Saturday, 28 January 2017

KUMBE JIRANI YANGU MCHAWI: MTUNZI: ELIAS K. MWALONGO(KANTON)



KUMBE JIRANI YANGU

MCHAWI






Mtunzi:
Elias K. Mwalongo






~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
KUMBE JIRANI YANGU MCHAWI
@Copyright by: Elias K. Mwalongo
S. L. P 977 Njombe
Simu: +255769313224
Facebook: Elias Mwalongo
Twitter: Elias Mwalongo
Instagram: @mwalongoelias








Chapa Ya Kwanza, Januari, 1, 2017


Haki zote zimehifadhiwa. Huruhusiwi kuiga, kupiga chapa, kutafsiri au kukitoa kitabu hiki kwa jinsi yoyote ile pasipo idhini ya mwandishi wa kitabu hiki au mhariri mhariri wake. Hatua za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika.


            ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~
SURA YA KWANZA
Tangu siku ile sijawahi kabisa kupata lepe la usingizi. Nimekuwa mtu wa shuruba na kujiinamia chini nisijue nini nifanye.Nikijaribu kulala chali nitazame juu ambako naamini ndiko aliko mwenyezi sipati nafuu, nikilala kiubavu nitazame pembeni huko nayo nagundua kuwa haisaidii, nikijaribu kulala kifudifudi nifumbe na macho nisikumbuke yote yaliyonisibu maishani na kunifikisha hapa kifungoni, bado nagundua kuwa ni kazi bure. Nikiamua kuamka na kujiketisha chini niegame ukutani huku nikijiinamia. Nafurukuta nawayawaya natamani kama nijifinye au nijipige teke. Mapigo ya moyo yanaenda kwa kasi yanapiga kama saa ya ukutani pwi-pwi-pwi. Makamasi yananifura kama mbeta ya ulanzi wa masika. Machozi yananitiririka mashavuni mwangu hadi chini yanatua huku yakilowanisha shati langu. Moyo umekufa ganzi hata nahisi kama vile unataka kumrudia aliyeuumba na mwili wangu huu kushuka mavumbini ulikotoka.
Nahangaika masikini Elias mimi kupoteza mawazo juu ya mazishi ya mwanangu Sabrina, binti yangu mdogo, wa pili kuzaliwa. Binti yangu mashuhuri aliyenifanya nijivune hapa kijijini na kuonekana wa maana. Mazishi ya binti yangu yananirudisha mbali nilikotoka na mikasa ya maisha iliyonikumba. Masikini mimi ninakumbuka kifo cha Salma dada yake Sabrina, narudi nyuma tena namkumbuka marehemu mwanangu Sostenes mdogo wao wa mwisho niliyempoteza angali mdogo kabisa. Tena ninakumbuka sana siku ile nilipotupa udongo kwenye kaburi la mke wangu kipenzi Salome, binti wa kipangwa niliyempata kwa shida nikalipa na mahali ya mafahali mawili kisha nikamuweka ndani awe mama wa wanangu, naye nilimpoteza angali kijana kabisa akaongozana na binti yake mkubwa Salma wakaniacha nafurukuta nalia na moyo wangu. Najaribu kufurukuta nisikumbuke ndo kwanza picha ya matukio hayo inanijia vizuri kabisa. Uvumilivu unanikabili na kunishinda nguvu, wacha nichukue kalamu yangu niwaandikie walau mjifunze kitu ili siku yatakapowakuta na nyinyi msihukumiwe kifungo cha maisha na kusota kifungoni huku kama mimi.
Ninakumbuka vishindo vya siku ile nikiwa kitandani usiku wa manane nimepumzika na mke wangu mpendwa. Vishindo vilivyosikika kuanzia kwenye dirisha la chumba changu vikazunguka nyumba yangu hadi upande wa pili kwenye chumba cha wanangu. Kwa hofu nikamwamsha mke wangu aliyekuwa amelala fofofo asikilize na yeye vishindo hivyo. Jinsi nilivyomwamusha ndivyo vishindo vilivyozidi kusikika kwa nguvu vikisogea tena jirani na dirisha la chumba chetu. Mwili ulitetemeka, kijasho chembamba kikanimiminika, na nywele zikanisimama. Mimi na na Mama Salma tukapiga moyo konde, yote tukamwachia mwenyezi maana yeye ndiye mpaji na mnyimaji. Vishindo vikaishia dirishani kwetu vilikoanzia na ghafla vikatoweka, kukawa kimya kabisa. Nilijaribu kufikiria ni nini kilikuwa kinatokea lakini sikupata jibu. Tulibaki tumedhoofika kwa hofu na mashaka. Tulijaribu kulala lakini haikuwezekana kwani hatukupata usingizi kabisa. Nilijaribu kuwasha tochi ya simu yangu, nikamulika kuanzia kwenye mlango wa chumba chetu sikuona kitu chochote, nikamulika kwa kona ya chumba chetu nikamwona mende mmoja tu akipotelea kwa sanduku la nguo la Mama Salma, nilimulika chumba kizima sikuona cha pekee, basi nikaizima tochi yangu. Baadae tulianza kunong`ona kwa sauti ya chini sauti iliyokuwa imejaa hofu na mashaka makubwa. Baadaye tulikaa kimya kwa kitambo kirefu. Macho yangu yalianza kuwa mazito, usingizizi ukaanza kuninyemelea kwa mbali. Ghafla nikaamshwa na jogoo wa Ndeluvale aliyewika kwa sauti kubwa. Ndeluvale yule jirani yangu mhunzi na fundi wa kutengeneza mikeka, na vikapu. Alikuwa na kuku wengi sana na walikuwa wakilala juu ya mti uliokuwa unapakana kati ya nyumba yangu na yake. Yule jogoo alipowika nikashtuka toka usingizini. Nikachukua simu yanu ya Tecno, nikaiwasha ili nitazame muda. Ilikuwa sa kumi na moja na dakika ishirini na tatu alfajiri. Kule kusinzia kulinisahaulisha vituko vilivyotokea usiku wa manane, sasa nikawa macho na taratibu kumbukumbu zikaanza kunirudia, nikakumbuka vizuri mimi na Mama Salma tulivyohangaika usiku kwa hofu na mioyo kutupwitapwita. Nikageuka kumtazama Mama Salma aliyekuwa amelala pembeni yangu, giza lilinizuia sikuweza kumtazama vizuri, nikataka niwashe tochi ya simu yangu ila nikaamua kuacha kwani kwa mbali nilikuwa namsikia akikoroma. Niliendelea kutafakari huku nimejiegesha kitandani nisione dalili ya kupata usingizi tena. Baada ya dakika chache nilianza kuhisi mwanga ukiongezeka mle  chumbani tokea dirishani, kumbe kulikuwa kunaelekea kupambazuka. Haikupita kitambo kikubwa Mama Salma naye akavuta pumzi ndefu kisha akageuka alale vizuri basi nikamwamsha kwani muda nao ulikuwa umetokomea. Akanitazama kwa mbali kwa kutumia mwanga ule ulioanza kupenyeza dirishani alfajiri ile. Baada ya muda nikaanza kumkumbusha kuhusu tukio la usiku lililotuogofya. Tulijaribu kuulizana ni nini kilichotutisha usiku lakini hakuna aliyeweza kugundua. Basi tukaamua kupotezea.
Niliamka nikatoka chumbani kwangu nikaanza kutoka taratibu kuelekea sebuleni. Kabla sijafika mlango wa kutokea nje nikashitushwa na kelele za mlango uliobamizwa chumbani kwa wanangu. Nikageuka haraka, masalale! Kumbe alikuwa ni Salma binti yangu wa kwanza. Nikamwuliza kulikoni mwanangu? Akajibu, baba Sostenesi anaumwa. Nikarudi haraka chumbani kumwita Mama Salma, ili aende akaangalie watoto. Akakurupuka haraka alijifunga kanga kiunoni, akavaa ndala zake na kukimbia hadi chumbani kwa Salma na wadogo zake. Alipofika alimkuta Sostenes akiwa amejilaza kitandani kwake, kitanda kilichokuwa pembeni mwa kitanda walichokuwa wanalalia dada zake Salma na Sabrina. Akamwuliza anaumwa nini, yeye katika umri wake mdogo hakuweza kueleza akasema tu kuwa hajisikii vizuri na mwili mzima ulikuwa unauma. Walijitahidi kumshawishi asimame lakini hakuweza kuhimili peke yake alihitaji kushikiliwa. Alikuwa amenyong`onyea hawezi kusimama peke yake. Basi tukahangaika masikini sisi tukampeleka dispensari yetu ya kata kwa pikipiki. Tulipofika tulipokelewa vizuri na manesi wawili. Tukawakabidhi mgonjwa wetu nasi tukaketi kwenye veranda kwanye benchi tukisubiri kuambimbwa mwanetu alikuwa anaumwa nini hasa.
Kule nyumbani Salma na Sabrina walikuwa wameenda shuleni. Tukaendelea kunong`ona pale nje mimi na mke wangu Salome. Mara mlango ulifunguliwa na nesi mmoja akatoka akatuambia kuwa mgonjwa wetu alikuwa anazidiwa na vipimo walivyokuwa navyo haviwezi kusaidia kujua tatizo la mgonjwa wetu, hivyo walitushauri tumpeleke hospitari ya wilaya ili tukasaidiwe huko. Maskini sisi, kipatochetu chenyewe ni duni. Basi tukachukua akiba yetu ya pesa tukaanza safari kuelekea hospitari ya wilaya ya kipindi hicho ambayo sasa ni hospitari ya mkoa wa Njombe. Tukiwa kwenye gari kuelekea hospitarini mwanetu Sostenes alitukatisha matumaini. Nilimwangalia mwanangu, nikaona mwanangu macho yamemtoka pima, mdomo wake mdogo na mwembamba ulikuwa umelegea na uko wazi, mapigo ya moyo yalipiga taratibu kama saa ya ukutani ambayo betri imeisha nguvu yake.    Macho ya mwanangu yalinitazama mimi bila kukonyeza mithiri ya mtu anayetaka kumaanisha kitu. Nikahisi kama vile mwanangu anataka kumaanisha `kwaheri`. Nilitamani hata nijipige teke nikome kufikilia kuwa mwanangu ananiaga lakini ndivyo ilivyokuwa. Niliendelea kumkodolea macho mwanangu kama yeye alivyonikodolea bila kukonyeza, lakini tulivyoendelea kutazamana vile mara nikaona macho yake yakazidi kusinyaa na kuwa madogo hadi yakafumba. Masalale! Moyo ulinidunda kwa nguvu na kwa woga. Nikamtikisa mwanangu alikuwa amelegea yuko hoi hana hali. Nikajaribu kusikiliza mwendo wa mapigo ya moyo kama ni ya haraka au taratibu, chaajabu niliishia kusikiliza mapigo ya moyo wangu mwenyewe. Kumbe sasa nilikuwa sijampakata mwanangu bali maiti ya mwanangu. Machozi yalianza kunitiririka mashavuni. Mama Salma sasa ilikuwa ni kilio na yowe. Tulihuzunika sisi tukalia na kuomboleza juu ya mwanetu aliyetutoka hali hatujui alikuwa anasumbuliwa na tatizo gani. Basi tuligeza gari na kuanza kurudi nyumbani. Sasa safari yetu ilikuwa ni ya kusafirisha maiti kupeleka nyumbani badala ya kusafirisha mgonjwa kwenda hospitari.
Tulifika kijijini kwetu mida ya jioni sana, tukakuta maandalizi ya msiba yanaendelea kufanyika kwani tuliwataarifu ndugu na jamaa kwamba mwanetu kipenzi ametutoka. Nasi tulipofika tulikuta ndugu wengine wakiwa wanalia kwa uchungu mkubwa, uchungu wenye masikitiko ya kumpoteza mwanetu kipenzi, mwanetu pekee wa kiume, mrithi wetu na tumaini la familia yetu. Msiba ulipokelewa maiti ikawekwa kwenye chumba maalumu nasi wafiwa tukaingia humo kuomboleza. Maandalizi yaliendelea, ndugu jamaa na majirani walifika kwenye msiba tukaomboleza pamoja. Moto ulikokwa nje uwanjani, watu walipika vyakula, michango mingi ilitolewa nao majirani kwa mioyo minyofu waliomboleza pamoja nasi usiku mzima hadi asubuhi. Siku hii ya pili ilikuwa ni siku ya mazishi ya mwanangu Sostenes. Ilikuwa ni siku ya mwisho ya kuona sura ya mwanangu. Ilinipasa nianze kusahau tabasamu lake, kicheko chake na upole wake uliojionyesha hata kwa mwonekano wa sura yake.
Maandalizi yalikamilika, mwanangu Sostenes akafungwa kama pipi kwenye sanda, akadumbukizwa kwenye jeneza dogo la saizi yake. Ilipofika saa nane mchana, jeneza likawekwa nje uwanjani, mwenyekiti wa msiba ule Mzee Ndeluvale ambaye alikuwa jirani yangu akatangaza kuwa maiti itaanza kuangwa tukianzia sisi wazazi wa marehemu, dada zake na ndugu wengine watafata hadi jamaa wote waishe. Agizo hilo lilifuatwa. Mimi nikawa wa kwanza kujongea mbele ya jeneza kuitazama sura ya mwanangu kwa mara ya mwisho. Nilisogea kwa ujasiri lakini ujasiri ukaniisha, chozi likanishuka. Nikachukua leso yangu mfukoni nikaanza kufuta machozi yaliyokuwa yakinititika mashavuni mwangu nikimlilia mwanangu. Mama yake ndo kabisa hakuweza kustahimili maumivu, aliishiwa nguvu asiweze hata kusimama peke yake alishikiliwa na ndugu wengine wakamkokota taratibu amtazame mwanae kwa mara ya mwisho. Sabrina. Dada yake mdogo wa marehemu Sostenes naye alilia kwa uchungu mkubwa, watu wakamshikilia upande kwa upande na kumsogeza jirani na jeneza la Sostenes mdogo wake. Huku akilia kwa kwikwi aliiangalia sura ya mdogo wake kwa mara ya mwisho kisha akapelekwa pembeni. Ndugu wengine wa marehemu nao wakapita kuuaga mwili wa ndugu yao Sostenes kisha majirani na wageni wote walifika kujumuika nasi wakapita kumwaga mwanangu kipenzi aliyekuwa amenitoka angali mtoto. Wakati zoezi hili likiendelea, Salma dada wa marehemu Sostenes aliyekuwa pembeni akadondoka ghafla na kupoteza fahamu. Watu wakambeba wakamweka kwenye kivuli wakampepea kwa muda mrefu lakini haikusaidia, akapelekwa hospitalini ambako alilazwa akahudumiwa vizuri na wauguzi.
Wakati ukafika wa kwenda makaburini kumzika mwanagu Sostenes. Sikuamini yaliyokuwa yakitokea siku ile. Niliona kama vile ni ndoto ninayoiota alasiri ile, lakini ulikuwa ndo ukweli wenyewe. Watu wakalibeba lile jeneza lililokuwa na mwili wa mwanangu huku wakipokezana baada ya kila kitambo kidogo.
Hatimaye wakafika nalo makaburini, wakaliweka jeneza pembeni mwa kaburi lililokuwa limeshaandaliwa. Katekista aliongoza sala ya mazishi, kisha zoezi la kumzika mwanangu likafuata. Jeneza liliingizwa kaburini taratibu hadi likatua kwenye sakafu ya kaburi lile. Wakachota mchanga na kuniletea ili mimi niwe wa kwanza kutupa mchanga kaburini japo kiganja kimoja. Nikasisimuka mwili, taratibu nikachota ule mchanga nikaumimina taratibu kwenye kaburi la mwanangu Sostenes. Jinsi nilivyozidi kumimina ule mchanga ndivyo na machozi yalivyozidi kunitiririka na mengine kumiminika hadi ndani ya kaburi la mwanangu. Nilipomaliza nikaondoka taratibu ili kumpisha mke wangu naye amzike mwanaye. Haikuwa rahishi Mama salima kuchukua kiganja cha mchanga na kumimina kwenye kaburi la mwanae, basi wanawake Fulani walimshikilia na kumsaidia hadi akatupa mchanga ndani ya kaburi la mwanae. Akafuata Sabrina japo naye kwa kushikiliwa. Ndugu wengine wakafuata na baadaye wengine wakalishambulia kaburi la mwanangu kwa kutupia mchanga kwa kutumia spedi na kushindilia kwa visigino vyao. Mimi nikiwa nimesimama pembeni niliwaza moyoni mwangu, nikajaribu kukumbuka mwanangu, machozi yakaanza kutoka tena. Kaburi lilipojaa wakaanza kushindilia kwa mikono. Mama Salma, mama wa marehemu alilia kwa nguvu hadi nikamwonea huruma japo mimi mwenyewe nilishikwa na uchungu sana kumpoteza mwanangu.
Kisha tukaweka mataji kwenye kaburi la mwanangu, nilianza mimi akafata mama yake akafuata Sabrina dada yake na kisha wajomba, binamu, shangazi na ndugu wengine wakafuata. Mazishi yalipomalizika mtangazaji, mzee Ndeluvale akatangaza kuwa watu warudi nyumbani kwa wafiwa wakanawe mikono, akimaanisha wakale chakula. Basi watu wakaanza kurudi, mimi nilikawia kidogo, nilitamani kama nibaki kaburini lakini ilinilazimu niondoke.
Tulipofika nyumbani chakula kilikuwa kimeandaliwa, watu wakala wakashiba na kusaza. Mimi sikuweza kula mchana ule. Nilianza kufatilia kujua hali ya binti yangu Salma aliyekuwa amepoteza fahamu wakati wa kwenda kuaga maiti ya mdogo wake. Hali ya binti yangu ilikuwa shwari, nikatiwa matumaini.
Usiku watu waliobaki kukesha na kuomboleza pamoja nasi, walikuwa wakiimba nyimbo za aina nyingi. Baadhi ya nyimbo hizo nilikuwa nazifahamu na nyingine zilikuwa ngeni kabisa kwangu. Nyimbo nilizokuwa nazifahamu ni kama vile ule unaoitwa Twiwalala:
Uliimbwa hivi:
Moooja, mbili tatu twende twiwalala, (We twiwalala) x 2
Ve twiwalala umwanavesu(We twiwalala)
Umwana vesu asivoneha (We twiwalala)
Umwana vesu ahele hwina (We twiwalala)
Moooja, mbili tatu twende twiwalala, (We twiwalala) x 2
Pia waliimba ule wimbo wa “Parapanda italia,” pia na nyimbo nyingine nyingi zilizomtaja na marehemu mwanangu. Tulifarijika kwani watu waliguswa na kifo cha mwanetu hata wakashiriki nasi katika tukio hilo. Uliipoimbwa wimbo wa `twiwalala` sikusita kusimama na mimi kuimba. Kwa kawaida wimbo huu unapoimbwa kwenye msiba watu huanza kucheza kwa kuruka na kuzungukazunguka wakipapasapasa kama vile wanatafuta kitu kilichopotea na kwa wakati ule hakika ulikuwa ni wakati wa kumtafuta mwanangu Sostenes. Hivyo nilijumuika nao kupapasa kumtafuta mwanangu.
Tulicheza tukaruka tukiimba huku tukipiga yowe, huuuuwi, huuuuwi! Mara tukaanza kuondoka kuelekea makaburini. Akina mama fulani waliokuwa wanaimbisha walitangulia mbele, mimi nilikuwa katikati ya watu wengine, nami nilikuwa nikiimba kwa sauti kwani wimbo ule nilikuwa naufahamu vizuri na nilikuwa naupenda. Tukashuka ule mteremko mara tukakata kona, tukapitiliza vile vichaka vilivyo jirani na makaburi hatimaye tukaingia eneo la makaburini usiku ule huku tukiimba kwa sauti na kupiga yowe. Hapo sasa na mimi nikaharakisha nikawa mbele jirani na wale akina mama waliokuwa wanaimbisha. Kwa mbali niliweza kuona eneo ambalo tulimzika mwanangu. Tulivyozidi kusogea kwa mbali niliona kama kitu cheusi mfano wa kifurushi kikitoweka kutoka pale lilipo kaburi la mwanangu. Nilishituka ghafla nywele zikasimama, mapigo ya moyo yalienda kwa kasi, moyo ukadunda duf-duf-duf kijasho chembamba kikaanza kunitoka. 

 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

SURA YA PILI

Nilijaribu kuwatazama wale wanawake nilikuta wala hawashituki kana kwamba hawajaona chochote, waliendelea kuimba kwa sauti na kupiga mayowe. Wala hakuna hata mtu mmoja aliyeonyesha kushangaa kile nilichokuwa nimekiona mimi. Nikajua ni mimi tu niliyekuwa nimeona na pengine nilitazama vibaya. Hivyo na mimi nikapotezea, nikaendelea kucheza na kuimba kama wengine kanakwamba na mimi sikuona kitu chochote cha kushangaza.
Tuliimba tukaruka na kucheza kuzunguka kaburi la mwanangu Sostenes, tulipiga mayowe. Mimi machozi yakanibubujika nilipomkumbuka mwanangu kipenzi, lakini nikapiga moyo konde. Baada ya kuzunguka lile kaburi mara dufu kisha tukaanza kurudi tunaimba nyumbani. Tulipoondoka kutokana na ukimya tuliouacha watu wengine walikuwa wameshalala, na sisi tulipowasili tulikuwa tumechoka na muda umeyoyoma, wengi wetu tukaenda kulala.
Mazungumzo ya watu waliokuwa wanaota moto nje yalinishitusha kutoka usingizini. Nilipojifunua blanketi usoni nikakutana na mwanga mkali wa asubuhi ile ambao ulikuwa umetanda mle chumbani. Nikatazama saa yangu kumbe ilikuwa ni saa kumi na mbili na nusu asubuhi. Nikaamka nikajiandaa ili nitoke nje. Nilipofungua mlango tu, nilikutana uso kwa uso na Ndeluvale jirani yangu, alikuwa akitabasamu kama vile alikuwa amefurahishwa na mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea pale nje huku wakiota moto. Lakini cha ajabu aliponiona tu, midomo yake iliyofunguka huku meno yakiwa nje nje na macho yakionyesha kuwa ni mwenye furaha ghafla vyote vilisinyaa, akafunga mdomo, meno hayakuonekana, macho yalionyesha ni mwenye aibu kama vile mtu ambaye amekosea jambo. Mimi sikujali, nikatoka pale nje nikawasalimia wote mikononi kwa upole tu nao wakapokea salamu yangu wakiambatanisha na pole kwa msiba. Nikajumuika nao kuota moto na kuendelea kusikiliza mazungumzo yao. Kufikia mida ya mchana watu wengi walikuwa wameshatawanyika wamerudi kwao kuendelea na shughuli zao za kila siku. Na ilipofika jioni wageni waliohitaji kulala ni baadhi tu ya ndugu zetu mana wengine walikuwa wameondoka na kurudi kwao. Nao ndugu zetu wachache waliokuwa wamekesha pamoja nasi na wakalala waliondoka asubuhi na kwenda kwao. Nikabaki mimi, mke wangu Salome na binti zetu wawili Salma na Sabrina baada ya kumpoteza mwanetu Sostenes mwanetu wa mwisho. Tukaendelea na shughuli zetu za kila siku huku tukilima na kuvuna na wanetu wakiendelea na shule.
Baada ya miezi kadhaa, mimi na mama Salma tulikuwa tumeshaanza kulisahau kabisa tukio la kumpoteza mwanetu Sostenes. Tukaendelea kuganga na maisha huku tukiwasomesha wanetu wawili waliokuwa wamesalia. Tuliendelea kulima mahindi, maharage, viazi, njegere na ngano. Tulilima kwa juhudi huku tukivuna na kuuza ili tupate mapesa ya kuwasomeshea wanetu Salma na Sabrina na kupata chochote kitu ndani ya nyumba.
Mwaka ule hakika tulijaliwa kupata mavuno ya kucheba. Tulilima mahindi, maharage na ngano vyote vikastawi vizuri vikanawili na kushona mashamba yetu. Ilipofika kiangazi muda wa kuvuna ilikuwa inatulazimu kurudi nyumbani kwa kuchelewa sana muda ukiwa umeenda, jua limezama na wakati mwingine tulikuwa tunarudi nyumbani usiku hata jua limeshajiendea kwao. Tulikuwa tukirudi nyumbani tunakuta wanetu wamesharudi toka shuleni wamefanya usafi pale nyumbani, nje na ndani kama tulivyowafundisha. Muda mwingine tulikuwa tukichelewa zaidi tunakuta wameshapika na chakula wanajisomea huku wanatusubiri tufike tule pamoja.
Siku hii ilikuwa tofauti kabisa. Siku hii ndio niliyotamani kugaagaa chini, nilitamani nilie huku nikitupatupa miguu kama mtoto mdogo anayelilia kunyonya au aliyenyang`anwa mdoli aliokuwa akiuchezea. Nilipiga moyo konde lakini wapi. Ilikuwa ni siku ile nimejitokea shambani na mke wangu, tulipokaribia kufika nyumbani kwa mbali tuliona watoto wa shule wakiwa wamejaa nje ya nyumba yetu. Tulijua labda wamekuja tu kuwatembelea rafiki zao maana wanetu walipendwa sana shuleni kwao kwa tabia zao nzuri walijipatia marafiki tele ambao mara nyingi walikuwa wanawatembelea hasa siku za Jumapili. Lakini siku hii ilikuwa ni Jumatano, tena muda ulikuwa umeshaenda giza ndo linanyemelea na wote walikuwa bado wamevaa sare za shule kanakwamba ndo wapo shuleni kumbe ni nyumbani kwangu. Nilijiuliza maswali mengi lakini sikupata jibu la haraka. Basi tukasogea kwa haraka ili kujua kilichokuwa kinaendelea. Tuliposogea jirani zaidi tukagundua wale watoto walikuwa na nyuso za huzuni, basi nikatupia huko ukuni ambao nilikuwa nimeubeba begani mwangu nikatangulia mbio nikimwacha mama Salma nyuma. Nikakuta wale watoto wamezunguka duara. Bila kusalimia wala kuhoji chochote nikapitiliza moja kwa moja kuchungulia nini kilikuwa katikati ya lile duara walilolitengeneza. Masalale! Nikakuta binti mmoja amempakata mwanangu Sabrina. Sabrina mwanangu alikuwa amelegea, amenyong`onyea yuko hoi bin taabani, anapumua kwa mbali hana hali binti yangu kipenzi. Nilihangaika mimi, niliingia ndani mara natoka hata nisijue nifanye nini. Nilihisi kuchanganyikiwa na akili kuniruka. Mama Salma akabaki analia pale nje mbele ya watoto wa shule, Salma nae ndo kwanza alikuwa Amelia hadi macho yamekuwa mekundu akabaki sasa analia kwa kwikwi asiweze kusema lolote. Kwa ujasiri nikamwuliza binti mmoja aliyeitwa Eliza, binti wa Mtendaji wa kijiji chetu alifahamika kwa jina la Ngomiposo, ambaye nilimfahamu kuwa ni rafiki wa karibu sana wa Sabrina ili anisimulie kilichomkuta binti yangu. Eliza hakusita akanieleza kwa uwazi na kwa makini akasema, “Sabrina aliniambia mchana kuwa kichwa kilikuwa kinamsumbua, tukajua labda ni jua lile kali la mchana lilikuwa linamdhuru, lakini baadaye akasema anahisi kizunguzungu na muda si mrefu akadondoka na kupoteza fahamu. Kwakuwa ulikuwa umefika muda wa kurudi nyumbani kuna mwalimu alisema tumbebe tumlete nyumbani. Tumekuja tunapokezana hadi tumefika hapa na tulipokuwa njiani alionyesha dalili za kutaka kuzinduka lakini alipozinduka ndio tukakuta amebaki amenyong`onyea amelegea hadi huruma jamani rafiki yetu. Tukajaribu kumuuliza nini kinamuuma japo kwa shida akasema mwili mzima unauma na wala hana nguvu. Tulipofika tulitaka tumpe chochote ale amekataa, hata maji ya kunywa nayo amekataa. Ndio maana tukaona ngoja tuwasubiri hapa hadi wazazi mrudi maana tusingemwacha peke yake.”
Niliwashukuru wale watoto kisha nikawasihi warudi nyumnani wasije wakaanza kutafutwa nasi tutamshughulikia Sabrina.  Wakaondoka kwa upole kanakwamba walitamani kuendelea kushuhudia hali ya rafiki yao. Wale watoto walipoondoka jioni ileile tulimpeleka mgonjwa kwenye dispensari ya kijiji lakini tuliambiwa kuwa mgonjwa amezidiwa na hawangeweza  kutusaidia hivyo wakatushauli tumpeleke hospitali ya wilaya. Kule kwenye hospitari ya wilaya ya kipindi hicho ambayo kwa sasa ndio imepewa hadhi ya kuwa hospitali ya mkoa walitupokea wakamfanyia vipimo mgonjwa wetu lakini wakasema hawakugundua tatizo lolote. Na hali ya mgonjwa iilikuwa ni dhaifu, alilegea mwili mzima hakuweza kusimama wala kutembea peke yake, alilalamika kuwa mwili wote unauma, miguu ilikuwa inauma na kuvimba na pumzi ilikuwa inambana. Kwa hali hii Daktari aliponiambia kuwa hawakugundua tatizo lolote niliishiwa pozi. Pale hospitali walitushauri tumpeleke hospitali ya rufaa.Tulikubali ushauri wao lakini mimi mawazo yalinihama, nilianza kumuwaza na kukumbuka mazishi ya mwanangu Sostenes. Nilimtazama mwangu Sabrina usoni, kisha machozi yakanitoka yakatiririka mashavuni mwangu kama mto ruhuji.
Jioni ile tulirudi nyumbani  na mgonjwa wetu. Baadhi ya ndugu na majirani walitushauri tuondoke naye jioni ile kwenda hospitali kubwa, nasi tulikubali kufanya hivyo lakini jioni ile pale nyumbani kulikuwa na rafiki yangu mmoja wa karibu sana aliyefahamika kwa jina la Shomeho. Aliniita pembeni akanishauri akisema, “inabidi mwende mkatembee”. Nilimtazama usoni kwani sikumwelewa alitaka kumaanisha nini. Ile kumtazama tu aligundua kuwa sikumwelewa, akaendelea, “ndio, mtazunguka hospitali zote watawaambia hawaoni tatizo, kwahiyo cha msingi hapa ni mguu kwa mguu kwa mganga wa kienyeji, atawasaidieni”. Alipotaja tu neno “mganga wa kienyeji” nikamtazama kwa ukali. Nikamwambia, “Shomeho kama huna cha kusema naomba ushone domo lako unyamaze, sio kunitajia mimi habari za mganga wa kienyeji. Mimi ni Mkristo tena mkatoriki na ni mtu mzima na ninajivunia utu uzima wangu. Eti nimuudhi muumba wangu ninayemwabudu kwa kuwafuata waganga. Mwee, nimalize pesa zangu kisa kumpa mganga wa kienyeji, anivalishe hirizi kiunoni na shingoni. Shomeho usinitie uchuro na ubaladhuri. Loo! Mguu huu haukanyagi kwa mganga ng`oo, yote namwachia Mungu.” Shomeho alitikisa kichwa akasema, “sawa ndugu yangu mimi nilikuwa nakushauri tu, naomba uniwie radhi kwa domo langu chafu, lakini `asiyesikia la mkuu huvunjika guu, mimi ndio rafiki yako na vilevile ni kaka yako nilikutangulia kuliona jua rafiki yangu, usinibeze`”. Nikasema `sawa ndugu yangu usiku mwema.`
Niliporudi ndani, mke wangu alinigundua kuwa nilikuwa nimefura hasira, akaniuliza, “kulikoni baba Salma mbona uko hivyo”. Nikamwambia, “mke wangu, we acha tu, watu wanatuchezea hapa kijijini. Mtu mzima na busara zake badala ya kutushauri tumtibu mwanetu eti anatushauri twende kwa mganga, mke wangu, umewahi kukanyaga kwa mganga wewe? Kama ni matatizo tayari tunayo kwanini kwenda kutafuta mengine huko?” Mke wangu akasema, “kwahiyo umemjibu nini mume wangu?” Nikamwambia, “katu mguu huu haukanyagi kwa mganga. Nimemwacha aende zake” Mke wangu aliniangalia kama vile alikuwa na neno la kusema, lakini akaishia kuguna kwa sauti ya chini, akamtazama Sabrina aliyekuwa amelala pale sebuleni, akiwa mgonjwa hajiwezi na sisi bado hatujui kilichomsibu mwanetu hadi kuwa mahututi vile. Nami nilitamani kutoa machozi kumlilia mwanangu, lakini nilijikaza kisabuni, nikaacha kabisa kufikiria juu ya ushauri wa Shomeho kutaka twende kwa mganga.
Usiku ule sikupata usingizi mawazo yalikuwa mbali huko nisikojua. Mama Salma na mgojwa Sabrina na Salma dada wa Sabrina walilala sebuleni, mimi nilijiegesha chumbani kwangu nisipate hata lepe la usingizi. Dakika zilizidi kwenda mbio, masaa nayo yakayoyoma huku nikiwaza nifanyaje mwanangu apone. Sikutaka kuendelea kufikiria juu ya ushauri wa Shomeho kuhusu kwenda kwa mganga wa kienyeji kuagua kwani nilikuwa sijawahi kufanya hivyo, ukizingatia mimi nilikuwa nimesoma seminarini ambako walitukanya kabisa mambo ya kuwategemea waganga wa kienyeji.
Ulikuwa ni usiku mtulivu kabisa, kulikuwa kimya kabisa zilisikika tu sauti za vyura wakilia kwa mbali sana. Ukimya huu ulianza kunishawishi nisinzie. Macho yalianza kuwa mazito, kope zikaanza kunifunga na kufunguka kwa taabu. Usingizi ukanikuda roba nami nikashindwa kupambana nao nikalala.
Nikiwa usingizini nilishitushwa na sauti za bundi wawili waliokuwa wakipiga kelele kwa kupokezana. Bundi hao walikuwa juu ya paa la nyumba yetu mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia mwa nyumba. Nikiwa bado usingizini niliwasikiliza vizuri huku moyo ukidunda kwa nguvu na mapigo ya moyo yakiwa yanaenda kasi ajabu. Nikapiga moyo konde, nikajivika ujasiri, nikajikaza kisabuni, kwa ujasiri nikaamka kitandani nikashuka nikavaa ndala zangu kisha nikaanza kutoka taratibu kuelekea mlangoni. Nilifika mlangoni huku nikipapasa maana ilikuwa ni giza tupu mle chumbani. Nikafungua mlango wa chumba changu taratibu kisha nikatokea sebuleni. Pale sebuleni kulikuwa na mwiko mkubwa ambao mke wangu alikuwa akiutumia kukorogea pombe ya machicha aliyokuwa akikorogea kwenye pipa, basi nikaubeba ule mwiko, nikaanza kutoka nje, nikafungua mlango taratibu ili nitoke nje. Nilipofika pale nje niliweza kuwasikia vizuri wale bundi na hakika walionekana kuwa jirani kabisa na mimi japo nilikuwa siwaoni. Nikanyanyua ule mwiko kisha nikaubamiza kwenye bati ya nyumba yangu, mara wale bundi walinyamaza maramoja. Nikabonda mara ya pili nikasikia wakipeperuka na kwenda kutua kwenye mti fulani uliokuwa jirani na nyumba yetu na ambako walikuwa wanalala kuku wa Ndeluvale. Huko wakaendelea kupiga kelele kwa kupokezana kama mwanzo. Nikaamua kuzunguka huko huko kisha nikarusha ule mwiko, nao wakatoweka hawakusikika tena. Basi nikaanza kurudi na kabla sijaenda chumbani nkaamua niingie jikoni nione mgonjwa anaendeleaje. Chaajabu nilipoingia mlangoni nilinusurika kumkanyaga nyoka mkubwa ambaye alikuwa anatoka mle jikoni. Nilishituka ghafla, nikaingia ndani kwa haraka huku nikiwa nahema kama mwanariadha. Waliokuwepo mle ndani jikoni walinishangaa hali niliyokuwa nayo kwa wakati ule. Nikajaribu kuwahadithia jinsi nilivyopishana na yule nyoka mkubwa mlangoni hawakunielewa, walinibishia wakasema wao walikuwa macho mle ndani hawakuona hata dalili ya kuwemo nyoka mle jikoni na moto ulikuwa unawaka na taa ilikuwa inamulika chumba kizima. Nikaamua kunyamaza maana ni mimi pekeyangu niliyekuwa nimeona sikuwa na shahidi mwingine. Hali ya mgonjwa kwa wakati ule ilikuwa ya kawaida. Mgonjwa alikuwa mnyonge, amepoa anahema kwa mbali. Sikutaka nimsumbue sana, nikawaacha wanakesha nikawaaga nikarudi chumbani kulala. Niliingia chumbani nikafunga mlango kwa ndani nikajilaza kitandani. Nililala chali macho yangu yakitazama juu aliko muumba. Baada ya muda nikajikuta katika sala nikimwomba Mungu amponye mwanangu. Nilisali hivi: Ewe Mungu muumba wa vyote. Wewe wajua kulala kwangu na kuamka kwangu, wewe wayajua matatizo yanayonikabili mimi mtumishi wako nisiye hata na thamani machoni pa walimwengu, naomba unipe thamani mbele yako. Ulinijalia makuu nikashangilia nikasherehekea nikifurahi. Hata hivyo sikukusahau wewe uliye muweza wa yote. Tazama Bwana, mwanangu Sostenes uliyenijalia wewe mwenyewe sipo nae tena. Alinitoka nikaomboleza natumaini sasa umempumzisha mbinguni mahali pa raha. Tazama nimegubikwa na pigo jingine tena Bwana. Mwana Sabrina yu hoi kitandani. Binti yangu hajiwezi, nimehangaika na bado nahangaika ili mwanangu apate ahueni niendelee kuweka matumaini yangu kwake. Naomba umponye mwangu, ili aendelee kuhesabika katika idadi ya wanangu ulionijalia…” Sala yangu haikuisha huku nikiendelea kusali, usingizi ukanivamia taratibu kisha ukanikuda roba nikaanza kusinzia. Ghafla nilisikia yowe ya msiba ikitokea jikoni. Kwa mara ya kwanza nilihisi niko ndotoni labda ninaota yale mazishi ya mwanangu Sostenes. Ilipopiga mara ya pili na ya tatu niligundua kuwa  haikuwa ndoto tena. Niliweza kuisikia sauti vizuri ikitokea jikoni. Niliposikiliza vizuri niligundua ilikuwa ni sauti ya Mama Salma na binti yangu Salma. Moyo uliniuma, nikatamani kumlaumu Mungu na kumwuliza kama nilikuwa nakosea kuomba amponye mwanangu hata akaamua kuichukua roho yake kabisa. Nilishindwa kuinuka kitandani, nikajikunyata nikalia masikini mimi, nikanawa machozi uso mzima. Nikajipigapiga masumbwi, nikajiona sifai kitu duniani hapa nikatamani kama na mimi nijifie niongozane na mwanangu huko mbinguni alikotangulia.
Zile yowe zilitosha kabisa kuwaita majirani. Mke wa Mzee Ndeluvale alikuwa wa kwanza kujumuika nasi kuomboleza kifo cha mwanangu Sabrina. Kwakuwa kulikuwa karibu kunapambazuka majirani wengi walianza kumiminika pale msibani. Ndugu na majirani walitaarifiwa juu ya tukio hilo nao wakaja kujumuika nasi. Maandalizi yalifanyika, watu walikula wakalala, maombolezo yakafanyika. Siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya mazishi ya mwangu Sabrina.
Siku ilipofika maiti iliandaliwa vizuri, mwili wa mwanangu kipenzi sasa ukafungwa kama pipi ndani ya sanda na kupangwa ndani ya jeneza dogo lililolingana na mwili wake. Ukafika muda wa kuaga maiti ya mwanangu. Nikajikaza kisabuni, nikalisogelea jeneza na kuitazama sura ya mwanangu Sabrina kwa mara ya mwisho. Machozi yalinitoka, mwili nilihisi umelegea kanakwamba ningehitaji mtu anishikilie nisidondoke lakini nilijikaza kisabuni nikayahimili maumivu. Wakati huu wa kumwaga mwanangu, Salma dada wa marehemu alizimia hakuweza kushiriki kuuaga mwili wa mdogowake. Mama Salma naye kwa  kushikiliwa na wanawake wenzake aliweza kushiriki hatua hii ya kumuaga mwanae wa pili. Tukio hili lilipokamilika, jeneza lilibebwa na maandamano kuelekea makaburini yakaanza mara. Tulipofika makaburini, katekista alituongoza katika sala ya mazishi, kisha mazishi yakaendelea.
Pale mwili wa mwanangu ulipotumbukizwa ndani ya kaburi nilitamani kama vile na mimi ningeingia ili twende pamoja huko alikokuwa anaenda, lakini haikuwa rahisi. Machozi ya uchungu yalinitoka yakachuruzika mashavuni mwangu hadi kudondoka chini. Makamasi nayo yakaanza kuchungulia puani mwangu kama vile yalitaka kushuhudia mazishi, ila nikayafuta kwa leso yangu. Nilimlilia mwanangu Sabrina hata nikamkumbuka na Sostenes mdogo wake Sabrina aliyetangulia kututoka. Nilivyoendelea kutazama nilitamani kama wale watu waache kufukia lile kaburi wasubiri labda mwanangu ataamka lakini ndo kwanza walianza kushindilia kaburi kwa nguvu kwa kutumia miguu. Niliona kanakwamba walikuwa wanafurahia kifo cha mwanangu. Lakini haikuwa hivyo bali ni taratibu za mazishi yote kushindilia kwa nguvu vile.
Mazishi yakamalizika, kama kawaida mtangazaji alitangaza kuwa watu wote warudi nyumbani kwa wafiwa ili wakanawe mikono. Basi watu wakaanza kurudi nyumbani nami nikaungana nao, nikaanza kuondoka taratibu huku nikiwa nimeshika leso mkononi nikifuta machozi yaliyokuwa yakinimiminika mashavuni mwangu. Nilipofika nyumbani nikapitiliza moja kwa moja chumbani na kujilaza chali kitandani. Mawazo yalinihama kabisa. Hakuna kingine nilichokifikiria zaidi ya mwanangu Sabrina, tena mawazo haya yakanipelekea kumuwaza mwanangu Sostenes alikuwa ameanza kusahaulika moyoni mwangu. Baadaye nilihisi kusinzia usingizi ukanichukua kwa muda nikalala. Nikaanza kuota ndoto mchana ule pale kitandani nikiwa nimejilaza chali. Niliposhituka niliweza kukumbuka kuwa katika ndoto yangu, kulikuwa na mtu mmoja ambaye namfahamu kabisa, alikuja nyumbani kumwulizia mwanangu Sostenes nikamwambia alishafariki, akaniuliza Sabrina yuko nikasema kaenda shuleni, yeye akaniambia kuwa atakaporudi atakuja kumchukua. Mimi nilipotaka kumwuliza kuwa alitaka kumpeleka wapi sauti haikunitoka, yeye akaanza kuondoka, nikataka nimwite asubiri tuzungumze ila hakuitika wala hakugeuka kunitazama. Nilitamani nisimame nimfate sikuweza miguu ilikuwa mizito kabisa sikuweza hata kuinuka. Nilivyoendelea kuita ndivyo alivyozidi kuondoka na kwenda zake.
Niliposhituka kutoka usingizini niliifikiria sana ndoto yangu ila sikupata jibu. Niliangalia saa ya mkononi nikakuta ni saa kumi na moja jioni. Nilivyoinua macho mlangoni nikakuta mlango unafunguliwa. Kumbe alikuwa ni Daudi mdogo wangu akiniita niende nikale. Basi bila kusita nikainuka nikaongozana naye ili nipoteze mawazo juu ya wanangu niliokuwa nimwapoteza. Nilikula chakula kisha nikarudi kulala tena. Nilianza kuhisi upweke wa nafsi kwa kuwapoteza wanangu wawili. Nilikuwa nimebakiwa na mwanangu mmoja Salma na mama yake tu. Nafsi iliniuma, nilijaribu kujiuliza na kujihoji kwanini mimi yalinikuta haya. Lakini niliishia kujisemea `huenda ni mpango wa Mungu tu, nilijifariji kwa kudhani labda alikuwa na mpango na mimi`. Nililala usingizi mzito siku hiyo sikushiriki kuimba nyimbo za misiba walizokuwa wanaimba watu usiku ule. Sikujua kama waliimba ule wimbo wa TWIWALALA na kwenda makaburini kama tulivyomfanyia mwanangu Sostenes. Nililala fofofo nisijue kilichoendelea usiku ule. Mama Salma naye alilala na wanawake wengine ndungu zetu waliofika kuomboleza pamoja nasi.
Usiku ukaisha, kukapambazuka na siku mpya ikawa imeanza. Ndugu wengine walianza kuondoka na kurudi kwao. Lakini siku ile ya pili baada ya mazishi ya mwanangu Sabrina ndugu wote tulikusanyika na kufanya kikao cha ukoo. Katika kikao hicho baadhi ya ndugu walishauri twende tukaague ili tujue ni nini kilichotukumba hadi tunawapoteza wanetu kiasi kile. Walisema tukatafute huenda kuna mbaya wetu hatutakii mema. Mimi binafsi sikuwa tayari kukanyaga kwa mganga. Nilikataa nikasema kuwa haya yote yalikuwa yanatokea kwa mpango wa Mungu. Hatukufikia mwafaka wa kwenda kwa mganga au kutoenda maana mimi nilikataa kabisa kukanyaga kwa mganga. Mke wangu hakuwa na la kusema alikuwa akinisikiliza mimi kama ningekubali kwenda kuagua.
Kikao kilimalizika ndugu wakatawanyika nasi tukaendelea na maisha tukiomboleza kwa kuwapoteza wanetu wawili. Sasa Salma alibaki peke yake wa kwenda shuleni na kurudi kusaidia kazi nyumbani. Bila shaka aliwakumbuka sana wadogo zake, lakini wasingeweza kurudi tena. Mimi na mke wangu Mama Salma tuliendelea na shughuli zetu. Baada ya kuomboleza kwa muda mrefu tuliendelea na shughuli zetu za shambani, kulima na kuvuna.
Mwanetu pekee aliyesalia, Salma aliendelea na shule. Yeye ndiye aliyebaki kuwa tegemeo letu pale nyumbani. Tulimpenda sana na tukamtunza kwa umakini na kumpa mahitaji yote aliyoyataka kadiri ya uwezo wetu. Tulimhamisisha mwanetu akazane kusoma kwani tulimtegemea kuwa ndiye ambaye angetutunza tutakapokuwa vikongwe nguvu zitakapotuishia hatuwezi kufanya kazi tena. Tulimpenda sana mwanetu. Nyumbani kulikuwa kumepoa na kila mtu aliyepita kutusalimia alihisi utulivu kanakwamba tulikuwa tumehama kumbe bado mimi, mama salma na Salma tulikuwepo.
Katika maisha yetu hatukusahau kusali sala za pamoja kila jioni na kuwaombea wenzetu ambao walikuwa wametutangulia kwa mwenyezi wakiwa bado watoto. Tulisali kila siku jioni tukipeleka shukrani na maombi yetu kwa mwenyezi aliye asili ya kila lililo jema. Wakati anafariki Sabrina aliyekuwa kidato cha kwanza, huku Salma alikuwa kidato cha pili. Siku zikazidi kusukumana, zikakimbizana zikaenda mbio nazo zikamalizika mara tukakuta binti yetu yupo kidato cha nne. Kwa hakika sasa alikuwa ni binti kweli wa kutazamwa mara mbili na wavulana aliopishana nao. Kama wazazi tulitambua hilo hivyo tulikuwa makini mwanetu asiharibikiwe maisha. Tukamfunza siri za maisha na mbinu za kufanikiwa. Tukampeleka sasa akae bwenini ili atulie ajiandae vizuri na mitihani.
Miezi ikayoyoma akakaribia kufanya mtihani wa taifa akiwa mzima na afya safi. Tukamsihi mwanetu akazane kusoma ajiandae vizuri na mitihani. Ikatangazwa siku ya mahafali naye akatujulisha, basi tukajipanga tukamshonea nguo nzuri. 
Siku ya mahafali ilipofika mimi na Mama Salma tulienda kumshangilia na kumpigia nderemo mwanetu. Tulimbebea zawadi kedekede na mazaga ya kutosha. Tulipiga na picha za ukumbusho huku tukiwa tumemvalisha mataji  mengi yamemjaa shingoni. Tulikula tukampa zawadi nyingi sana. Tukamsihi sana ajiandae vizuri na mtihani wa Taifa.
Hatimaye siku ikafika mwanetu akaingia kwenye chumba cha mtihani.
Aliyazingatia tuliyokuwa tumemfunza akafanya mtihani wake kwa utulivu, hata mitihani yote ikaisha na akarudi nyumbani kama mhitimu. Tulimpokea kwa furaha na bashasha tukamchinjia na jogoo ale ajinome mwanetu kipenzi.


 ~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~~

SURA YA TATU

Shamrashamra za mahafali ya mwanetu kipenzi zililipomalizika tukaendelea kuishi pamoja nyumbani na yeye akishiriki kazi za shambani, kwani alikuwa anaweza kufanya shughuli hizo na ndizo shughuli pekee zilizotuingizia kipato ndani ya nyumba. Mwaka ule mwezi ule wa kumi alipokuwa ametoka tu kuhitimu kidato cha nne tulikuwa tunafanya kazi ya kuandaa mashamba ya kulima mwaka ule. Tulikuwa tumeandaa mashamba mawili makubwa ya viazi na yakakamilika tukapanda kisha tukaanza kuandaa mashamba ya kulima ili tupande mahindi. Hili shamba tulianza kulifyeka mapema kwani lilikuwa ni shamba jipya na ni mara ya kwanza kulilima. Tulifyeka tukamaliza ndani ya wiki mbili. Baada ya nyasi kukauka tukachoma moto kisha tukaanza kulima. Tukalima kwa juhudi sana. Tulikuwa tunajihimu mapema asubuhi huku tukijifungasha kande au viazi vitamu kwenye kikapu vya kula shambani. Tulirudi jioni sana tukiwa tumechoka. Nilikuwa nikimtazama mwanangu akiwa mchovu namwonea huruma lakini hakukuwa na namna maana ilitupasa kufanya hivyo ili siku ziende na familia yetu isiwe ombaomba. Baada ya wiki tatu tulimaliza kazi ya kulima shamba hilo. Tulipomaliza kulima shamba hilo tuliamua kupumzika siku tatu mfululizo bila kufanya kazi yoyote ya shamba.
Baadaye tuliamua kuanza kuandaa shamba jingine ambalo mwaka wa nyuma yake tulikuwa tumelima mahindi hivyo kulikuwa na mabuwa ya kufyeka na kuchoma moto kisha kulima.
Sasa ilikuwa ni mwezi wa kumi na moja. Tulifyeka kwa muda wa wiki moja na ile sehemu iliyobaki ilikuwa ya kumalizia kwa siku moja. Siku hiyo tulijihimu kama tulivyozoea kujihimu tulipokuwa tunalima shamba lile la kwanza ambalo lilikuwa jipya. Siku ile tulijihimu tukabeba mayao kama chakula chetu cha mchana kwenye kikapu. Tulipofika tukakiweka pembeni ya shamba chini ya mti uliokuwa na kivuli kizuri. Kisha kila mmoja akashika jembe lake na kazi ikaendelea. Zilipita dakika chache, haikufika hata saa moja, mara Salma alikurupuka kwa mshituko akatupia jembe pembeni huko akaanza kukimbia kimbia huku akiita `mamaaa mamaaaa`. Akarukaruka kisha akaanza kukimbia kuelekea alikokuwa mama yake. Mimi kwa mshangao na kwa kuhamaki nikamwambia Mama Salma `Mwangalie mtoto huyo kuna nini`. Salma alipofika kwa mama yake akajitupa chini na kuendelea kulia kwa sauti bila kusema shida ilikuwa nini. Alilia akigaagaa na kujitupatupa maskini binti yangu Salma.Tukajaribu kumshika lakini alifurukuta kiasi cha kutushinda nguvu mimi na Mama yake..........................

KALIA KIGODA MWANAKWETU WEYE, MAMBO BADO!!!!!!!!!!!!!!!!!!

 ^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^^
BILA KUCHELEWA ANZA KUWEK ODA YA KITABU CHKO KWA BEI RAFIKI



2 comments:

NITAKUPENDA DAIMA

Mtunzi: Elias Kalistus Mwalongo Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Ruaha(RUCU) Simu: 0769313224 ____________ Laazizi wangu wa moyo, nat...