao. Nao ndugu zetu wachache waliokuwa
wamekesha pamoja nasi na wakalala waliondoka asubuhi na kwenda kwao. Nikabaki
mimi, mke wangu Salome na binti zetu wawili Salma na Sabrina baada ya kumpoteza
mwanetu Sostenes mwanetu wa mwisho. Tukaendelea na shughuli zetu za kila siku
huku tukilima na kuvuna na wanetu wakiendelea na shule.
Baada
ya miezi kadhaa, mimi na mama Salma tulikuwa tumeshaanza kulisahau kabisa tukio
la kumpoteza mwanetu Sostenes. Tukaendelea kuganga na maisha huku tukiwasomesha
wanetu wawili waliokuwa wamesalia. Tuliendelea kulima mahindi, maharage, viazi,
njegere na ngano. Tulilima kwa juhudi huku tukivuna na kuuza ili tupate mapesa ya kuwasomeshea wanetu Salma na
Sabrina na kupata chochote kitu ndani
ya nyumba.
Mwaka
ule hakika tulijaliwa kupata mavuno ya
kucheba. Tulilima mahindi, maharage na ngano vyote vikastawi vizuri
vikanawili na kushona mashamba yetu. Ilipofika kiangazi muda wa kuvuna ilikuwa
inatulazimu kurudi nyumbani kwa kuchelewa sana muda ukiwa umeenda, jua limezama
na wakati mwingine tulikuwa tunarudi nyumbani usiku hata jua limeshajiendea
kwao. Tulikuwa tukirudi nyumbani tunakuta wanetu wamesharudi toka shuleni
wamefanya usafi pale nyumbani, nje na ndani kama tulivyowafundisha. Muda
mwingine tulikuwa tukichelewa zaidi tunakuta wameshapika na chakula wanajisomea
huku wanatusubiri tufike tule pamoja.
Siku
hii ilikuwa tofauti kabisa. Siku hii ndio niliyotamani kugaagaa chini,
nilitamani nilie huku nikitupatupa miguu kama mtoto mdogo anayelilia kunyonya
au aliyenyang`anwa mdoli aliokuwa akiuchezea. Nilipiga moyo konde lakini wapi.
Ilikuwa ni siku ile nimejitokea shambani na mke wangu, tulipokaribia kufika
nyumbani kwa mbali tuliona watoto wa shule wakiwa wamejaa nje ya nyumba yetu.
Tulijua labda wamekuja tu kuwatembelea rafiki zao maana wanetu walipendwa sana
shuleni kwao kwa tabia zao nzuri walijipatia marafiki tele ambao mara nyingi
walikuwa wanawatembelea hasa siku za Jumapili. Lakini siku hii ilikuwa ni Jumatano,
tena muda ulikuwa umeshaenda giza ndo linanyemelea na wote walikuwa bado
wamevaa sare za shule kanakwamba ndo wapo shuleni kumbe ni nyumbani kwangu.
Nilijiuliza maswali mengi lakini sikupata jibu la haraka. Basi tukasogea kwa
haraka ili kujua kilichokuwa kinaendelea. Tuliposogea jirani zaidi tukagundua
wale watoto walikuwa na nyuso za huzuni, basi nikatupia huko ukuni ambao
nilikuwa nimeubeba begani mwangu nikatangulia mbio nikimwacha mama Salma nyuma.
Nikakuta wale watoto wamezunguka duara. Bila kusalimia wala kuhoji chochote
nikapitiliza moja kwa moja kuchungulia nini kilikuwa katikati ya lile duara
walilolitengeneza. Masalale! Nikakuta binti mmoja amempakata mwanangu Sabrina.
Sabrina mwanangu alikuwa amelegea, amenyong`onyea yuko hoi bin taabani,
anapumua kwa mbali hana hali binti yangu kipenzi. Nilihangaika mimi, niliingia
ndani mara natoka hata nisijue nifanye nini. Nilihisi kuchanganyikiwa na akili
kuniruka. Mama Salma akabaki analia pale nje mbele ya watoto wa shule, Salma
nae ndo kwanza alikuwa Amelia hadi macho yamekuwa mekundu akabaki sasa analia
kwa kwikwi asiweze kusema lolote. Kwa ujasiri nikamwuliza binti mmoja aliyeitwa
Eliza, binti wa Mtendaji wa kijiji chetu alifahamika kwa jina la Ngomiposo,
ambaye nilimfahamu kuwa ni rafiki wa karibu sana wa Sabrina ili anisimulie
kilichomkuta binti yangu. Eliza hakusita akanieleza kwa uwazi na kwa makini
akasema, “Sabrina aliniambia mchana kuwa kichwa kilikuwa kinamsumbua, tukajua
labda ni jua lile kali la mchana lilikuwa linamdhuru, lakini baadaye akasema
anahisi kizunguzungu na muda si mrefu akadondoka na kupoteza fahamu. Kwakuwa
ulikuwa umefika muda wa kurudi nyumbani kuna mwalimu alisema tumbebe tumlete
nyumbani. Tumekuja tunapokezana hadi tumefika hapa na tulipokuwa njiani
alionyesha dalili za kutaka kuzinduka lakini alipozinduka ndio tukakuta amebaki
amenyong`onyea amelegea hadi huruma jamani rafiki yetu. Tukajaribu kumuuliza
nini kinamuuma japo kwa shida akasema mwili mzima unauma na wala hana nguvu.
Tulipofika tulitaka tumpe chochote ale amekataa, hata maji ya kunywa nayo amekataa.
Ndio maana tukaona ngoja tuwasubiri hapa hadi wazazi mrudi maana tusingemwacha
peke yake.”
Niliwashukuru
wale watoto kisha nikawasihi warudi nyumnani wasije wakaanza kutafutwa nasi
tutamshughulikia Sabrina. Wakaondoka kwa
upole kanakwamba walitamani kuendelea kushuhudia hali ya rafiki yao. Wale
watoto walipoondoka jioni ileile tulimpeleka mgonjwa kwenye dispensari ya
kijiji lakini tuliambiwa kuwa mgonjwa amezidiwa na hawangeweza kutusaidia hivyo wakatushauli tumpeleke
hospitali ya wilaya. Kule kwenye hospitari ya wilaya ya kipindi hicho ambayo
kwa sasa ndio imepewa hadhi ya kuwa hospitali ya mkoa walitupokea wakamfanyia
vipimo mgonjwa wetu lakini wakasema hawakugundua tatizo lolote. Na hali ya
mgonjwa iilikuwa ni dhaifu, alilegea mwili mzima hakuweza kusimama wala
kutembea peke yake, alilalamika kuwa mwili wote unauma, miguu ilikuwa inauma na
kuvimba na pumzi ilikuwa inambana. Kwa hali hii Daktari aliponiambia kuwa
hawakugundua tatizo lolote niliishiwa pozi. Pale hospitali walitushauri
tumpeleke hospitali ya rufaa.Tulikubali ushauri wao lakini mimi mawazo
yalinihama, nilianza kumuwaza na kukumbuka mazishi ya mwanangu Sostenes.
Nilimtazama mwangu Sabrina usoni, kisha machozi yakanitoka yakatiririka mashavuni
mwangu kama mto ruhuji.
Jioni
ile tulirudi nyumbani na mgonjwa wetu.
Baadhi ya ndugu na majirani walitushauri tuondoke naye jioni ile kwenda hospitali
kubwa, nasi tulikubali kufanya hivyo lakini jioni ile pale nyumbani kulikuwa na
rafiki yangu mmoja wa karibu sana aliyefahamika kwa jina la Shomeho. Aliniita
pembeni akanishauri akisema, “inabidi mwende mkatembee”. Nilimtazama usoni
kwani sikumwelewa alitaka kumaanisha nini. Ile kumtazama tu aligundua kuwa
sikumwelewa, akaendelea, “ndio, mtazunguka hospitali zote watawaambia hawaoni
tatizo, kwahiyo cha msingi hapa ni mguu kwa mguu kwa mganga wa kienyeji,
atawasaidieni”. Alipotaja tu neno “mganga wa kienyeji” nikamtazama kwa ukali.
Nikamwambia, “Shomeho kama huna cha kusema naomba ushone domo lako unyamaze,
sio kunitajia mimi habari za mganga wa kienyeji. Mimi ni Mkristo tena mkatoriki
na ni mtu mzima na ninajivunia utu uzima wangu. Eti nimuudhi muumba wangu
ninayemwabudu kwa kuwafuata waganga. Mwee, nimalize pesa zangu kisa kumpa
mganga wa kienyeji, anivalishe hirizi kiunoni na shingoni. Shomeho usinitie
uchuro na ubaladhuri. Loo! Mguu huu haukanyagi kwa mganga ng`oo, yote namwachia
Mungu.” Shomeho alitikisa kichwa akasema, “sawa ndugu yangu mimi nilikuwa
nakushauri tu, naomba uniwie radhi kwa domo
langu chafu, lakini `asiyesikia la mkuu huvunjika guu, mimi ndio rafiki
yako na vilevile ni kaka yako nilikutangulia kuliona jua rafiki yangu, usinibeze`”.
Nikasema `sawa ndugu yangu usiku mwema.`
Niliporudi
ndani, mke wangu alinigundua kuwa nilikuwa nimefura hasira, akaniuliza,
“kulikoni baba Salma mbona uko hivyo”. Nikamwambia, “mke wangu, we acha tu,
watu wanatuchezea hapa kijijini. Mtu mzima na busara zake badala ya kutushauri
tumtibu mwanetu eti anatushauri twende kwa mganga, mke wangu, umewahi kukanyaga
kwa mganga wewe? Kama ni matatizo tayari tunayo kwanini kwenda kutafuta mengine
huko?” Mke wangu akasema, “kwahiyo umemjibu nini mume wangu?” Nikamwambia,
“katu mguu huu haukanyagi kwa mganga. Nimemwacha aende zake” Mke wangu
aliniangalia kama vile alikuwa na neno la kusema, lakini akaishia kuguna kwa
sauti ya chini, akamtazama Sabrina aliyekuwa amelala pale sebuleni, akiwa
mgonjwa hajiwezi na sisi bado hatujui kilichomsibu mwanetu hadi kuwa mahututi
vile. Nami nilitamani kutoa machozi kumlilia mwanangu, lakini nilijikaza
kisabuni, nikaacha kabisa kufikiria juu ya ushauri wa Shomeho kutaka twende kwa
mganga.
Usiku
ule sikupata usingizi mawazo yalikuwa mbali huko nisikojua. Mama Salma na
mgojwa Sabrina na Salma dada wa Sabrina walilala sebuleni, mimi nilijiegesha
chumbani kwangu nisipate hata lepe la usingizi. Dakika zilizidi kwenda mbio,
masaa nayo yakayoyoma huku nikiwaza nifanyaje mwanangu apone. Sikutaka
kuendelea kufikiria juu ya ushauri wa Shomeho kuhusu kwenda kwa mganga wa
kienyeji kuagua kwani nilikuwa sijawahi kufanya hivyo, ukizingatia mimi
nilikuwa nimesoma seminarini ambako walitukanya kabisa mambo ya kuwategemea
waganga wa kienyeji.
Ulikuwa
ni usiku mtulivu kabisa, kulikuwa kimya kabisa zilisikika tu sauti za vyura
wakilia kwa mbali sana. Ukimya huu ulianza kunishawishi nisinzie. Macho
yalianza kuwa mazito, kope zikaanza kunifunga na kufunguka kwa taabu. Usingizi
ukanikuda roba nami nikashindwa kupambana nao nikalala.
Nikiwa
usingizini nilishitushwa na sauti za bundi wawili waliokuwa wakipiga kelele kwa
kupokezana. Bundi hao walikuwa juu ya paa la nyumba yetu mmoja upande wa
kushoto na mwingine upande wa kulia mwa nyumba. Nikiwa bado usingizini
niliwasikiliza vizuri huku moyo ukidunda kwa nguvu na mapigo ya moyo yakiwa
yanaenda kasi ajabu. Nikapiga moyo konde, nikajivika ujasiri, nikajikaza
kisabuni, kwa ujasiri nikaamka kitandani nikashuka nikavaa ndala zangu kisha
nikaanza kutoka taratibu kuelekea mlangoni. Nilifika mlangoni huku nikipapasa
maana ilikuwa ni giza tupu mle chumbani. Nikafungua mlango wa chumba changu
taratibu kisha nikatokea sebuleni. Pale sebuleni kulikuwa na mwiko mkubwa ambao
mke wangu alikuwa akiutumia kukorogea pombe ya machicha aliyokuwa akikorogea
kwenye pipa, basi nikaubeba ule mwiko, nikaanza kutoka nje, nikafungua mlango
taratibu ili nitoke nje. Nilipofika pale nje niliweza kuwasikia vizuri wale
bundi na hakika walionekana kuwa jirani kabisa na mimi japo nilikuwa siwaoni.
Nikanyanyua ule mwiko kisha nikaubamiza kwenye bati ya nyumba yangu, mara wale
bundi walinyamaza maramoja. Nikabonda mara ya pili nikasikia wakipeperuka na
kwenda kutua kwenye mti fulani uliokuwa jirani na nyumba yetu na ambako
walikuwa wanalala kuku wa Ndeluvale. Huko wakaendelea kupiga kelele kwa
kupokezana kama mwanzo. Nikaamua kuzunguka huko huko kisha nikarusha ule mwiko,
nao wakatoweka hawakusikika tena. Basi nikaanza kurudi na kabla sijaenda
chumbani nkaamua niingie jikoni nione mgonjwa anaendeleaje. Chaajabu
nilipoingia mlangoni nilinusurika kumkanyaga nyoka mkubwa ambaye alikuwa
anatoka mle jikoni. Nilishituka ghafla, nikaingia ndani kwa haraka huku nikiwa
nahema kama mwanariadha. Waliokuwepo mle ndani jikoni walinishangaa hali
niliyokuwa nayo kwa wakati ule. Nikajaribu kuwahadithia jinsi nilivyopishana na
yule nyoka mkubwa mlangoni hawakunielewa, walinibishia wakasema wao walikuwa
macho mle ndani hawakuona hata dalili ya kuwemo nyoka mle jikoni na moto
ulikuwa unawaka na taa ilikuwa inamulika chumba kizima. Nikaamua kunyamaza
maana ni mimi pekeyangu niliyekuwa nimeona sikuwa na shahidi mwingine. Hali ya
mgonjwa kwa wakati ule ilikuwa ya kawaida. Mgonjwa alikuwa mnyonge, amepoa
anahema kwa mbali. Sikutaka nimsumbue sana, nikawaacha wanakesha nikawaaga
nikarudi chumbani kulala. Niliingia chumbani nikafunga mlango kwa ndani
nikajilaza kitandani. Nililala chali macho yangu yakitazama juu aliko muumba.
Baada ya muda nikajikuta katika sala nikimwomba Mungu amponye mwanangu.
Nilisali hivi: Ewe Mungu muumba wa vyote. Wewe wajua kulala kwangu na kuamka
kwangu, wewe wayajua matatizo yanayonikabili mimi mtumishi wako nisiye hata na
thamani machoni pa walimwengu, naomba unipe thamani mbele yako. Ulinijalia
makuu nikashangilia nikasherehekea nikifurahi. Hata hivyo sikukusahau wewe
uliye muweza wa yote. Tazama Bwana, mwanangu Sostenes uliyenijalia wewe
mwenyewe sipo nae tena. Alinitoka nikaomboleza natumaini sasa umempumzisha
mbinguni mahali pa raha. Tazama nimegubikwa na pigo jingine tena Bwana. Mwana
Sabrina yu hoi kitandani. Binti yangu hajiwezi, nimehangaika na bado nahangaika
ili mwanangu apate ahueni niendelee kuweka matumaini yangu kwake. Naomba
umponye mwangu, ili aendelee kuhesabika katika idadi ya wanangu ulionijalia…”
Sala yangu haikuisha huku nikiendelea kusali, usingizi ukanivamia taratibu
kisha ukanikuda roba nikaanza kusinzia. Ghafla nilisikia yowe ya msiba ikitokea
jikoni. Kwa mara ya kwanza nilihisi niko ndotoni labda ninaota yale mazishi ya
mwanangu Sostenes. Ilipopiga mara ya pili na ya tatu niligundua kuwa haikuwa ndoto tena. Niliweza kuisikia sauti
vizuri ikitokea jikoni. Niliposikiliza vizuri niligundua ilikuwa ni sauti ya
Mama Salma na binti yangu Salma. Moyo uliniuma, nikatamani kumlaumu Mungu na
kumwuliza kama nilikuwa nakosea kuomba amponye mwanangu hata akaamua kuichukua
roho yake kabisa. Nilishindwa kuinuka kitandani, nikajikunyata nikalia masikini
mimi, nikanawa machozi uso mzima. Nikajipigapiga masumbwi, nikajiona sifai kitu
duniani hapa nikatamani kama na mimi nijifie niongozane na mwanangu huko
mbinguni alikotangulia.
Zile
yowe zilitosha kabisa kuwaita majirani. Mke wa Mzee Ndeluvale alikuwa wa kwanza
kujumuika nasi kuomboleza kifo cha mwanangu Sabrina. Kwakuwa kulikuwa karibu
kunapambazuka majirani wengi walianza kumiminika pale msibani. Ndugu na
majirani walitaarifiwa juu ya tukio hilo nao wakaja kujumuika nasi. Maandalizi
yalifanyika, watu walikula wakalala, maombolezo yakafanyika. Siku iliyofuata
ilikuwa ni siku ya mazishi ya mwangu Sabrina.
Siku
ilipofika maiti iliandaliwa vizuri, mwili wa mwanangu kipenzi sasa ukafungwa
kama pipi ndani ya sanda na kupangwa ndani ya jeneza dogo lililolingana na
mwili wake. Ukafika muda wa kuaga maiti ya mwanangu. Nikajikaza kisabuni,
nikalisogelea jeneza na kuitazama sura ya mwanangu Sabrina kwa mara ya mwisho.
Machozi yalinitoka, mwili nilihisi umelegea kanakwamba ningehitaji mtu
anishikilie nisidondoke lakini nilijikaza kisabuni nikayahimili maumivu. Wakati
huu wa kumwaga mwanangu, Salma dada wa marehemu alizimia hakuweza kushiriki
kuuaga mwili wa mdogowake. Mama Salma naye kwa
kushikiliwa na wanawake wenzake aliweza kushiriki hatua hii ya kumuaga
mwanae wa pili. Tukio hili lilipokamilika, jeneza lilibebwa na maandamano
kuelekea makaburini yakaanza mara. Tulipofika makaburini, katekista alituongoza
katika sala ya mazishi, kisha mazishi yakaendelea.
Pale mwili wa mwanangu
ulipotumbukizwa ndani ya kaburi nilitamani kama vile na mimi ningeingia ili
twende pamoja huko alikokuwa anaenda, lakini haikuwa rahisi. Machozi ya uchungu
yalinitoka yakachuruzika mashavuni mwangu hadi kudondoka chini. Makamasi nayo
yakaanza kuchungulia puani mwangu kama vile yalitaka kushuhudia mazishi, ila
nikayafuta kwa leso yangu. Nilimlilia mwanangu Sabrina hata nikamkumbuka na
Sostenes mdogo wake Sabrina aliyetangulia kututoka. Nilivyoendelea kutazama
nilitamani kama wale watu waache kufukia lile kaburi wasubiri labda mwanangu
ataamka lakini ndo kwanza walianza kushindilia kaburi kwa nguvu kwa kutumia
miguu. Niliona kanakwamba walikuwa wanafurahia kifo cha mwanangu. Lakini
haikuwa hivyo bali ni taratibu za mazishi yote kushindilia kwa nguvu vile.
Mazishi
yakamalizika, kama kawaida mtangazaji alitangaza kuwa watu wote warudi nyumbani
kwa wafiwa ili wakanawe mikono. Basi
watu wakaanza kurudi nyumbani nami nikaungana nao, nikaanza kuondoka taratibu
huku nikiwa nimeshika leso mkononi nikifuta machozi yaliyokuwa yakinimiminika
mashavuni mwangu. Nilipofika nyumbani nikapitiliza moja kwa moja chumbani na
kujilaza chali kitandani. Mawazo yalinihama kabisa. Hakuna kingine
nilichokifikiria zaidi ya mwanangu Sabrina, tena mawazo haya yakanipelekea
kumuwaza mwanangu Sostenes alikuwa ameanza kusahaulika moyoni mwangu. Baadaye
nilihisi kusinzia usingizi ukanichukua kwa muda nikalala. Nikaanza kuota ndoto
mchana ule pale kitandani nikiwa nimejilaza chali. Niliposhituka niliweza
kukumbuka kuwa katika ndoto yangu, kulikuwa na mtu mmoja ambaye namfahamu
kabisa, alikuja nyumbani kumwulizia mwanangu Sostenes nikamwambia alishafariki,
akaniuliza Sabrina yuko nikasema kaenda shuleni, yeye akaniambia kuwa
atakaporudi atakuja kumchukua. Mimi nilipotaka kumwuliza kuwa alitaka kumpeleka
wapi sauti haikunitoka, yeye akaanza kuondoka, nikataka nimwite asubiri
tuzungumze ila hakuitika wala hakugeuka kunitazama. Nilitamani nisimame nimfate
sikuweza miguu ilikuwa mizito kabisa sikuweza hata kuinuka. Nilivyoendelea
kuita ndivyo alivyozidi kuondoka na kwenda zake.
Niliposhituka
kutoka usingizini niliifikiria sana ndoto yangu ila sikupata jibu. Niliangalia
saa ya mkononi nikakuta ni saa kumi na moja jioni. Nilivyoinua macho mlangoni
nikakuta mlango unafunguliwa. Kumbe alikuwa ni Daudi mdogo wangu akiniita
niende nikale. Basi bila kusita nikainuka nikaongozana naye ili nipoteze mawazo
juu ya wanangu niliokuwa nimwapoteza. Nilikula chakula kisha nikarudi kulala
tena. Nilianza kuhisi upweke wa nafsi kwa kuwapoteza wanangu wawili. Nilikuwa
nimebakiwa na mwanangu mmoja Salma na mama yake tu. Nafsi iliniuma, nilijaribu
kujiuliza na kujihoji kwanini mimi yalinikuta haya. Lakini niliishia kujisemea
`huenda ni mpango wa Mungu tu, nilijifariji kwa kudhani labda alikuwa na mpango
na mimi`. Nililala usingizi mzito siku hiyo sikushiriki kuimba nyimbo za misiba
walizokuwa wanaimba watu usiku ule. Sikujua kama waliimba ule wimbo wa TWIWALALA na kwenda makaburini kama
tulivyomfanyia mwanangu Sostenes. Nililala fofofo nisijue kilichoendelea usiku
ule. Mama Salma naye alilala na wanawake wengine ndungu zetu waliofika
kuomboleza pamoja nasi.
Usiku
ukaisha, kukapambazuka na siku mpya ikawa imeanza. Ndugu wengine walianza
kuondoka na kurudi kwao. Lakini siku ile ya pili baada ya mazishi ya mwanangu
Sabrina ndugu wote tulikusanyika na kufanya kikao cha ukoo. Katika kikao hicho
baadhi ya ndugu walishauri twende tukaague ili tujue ni nini kilichotukumba
hadi tunawapoteza wanetu kiasi kile. Walisema tukatafute huenda kuna mbaya wetu
hatutakii mema. Mimi binafsi sikuwa tayari kukanyaga kwa mganga. Nilikataa
nikasema kuwa haya yote yalikuwa yanatokea kwa mpango wa Mungu. Hatukufikia
mwafaka wa kwenda kwa mganga au kutoenda maana mimi nilikataa kabisa kukanyaga
kwa mganga. Mke wangu hakuwa na la kusema alikuwa akinisikiliza mimi kama
ningekubali kwenda kuagua.
Kikao
kilimalizika ndugu wakatawanyika nasi tukaendelea na maisha tukiomboleza kwa
kuwapoteza wanetu wawili. Sasa Salma alibaki peke yake wa kwenda shuleni na
kurudi kusaidia kazi nyumbani. Bila shaka aliwakumbuka sana wadogo zake, lakini
wasingeweza kurudi tena. Mimi na mke wangu Mama Salma tuliendelea na shughuli
zetu. Baada ya kuomboleza kwa muda mrefu tuliendelea na shughuli zetu za
shambani, kulima na kuvuna.
Mwanetu
pekee aliyesalia, Salma aliendelea na shule. Yeye ndiye aliyebaki kuwa tegemeo
letu pale nyumbani. Tulimpenda sana na tukamtunza kwa umakini na kumpa mahitaji
yote aliyoyataka kadiri ya uwezo wetu. Tulimhamisisha mwanetu akazane kusoma
kwani tulimtegemea kuwa ndiye ambaye angetutunza tutakapokuwa vikongwe nguvu
zitakapotuishia hatuwezi kufanya kazi tena. Tulimpenda sana mwanetu. Nyumbani
kulikuwa kumepoa na kila mtu aliyepita kutusalimia alihisi utulivu kanakwamba
tulikuwa tumehama kumbe bado mimi, mama salma na Salma tulikuwepo.
Katika
maisha yetu hatukusahau kusali sala za pamoja kila jioni na kuwaombea wenzetu
ambao walikuwa wametutangulia kwa mwenyezi wakiwa bado watoto. Tulisali kila
siku jioni tukipeleka shukrani na maombi yetu kwa mwenyezi aliye asili ya kila
lililo jema. Wakati anafariki Sabrina aliyekuwa kidato cha kwanza, huku Salma
alikuwa kidato cha pili. Siku zikazidi kusukumana, zikakimbizana zikaenda mbio
nazo zikamalizika mara tukakuta binti yetu yupo kidato cha nne. Kwa hakika sasa
alikuwa ni binti kweli wa kutazamwa
mara mbili na wavulana aliopishana nao. Kama wazazi tulitambua hilo hivyo
tulikuwa makini mwanetu asiharibikiwe maisha. Tukamfunza siri za maisha na
mbinu za kufanikiwa. Tukampeleka sasa akae bwenini ili atulie ajiandae vizuri
na mitihani.
Miezi
ikayoyoma akakaribia kufanya mtihani wa taifa akiwa mzima na afya safi.
Tukamsihi mwanetu akazane kusoma ajiandae vizuri na mitihani. Ikatangazwa siku
ya mahafali naye akatujulisha, basi tukajipanga tukamshonea nguo nzuri.
Siku ya
mahafali ilipofika mimi na Mama Salma tulienda kumshangilia na kumpigia nderemo
mwanetu. Tulimbebea zawadi kedekede na mazaga ya kutosha. Tulipiga na picha za
ukumbusho huku tukiwa tumemvalisha mataji
mengi yamemjaa shingoni. Tulikula tukampa zawadi nyingi sana. Tukamsihi
sana ajiandae vizuri na mtihani wa Taifa.
Hatimaye
siku ikafika mwanetu akaingia kwenye chumba cha mtihani.
Aliyazingatia
tuliyokuwa tumemfunza akafanya mtihani wake kwa utulivu, hata mitihani yote
ikaisha na akarudi nyumbani kama mhitimu. Tulimpokea kwa furaha na bashasha
tukamchinjia na jogoo ale ajinome mwanetu kipenzi.
~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
SURA YA TATU
Shamrashamra
za mahafali ya mwanetu kipenzi zililipomalizika tukaendelea kuishi pamoja
nyumbani na yeye akishiriki kazi za shambani, kwani alikuwa anaweza kufanya
shughuli hizo na ndizo shughuli pekee zilizotuingizia kipato ndani ya nyumba.
Mwaka ule mwezi ule wa kumi alipokuwa ametoka tu kuhitimu kidato cha nne
tulikuwa tunafanya kazi ya kuandaa mashamba ya kulima mwaka ule. Tulikuwa
tumeandaa mashamba mawili makubwa ya viazi na yakakamilika tukapanda kisha
tukaanza kuandaa mashamba ya kulima ili tupande mahindi. Hili shamba tulianza
kulifyeka mapema kwani lilikuwa ni shamba jipya na ni mara ya kwanza kulilima.
Tulifyeka tukamaliza ndani ya wiki mbili. Baada ya nyasi kukauka tukachoma moto
kisha tukaanza kulima. Tukalima kwa juhudi sana. Tulikuwa tunajihimu mapema
asubuhi huku tukijifungasha kande au viazi vitamu kwenye kikapu vya kula
shambani. Tulirudi jioni sana tukiwa tumechoka. Nilikuwa nikimtazama mwanangu
akiwa mchovu namwonea huruma lakini hakukuwa na namna maana ilitupasa kufanya
hivyo ili siku ziende na familia yetu isiwe ombaomba. Baada ya wiki tatu
tulimaliza kazi ya kulima shamba hilo. Tulipomaliza kulima shamba hilo tuliamua
kupumzika siku tatu mfululizo bila kufanya kazi yoyote ya shamba.
Baadaye
tuliamua kuanza kuandaa shamba jingine ambalo mwaka wa nyuma yake tulikuwa
tumelima mahindi hivyo kulikuwa na mabuwa ya kufyeka na kuchoma moto kisha
kulima.
Sasa ilikuwa ni mwezi wa kumi
na moja. Tulifyeka kwa muda wa wiki moja na ile sehemu iliyobaki ilikuwa ya
kumalizia kwa siku moja. Siku hiyo tulijihimu kama tulivyozoea kujihimu
tulipokuwa tunalima shamba lile la kwanza ambalo lilikuwa jipya. Siku ile
tulijihimu tukabeba mayao kama
chakula chetu cha mchana kwenye kikapu. Tulipofika tukakiweka pembeni ya shamba
chini ya mti uliokuwa na kivuli kizuri. Kisha kila mmoja akashika jembe lake na
kazi ikaendelea. Zilipita dakika chache, haikufika hata saa moja, mara Salma
alikurupuka kwa mshituko akatupia jembe pembeni huko akaanza kukimbia kimbia
huku akiita `mamaaa mamaaaa`. Akarukaruka kisha akaanza kukimbia kuelekea
alikokuwa mama yake. Mimi kwa mshangao na kwa kuhamaki nikamwambia Mama Salma
`Mwangalie mtoto huyo kuna nini`. Salma alipofika kwa mama yake akajitupa chini
na kuendelea kulia kwa sauti bila kusema shida ilikuwa nini. Alilia akigaagaa
na kujitupatupa maskini binti yangu Salma.Tukajaribu kumshika lakini
alifurukuta kiasi cha kutushinda nguvu mimi na Mama yake..........................
KALIA KIGODA MWANAKWETU WEYE, MAMBO BADO!!!!!!!!!!!!!!!!!!
^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^



Asante Mungu kwa kunijalia haya yote. Aminia
ReplyDeleteNimeipenda hakika
ReplyDelete